Wiki hii baadhi ya waandishi na wachambuzi wa wa habari michezo tulipata fursa isiyo rasmi kujadiliana na kocha Meja Mingange kuhusu mustakabali wa soka letu kupitia kundi sogozi. Lakini majadiliano hayo ya kujengeena uwezo yalileta hoja ambazo zinafaa kuwafikia viongozi na wadau wa sekta ya michezo. Kocha Mingange amepata kuzifundisha timu mbalimbali za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara pamoja na zingine za Ligi Kuu Zanzibar.
Makala haya yanaeleza maono yake namna ya kupata mafanikio katika mchezo wa kandanda. Kuanzia michango ya nafasi ya viongozi wa serikali, mashirikisho ya soka, wadau, makocha, wachezaji, wataalamu wa afya na vyakula na mashabiki ambao mchango wao utaweza kuleta tija kwa taifa.
UWEZO WA WACHEZAJI NA MBINU ZA MAKOCHA
“Kiwango cha soka letu linaonekana kuamuliwa au kubebwa na matokeo ya Simba na Yanga. Wengi wanaamini ubora wa Taifa Stars unatokana na timu hizo kongwe, lakini hata hizo zinabebwa na wachezaji wa kigeni. Tumeona pasipo Meddie Kagere Simba hawapati matokeo mazuri. Wachezaji wetu wengi hawana uwezo wa kuelewa ‘tactical’ na ‘technic’ za makocha kwa sababu hawana msingi wa kufundishwa academy kuelewa mambo ya msingi katika mpira.
“Tunataka kushinda na kujilaumu kwa vitu ambavyo sio vya kiwango chetu. Wapo wachezaji Taifa Stars wamedumu miaka mitano hadi sita, lakini kwanini kiwango chetu kinabaki sehemu moja? Tuna changamoto ya kuwa na wachezaji wanaong’amua mbinu za mwalimu, hili linatakiwa kufanyika tangu wakiwa wadogo.”
TUNAKWAMA HAPA KUPATA MAFANIKIO
“Tanzania hatujafahamu tutafikaje waliko wenzetu na walifanyaje wakafika huko. Soka ni taaluma pana sana watu wasiishie kwenye kupiga pasi na mifumo tu. Kuna masuala ya kutiliwa mkazo na elimu ya kutosha kuhusu utawala (Soccer Management), matibabu, fedha, masoko, vyakula, vifaa, viwanja, matangazo, ujuzi wa makocha, shule za mpira na kadhalika,
“Sasa tuje kwenye timu ya Taifa hasa kwenye uteuzi wa wachezaji, maana naangalia nchi nyingi zinavyofanya. Nchi zote duniani kuna timu kubwa. Timu kubwa zote zina wachezaji bora sababu ni kwamba uchumi wao uko vizuri. Hapa kwetu Yanga, Simba na Azam, kwa bahati mbaya timu hizi zimesajili wachezaji 10 wa kigeni ili wafanye vizuri kwenye Ligi na Kimataifa,
“Tujiulize, je mchezaji kama Andrew Simchimba wa Azam anacheza mara kwa mara? Huyu ni nambari 9, alipokuwa timu ya Coastal Union kwa mkopo alikuwa anacheza, kwahiyo alikuwa anapata ‘match fitness’ na ‘experience’. Tuje kwa Ditram Nchimbi, nilimtoa Majimaji ya Songea kwenda Mbeya City mwaka 2015 nilimtaka kwa nafasi ya nambari 9. Msimu wa 2016/2017 alikuwa yuko vizuri sana pale Mbeya City kama mshambuliaji kiranja. Kwa sasa yupo Yanga, je anacheza nambari 9? Nini nataka kuongea, ni kwamba hakuna mpango madhubuti kuanzia kwenye klabu hata timu ya Taifa kwa ajili ya kutengeneza wachezaji.
NAFASI YA WAKURUGENZI WA UFUNDI TIMU ZA LIGI KUU
“Hayo matatizo yako pande mbili; kwanza ningemshauri mkurugenzi wa ufundi na Kamati ya Utendaji kutengeneza ‘pepa’ ikielekeza kuwa tuna shida sehemu moja,mbili,tatu. Nini kifanyike pamoja na mipango yenu ya klabu. Mambo haya yazingatiwe. Jambo la pili sidhani na siamini kama timu zetu zote za Ligi Kuu kama wana wakurugenzi wa ufundi na kama wapo kazi zao nini?
