Tuwatakie wote kheri za 2017.
Wakati huu mwaka jana mshindi wa ligi ya England hakuwa akieleweka sawasawa. Ingawa Arsenal walichapwa 1-0 na Chelsea kati kati ya Januari 2016, na Tottenham Spurs walikuwa wakija kasi kiongozi alikuwa Leicester City. Si wengi waliokuwa wakiamini jitihada za Leicester City (“mbweha”) , ingawa hatimaye walishinda kombe la mwezi Mei 2016.
Man United haikuwa ikifanya vizuri na Man City vile vile. Hata hivyo tulitegemea Chelsea, Arsenal na Spurs kuipiku Leicester City.
Hadi sasa Chelsea imecheza mechi 13 bila kufungwa. Anayeongoza rekodi kama hii ni Arsenal – kwa kucheza mechi 14 bila kufungwa mwaka 2002, na tukirudi nyuma zaidi, Tottenham mwaka 1960, Preston na Sunderland pia mwaka 1892.
Jumamosi hii Chelsea iliwatoa Stoke City 3-0. Akichambua mechi hiyo mchezaji wa zamani wa Man United, Phil Neville alisema Chelsea wanazishinda timu nyingine kutokana na mtindo wao wa kasi na kwenda mbele.
“Mtindo huu unatokana na kocha Antonio Conte…amejaa hamasa kali.” Alisema Bw Neville.
Chelsea inafuatwa na timu nyingine yenye pia kocha aliyejaa ari Mjerumani, Jurgen Klopp. Jumamosi Liverpool waliichapa Man City 1-0. Ushindi wa Liverpool dhidi ya Man City umejenga hisia za wasiwasi kwa Pep Gurdiola anayezungumziwa na mbinu zake tofauti. Gurdiola amesisitiza kuwa hata kama hakutakuwepo matokeo sasa hivi, mbinu anazotumia haziwezi kubadilishwa.
Wengine wanaofuata ni Arsenal walioitwanga Crystal Palace 2-0 na bao la Olivier Giroud limezungungumziwa sana kama moja ya mabao ya mwaka 2017. Limelinganishwa na lile la mshambuliaji wa zamani wa Arsenal , Dennis Bergkamp, mechi ya Arsenal na Leicester United mwaka 1997. David Platt alimrushia Bergkamp pasi ya mbali. Bergkamp alimlisha mlinzi wa Leicester Matt Elliott “kanzu”, kisha akaupiga dana dana na kufyatua bao la karibu lililompita golikipa Casey Keller.
Bao lake Olivier Giroud lilitokana na pasi ya Alexis Sanchez iliyomfikia kati kati ya walinzi kadhaa wa Crystal Palace. Giroud alijipinda akauzungusha mpira na kuurusha nyavuni.
Sanaa hii imelinganishwa ya mshambuliaji Henrikh Mkhitaryan wa Man United juma lililopita alipopiga bao lililozungumziwa kipindi chote cha sherehe za Krismasi. Man United nao wameanza kuwika tena baada ya kuwanyuka Middlesborough (Boro) 2-1.
Boro waliwapa kazi sana Man United, na ingawa kocha Jose Mourinho alimwomba samahani kocha Aitor Karanka – waliofanya kazi pamoja zamani Real Madrid- Bao la Paul Pogba lililofungwa dakika 86 za mwisho mwisho, moja baada ya lile la Antony Martial (85) lilionesha kuwa Man United wanarejea enzi za mzee Alex Ferguson.
Tottehnam Spurs inayofukuzana na Arsenal katika namba tatu na nne, iliitandika Watford 4-1 – washambuliaji Delli Ali na Henry Kane walichangiana mabao mawili kila mmoja. Ingawa Watford (“manyigu”) walijitahidi kufunga bao moja la kufuta machozi, halikufua dafu.
Ligi ilivyo sasa hivi ni Chelsea – pointi 49, Liverpool 43, Arsenal 40 na Tottenham 39. Wanaofuata ni Man City baadaya kufungwa jana na Liverpool ,39 na Man United 36.
Kwa upande wa wachezaji Chelsea pia inaongoza dimba kupitia mshambualiaji Diego Costa (mabao 14) akifuatiwa na Alex Sanchez, 12, Zaltan Ibrahimovic, 12 , Romelu Lukaku , Everton -10- na Harry Kane ,10.