WAKATI mwamuzi alipopuliza filimbi ya kuashiria kumalizika kwa mchezo wa fainali kati ya Timu ya Taifa ya Ureno na Hispania ilikuwa ishara ya kumtawaza bingwa wa mashindano ya Nations League barani Ulaya. Filimbi hiyo ilikuwa na maana kubwa sana kwa nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 40 sasa alikuwa anaiwakilisha Ureno katika mashindano hayo huku akitazamwa na kaka zake waliomlea katika timu ya Taifa, Pepe Lima, Luis Figo na mastaa wengine walikuwa jukwaani. TANZANIASPORTS inakuletea uchambuzi wa matukio muhimu kwenye mchezo huo uliokuwa kivutio kwa watazamaji sehemu mbalimbali duniani. Ni mchezo ambao ulibeba taswira ya vipaji vya vinavyostaafu na vile vipya ambavyo miguu yao imebeba thamani kubwa na umahiri katika usakataji wa soka.
Ronaldo na uzee wake
Katika mchezo wa soka mchezaji akifikisha umri wa miaka 30 huwa anaitwa mzee. Mara nyingi baada ya timu huwa haziwatumii wachezaji wa namna hii. Baadhi yao kama Inter Milan ina mchezaji katika nafasi ya ulinzi Acerbi mwenye umri wa miaka 38. Luka Modric ana miaka 39 ambapo anamalizia msimu katika klabu ya Real Madrid. Nafasi pekee yenye uhakika kwa wachezaji hata wakivuka miaka 30 ni golikipa. Makipa wengi wamekuwa wakicheza hata katika umri wa miaka 35 kwenda juu wakiwemo, Gianluigi Buffon, Iker Cassilas, Edwin Van Der Sar, Manuel Nueur na wengineo.
Hata hivyo Ronaldo amefikisha umri wa miaka 40 huku akiwa ameandika rekodi ya mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga bao katika mchezo wa fainali ya mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka la Ulaya. Ronaldo alifunga bao la kusawazisha baada ya kazi nzuri ya beki wa kushoto wa Ureno, Nuno Mendes. Bao hilo lilimpa Ronaldo kuonesha ishara ya kutoa ujumbe kwa mashabiki na wadau kuwa “kuna Cristiano Ronaldo mmoja tu” kwenye kandanda duniani.
Kiwango cha Nuno Mendes
Mashambulizi mengi ya Ureno yalikuwa yanaanzia upande wao wa kushoto. Katika upande huo mapishi ya mashambulizi yalikuwa yanapikwa na Nuno Mendes, jitu jeusi lenye kazi, chenga na kiwnago cha hali ya juu. umahiri wa Mendes ulionekana katika kikosi cha PSG msimu huu ambako amefanya mambo makubwa na kuipa taji la kwanza la UEFA.
Ureno walikuwa wakitumia mbinu ya kupanga mashambulizi kutokea pembeni kushoto kutokana na uwezo mkubwa w abeki huyo kuwa na muono mzuri wa kutengeneza mabao na kufunga. Katika moja ya matukio ya kukumbuwa Nuno Mendes alipachika bao la kusawazisha kwa Ureno baada ya Hispania kutangulia kufunga kutokana na makosa ya walinzi wa kati wa Ureno. Nuno Mendes akiendelea hivi ina maana itakuwa silaha muhimu kwenye fainali za Kombe la Dunia zijazo pamoja naKombe la Dunia la Klabu litakalofanyika nchini Marekani hivi karibuni.
Makosa ya Robert Martinez
Kocha wa Ureno alikuwa anatamani kuona J. Neves akiwa uwanjani. Lakini chipukizi huyo kw asili ni kiungo wa ulinzi na ushambuliaji. Kocha wa Ureno alimpanga kama beki wa kulia mwenye jukumu la kucheza nafasi tatu kwa wakati mmoja; kwanza alionekana akicheza kama beki wa kulia, kisha winga wa kulia na kiungo wa tatu katika mfumo wa 4-3-2-1.
Nyota huyo aliyeng’ara PSG alikuwa akipata shida kukabiliana na winga hatari wa Hispania Nico Williams hivyo ikaonekana kama vile nafasi ya beki wa kulia wa Ureno ni uchochoro. Kipindi cha pili Roberto Martinez ili kutatua tatizo hilo alimwingiza mwenye namba yake, Semedo. Ujio wa Semedo uliimarisha nafasi ya beki wa kulia hali iliyosababisha kocha wa Hispania Luis De La Fuerte kumtoa Nico Williams maana alishakuwa amepotezwa vibaya mno na kukosa makali ya awali.