“Hawa ndiyo wenye mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Lazima mkurugenzi wa ufundi awe mtu mwenye ujuzi mkubwa kuliko hata kocha wa timu. Timu kama Simba,Yanga na Azam sio kama haliwezekani. Lakini TFF iweke kanuni kabisa kwenye Ligi kinyume cha hivyo hakuna kushiriki,
“Mbona sasa hivi wameanza kuvikomalia viwanja na kuvifungia na inawezekana, ingawa bado sindano haijaingia vizuri. Kwa mfano viwanja ambavyo viko sawa ni vitatu tu, navyo ni Uwanja wa Mkapa (Dar es salaam), Uwanja wa Azam (Dar es salaam), Uwanja wa Samora (Iringa). Watu wasiangalie picha tu hapana. Vyumba vya wachezaji, usafi wa vyoo, maji ya kutosha, hayo ni mambo muhimu,
“TFF wangekuja na msisitizo iwekwe kwenye kanuni kila mechi ya Ligi Kuu na daraja la kwanza lazima si ombi wawepo na mchezaji wa chini ya umri wa miaka 20 mmoja ama wawili. Baada ya miaka mitano mna wachezaji wengi vijana wana uwezo mkubwa. Ni jambo zito kwa viongozi wa mpira wetu ila kanuni zikiwabana na kufuatiliwa na TFF linawezekana. Binafsi nimewahi kubadilisha Opec International kutoka wazee akina Athuman Mboke namba 9 hadi Thomas Mboke baada ya miaka 4. Ni mchakato wa muda kupata matunda mazuri.”
KUHUSU NAFASI YA KOCHA WA TAIFA STARS NA SERIKALI
“Watu wengi hata waliopo TFF hawalijui hili kupata kocha wa timu ya Taifa ujue ndiye kiranja wa makocha wote wakiwemo akina Meja Mingange. Sasa tatizo utashi wa serikali sizungumzii mpira tu. Tanzania imejaliwa vipaji na uchangamfu wa wananchi wake. Hassan Mwakinyo, Dulla Mbabe, Ibrahim Class, Twaha Kiduku wangepata makocha bora kutoka huko duniani hakuna wa kutuzuia katika mchezo wa ngumi, riadha, baiskeli, kuogelea, na kila mchezo.
“Sasa tuje kwenye mada yangu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwapa TFF jukumu la kutafuta kocha wa timu ya taifa. Walipatikana makocha watatu. Wawili walitoka nchini Ufaransa, hawa walikuja kuendesha kozi za walimu wa walimu (Instructors course) nami nikiwemo mwaka 2006 ilifanyika Karume jijini Dar es salaam. Wale Wafaransa wa kwanza walitaka dola 50,000,wapewe nyumba na usafiri.
“Mfaransa wa pili alikuwepo huko Misri mwaka 2019 alienda na timu moja ya Afrika magharibi, nafikiri ni Guinea, huyu alitaka dola 30,000, nyumba na gari. Kocha wa tatu alitoka kwa wenye mpira duniani Brazil. Huyu alitaka dola 30,000 na apewe malipo ya kusaini mkataba dola 200,000 keshi, nyumba na gari. Ilishindikana akaja mtu mmoja namjua kutoka Brazil,
“Nimesema serikali haishindwi kumlipa kocha kiasi hicho cha pesa, ila nchi zinazoweza ni Benin, Guinea, Togo, kwa vile wana utashi. Kocha mkubwa kama huyo ana manufaa mengi anaweza akabadili miundo mbinu ya soka lenu. Tuna safari ndefu. Nasema Azam wanajitahidi sana ila wanatakiwa waende mbali wakiamua, na bado waweke nguvu kwa vijana, waajiri mkurugenzi wa ufundi wa maana kutoka nje watafika mbali kisoka na watawafunika hawa wazee wa kugombea wachezaji.”
Comments
Loading…