Katibu wa Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui
Mmoja wa makocha wa timu ya taifa ya riadha kutoka Cuba, George Luis Bravo amerejeshwa kwao ghafla baada ya kufunga ndoa na mwanariadha wa Tanzania, imebainika.
Bravo na Mcuba mwenzake Andres Barow walikuwa jijini Arusha wakifundisha wanariadha mbalimbali ili kuwaweka fiti kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.
Hatahivyo, habari zilizopatikana wiki hii zilisema kuwa kocha huyo ambaye mwaka jana alimuoa mwanariadha wa Tanzania anayefanyakazi katika Jeshi la Polisi, Cecilia Matee, amerejeshwa kwao kufuatia kitendo hicho.
Chanzo chetu kilisema kuwa Idara ya Uhamiaji nchini ilipokea maelekezo kutoka ubalozi wa Cuba ukiitaka idara hiyo kumuondoa nchini kocha huyo mara moja kutokana na shughuli za kikazi.
Alipoulizwa jana msemaji wa idara hiyo, Abdi Ijimbo alisema kuwa anawasiliana na idara inayoshughulikia utoaji wa vibali ili kujua kama kuna kitu kama hicho. Hatahivyo, hadi tunakwenda mitamboni alikuwa hajatoa jibu.
Akizungumza kwa simu, Katibu wa Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui alisema juzi kuwa yeye hajui alipo kocha huyo, lakini amesikia tetesi kuwa hayupo tena Arusha.
“Kwa kweli sijui yuko wapi, lakini nilichosikia ni kwamba hayuko Arusha,” alisema Nyambui ambaye ni mmoja wa viongozi wa michezo walioshiriki katika sherehe ya ndoa ya kocha huyo iliyofanyika Tabata jijini Dar es Salaam baada ya kufunga ndoa katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ilala.
Naye kocha mwingine kutoka Cuba ambaye yuko Arusha, Barow alikiri kuwa mwenzake hayuko jijini humo amekwenda Dar es Salaam kushughulikia matatizo yake ya kifamilia, huku akisisitiza kuwa hatarejea tena Arusha, bila kufafanua matatizo yaliomsibu mwenzake huyo na kusema ataletwa kocha mwingine Mcuba kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na George.
Mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini, Leonard Thadeo alisema hivi karibuni kuwa ofisi yake haina taarifa za kuondoka kwa kocha huyo kwani kama ingekuwa kweli, idara yake ndio ingeshughulikia tiketi yake.
“Sina taarifa za kuondoka kwake na kama ni kweli sisi ndio tungetoa tiketi yake lakini mbona hatuja mpa hiyo tiketi?” alihoji Thadeo.
Mwandishi wa habari hizi alimpigia simu Matee na kupokelewa na dada yake, ambaye hakujulikana jina lake mara moja alisema kuwa mdogo wake amelazwa katika hospitali ya Polisi barabara ya Kilwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa tumbo.
Hatahivyo, mwandishi wetu siku iliyofuata aliwasiliana na Matee aliyedai kuwa mumewe yuko Arusha, kauli ambayo inapingana na ile ya kocha mwingine aliyesisitiza kuwa yuko jijini Dar es Salaam na hatarudi tena Arusha.
“George yupo Arusha anaendelea na kazi na hana simu ila nikipata simu ya rafiki yake mmoja ambaye mara nyingi yuko naye, nitakupatia ili uwasiliane,” alisema Cecilia lakini hadi tunakwenda mitamboni hajatuma namba hiyo.
Hatahivyo, ofisa mmoja kutoka ubalozi wa Cuba (ambave hakupenda kutajwa jina kwani sio msemaji), alikiri kuwa kocha huyo ametakiwa kurudi nchini mwao haraka ila kinachosubiriwa ni kwa Serikali ya Tanzania kukubali kumpokea kocha atakayembadili George, kwa kuwa Tanzania ndio inamlipa mshahara.
Juhudi za NIPASHE kumpata msemaji wa Ubalozi hazikufanikiwa baada kila mara kuambiwa kuwa wako vikaoni, lakini wangewasiliana na mwandishi kwa simu, lakini hawajafanya hivyo hadi tunakwenda mitamboni.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Loading…