Miguu ya Nico,Yamal
Hakuna ubishi vijana hawa wana vipaji vya hali ya juu. kwanza ni marafiki na watani wakubwa, si ajabu ukimsikia Nico Williams kwenye mahojiano na vyombo vya habari akimwita Lamine Yamal ni mwanaharamu. Ni lugha yao ya utani wa mara kwa mara. Hata hivyo fainali hii imetuonesha namna vijana hawa wawili walivyo silaha muhimu sana kwa Hispania.
Nico Willaims anaweza kucheza nafasi mbili; winga wa kulia au winga wa kushoto, wakati Lamine Yamal anaweza kucheza winga wa kulia na eneo la kiungo mshambuliaji yaani namba 10. Katika mashindano kadhaa vijanja hawa wameonesha vipaji vyaona kuutangazia ulimwengu kuwa wana miguu yenye thamani kubwa.
Ushindani walionao wanapokuwa uwanjani ni kuifanya Hispania iwe hatari zaidi. Wanashindana wenyewe kwa wenyewe kuwa wabunifu na kupika mashambulizi hatari. Wanashindana kwa uwezo wa kupiga chenga. Wanashindana kwa kutafuta mabao na kupiga mashuti makali langoni. Wote kwa pamoja wanaweza kucheza mifumo mingi; 4-4-2, 3-4-3, 4-3-3, au 5-3-2. Ni dhahiri kwa kizazi kipya hawa ni wachezaji wa kutazamwa zaidi kwani wanaleta kitu cha kipekee kwenye mchezo wa soka. Pia ni kiwakilishi cha ubora wa vipaji kutoka Ligi Kuu Hispania, La Liga.
Wakati Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakiwa ukingoni sasa ni dhahiri kizazi kingine kinakuja kutawala soka. Katika kizazi hicho vinara wake ni Nico Williams na Lamine Yamal. Hawa ni wachezaji wa kuchungwa katika mechi zote wanazopangwa.
De La Fuerte ni tegemezi mno?
Kipindi cha pili cha mchezo wa fainali kilikuja na mbinu tofauti, Lamine Yamal hakuwa katika ubora ule wa kipindi cha kwanza kwa sababu muda mwingi alikuwa haingia eneo la hatari bali kupokea na kutoa pasi katika eneo la winga wa kulia. Tofauti na Nico Williams ambaye alijaribukupimana ubavu na Semedo. Hata hivyo swali moja tu linalotakiwa kujibiwa, itakuwaje pale Lamine Yamal na Nico Williams wanapozidiwa?
Kwa maana kwamba Hispania inawategemea sana vijana hawa, kiasi kwamba pale walipobanwa kutokana na umahiri wa mabeki wa pembeni wa Ureno ilionekana wazi wamekwama kuleta maajabu kama walivyozeleka. Je, kocha Luis De La Fuerte anawategemea mno bila mpango mbadala? Na hata walipotolewa Hispania ilibadilika kwa sababu ilirudi kwneye mfumo wa 4-4-2 kwani Alvaro Morata ndiye alikuja kuongoza safu ya ushambuliaji ambao ni wa kawaida tofauti na unapokuwa na Nico na Yamal. Katika muktadha huo unaona bayana kuna namna Hispania wanatakiwa kufanya nje ya Yamal na Nico. Wakikwama vijana hawa, timu inayumba kabisa.
Kwaheri Ronaldo
Ronaldo anaweza kumaliza dakika 90 za mchezo. Ilipofika dakika 80 Cristiano Ronaldo alionekana kuzungumza mara kw amara na kocha wake. ni wazi sasa ameanza kuridhika kuwa muda wake umekwisha na anatakiwa kujiweka pembeni. Ureno bila yeye inakosa mtu mwenye ushawishi kwenye mchezo, lakini kasi yao ya kucheza huwa inaomgezeka maradufu. Tatizo lao ni mpachika mabao pale mbele. Ureno hawana mshambuliaji wa maana licha ya kuwa na vipaji vingi katika kungo, mabeki na mawinga. Lakini namba 9 bado ni changamoto. Ronaldo huyu ameonesha sasa muda umewadia, lazima ang’atuke kwenye mchezo wa soka kama mchezaji. Na bila shaka Fainali za Kombe la Dunia zijazo mwaka 2026 zitakuwa za mwisho kwake. Kwaheri Ronaldo.

