Mechi za Ligi Kuu ya England (EPL) Jumamosi hii zimeisha kwa mshindo, Chelsea na Manchester United wakipokea kichapo.
Mabingwa wa Ulaya, Chelsea walifurukuta kusawazisha bao walilokuwa wamefungwa na West Bromwich Albion, lakini hatimaye waliufyata.
West Brom wanaofundishwa na Steve Clarke aliyepata kuwa kocha msaidizi wa Chelsea, walimaliza mchezo kwa kuwakung’uta vijana wa Stamford Bridge mabao 2-1.
Ushindi wa West Brom waliokuwa wakifundishwa na kocha wa sasa wa Chelsea, Roberto Di Matteo umewapandisha hadi kwenye nne bora, walikopata kukaa ligi ilipoanza.
Wafungaji wa mabao ya West Brom walikuwa Shane Long na Peter Odemwingie, wakati Chelsea ilipata bao kupitia kwa Mbelgiji, Eden Hazard.
Nao Manchester United waliokuwa wakiongoza ligi, walipokonywa uongozi huo kwa kushangazwa na kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Norwich.
Huu ulikuwa ushindi wa pili tu wa Norwich msimu huu, wa kwanza ukiwa dhidi ya Arsenal ambao uliajabisha wengi.
Muuaji wa Mashetani Wekundu hao alikuwa mchezaji wao wa zamani, Anthony Pilkington aliyemzubaisha kipa Anders Lindegaard kwa kutumbukiza mpira kimiani kwa kichwa dakika ya 60.
Queen Park Rangers (QPR) wamezidi kuandamwa na mikosi, baada ya kufungwa na wanyonge wenzao, Southampton kwa mabao 3-1.
Licha ya mmiliki wa klabu, Tony Fernandes kudai ana imani na kocha Mark Hughes, ni wazi kocha huyo atakuwa na wakati mgumu kwa mwelekeo huu.
Kwa mechi ya nyumbani Loftus Road kama hii, wakicheza na timu dhaifu mfano wa Southampton, washabiki walitarajia ushindi ikishindikana sare.
Lakini waliambulia kipigo kizito, na ndiyo maana uwanja ulitawaliwa na zomea zomea tangu walivyoanza kucheza hovyo.
Msimu uliwafungukia Reading kwa kupata ushindi wao wa kwanza walipocheza na timu ngumu ya Everton. Walishinda mabao 2-1.
Everton waliokuwa na kawaida ya kuanza kufungwa kisha kujikomboa, walijaribu lakini mambo yakaonekana kuwa magumu, hata kwa Reading ambao wana kawaida ya kucheza vyema mwanzoni na kuchoka kipindi cha pili.
Manchester City waliongeza shinikizo kwa majirani wao United, kwa kuwakunguta Aston Villa mabao 5-0 na kushika usukani wa ligi.
Villa walionekana wachovu mbele ya City uwanjani Etihad, tofauti na walivyokuwa kwa Manchester United wiki iliyopita.
City waliokuwa wakichagizwa kwa mwenendo usioridhisha siku chache zilizopita, walibadilika na mabao yao yalifungwa na David Silva, Sergio Aguero mawili na Carlos Tevez mawili pia.
Brendan Rodgers wa Liverpool alikuwa kocha mwenye furaha, baada ya vijana wake kuwachakaza wagumu wa Wigan kwa mabao 3-0 nyumbani Anfield.
Mabao yote yalifungwa kipindi cha pili kupitia kwa Luis Suarez aliyepachika mawili na Jose Enrique.
Swansea walioanza ligi kwa mfululizo wa ushindi kabla ya kutetereka, walisimama kidete ugenini na kuwafunga Newcastle mabao 2-1.
Michu alikuwa wa kwanza kuzifumani nyavu, na mashabiki wa Newcastle walianza kuondoka uwanjani pale Jonathan de Guzman alipofunga bao la pili.
Hata hivyo, washabiki waliobaki uwanjani walifutwa machozi kwa bao la dakika ya 90 kutoka kwa nyota wao, Demba Ba na kufanya mechi imalizike kwa mabao 2-1.
Katika mchezo wa watani wa jadi wa London Kaskazini, Arsenal walicheka mwisho na zaidi, baada ya kuwaadhiri Tottenham Hotspurs kwa mabao 5-2.
Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Adebayor alikuwa mwiba kwa Arsenal kwa kuwafunga dakika ya 10, lakini akageuka tatizo kwake na kwa timu kwa kupata kadi nyekundu dakika chache baadaye.
Raia huyo wa Togo anayedaiwa kutaka kuondoka Spurs, alitolewa nje na mwamuzi Howard Webb kwa rafu mbaya dhidi ya Santi Cazorla.
Beki Mjerumani, Per Mertesacker alirekebisha makosa ya kusababisha bao dhidi ya timu yake kwa kufunga bao safi la kichwa dakika ya 24.
Mabao mengine ya Arsenal yalifungwa na Lucas Podolski, Olivier Giroud, Santi Cazorla na Theo Walcott.
Kocha Andre Villas-Boas aliyeunga mkono kadi nyekundu dhidi ya Adebayor, aliwasifu wachezaji wake, akisema walifanya vyema licha ya kuwa 10 muda mrefu wa mchezo.
Comments
Loading…