*Manchester United wasogea taratibu
Vigogo wanaofukuzia ubingwa wa England nyuma ya Leicester wamepata
pigo kubwa, baada ya wote kufungwa na sasa wamebaki wakijiuguza
majeraha yao.
Leicester waliotangulia kucheza walibanwa kwa kwenda sare na West
Bromwich Albion Jumanne, kikawa kicheko kwa Arsenal, Manchester City
na zaidi sana Tottenham Hotspur ambao kama wangeshinda Jumatano hii
wangeongoza ligi.
Manchester United wao walikuwa na kicheko, kwani walifanikiwa
kuwafunga Watford 1-0, ukiwa ni ushindi wa nne mfululizo na
kumpunguzia shinikizo kocha Louis van Gaal. Bao la United lilifungwa
na Juan Mata katika dakika ya 83 kwa mpira wa adhabu ndogo.
Mshambuliaji chipukizi wa Man U, Marcus Rashford aliyetikisa katika
mechi mbili zilizopita kwa kufunga mabao mawili kila mchezo, usiku wa
Jumatano hii alikuwa kimya, lakini kwa upande wa Watford, Odion Ighalo
alipoteza nafasi mbili nzuri, na si ajabu kingekuwa kilio kwa timu nne
kubwa.
Rashford alibadilishana nafasi na chipukizi mwingine, Anthony Martial
kutoka Ufaransa, na ndiye alichezewa rafu na kusababisha mpira wa
adhabu uliotiwa kimiani na Mata kutoka umbali wa yadi 20.
Lakini kibao kikawageukia wababe hao watatu bila kuamini, ambapo Arsenal
walifungwa nyumbani na Swansea 2-1; Man City wakacharazwa 3-0 na
Liverpool huku Spurs nao wakipokea kisago cha 1-0 kutoka kwa West Ham.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba tayari alikuwa na hofu
katika usiku huo ambao wababe watatu walikuwa uwanjani. Arsenal
wanabaki nafasi ya tatu, wakiwa pointi sita nyuma ya vinara Leicester
waliojikusanyia 57, ila Wenger anaahidi kwamba vijana wake watarudi
vyema.
Spurs wao walipoteza fursa ya kushika usukani wa ligi na sasa wamebaki
pointi tatu nyuma ya Leicester. Spurs wana mabao saba ya kufunga zaidi
ya vinara hao hivyo wangeshinda Jumatano hii wangeukamata uongozi wa
ligi.
Spurs watakutana na Arsenal Jumamosi hii, wakionekana kutojiamini na
wanaongezewa taabu kutokana na kuumia kwa mlinzi Laurent Koscielny na
golikipa Petr Cech.
Man City sasa wamebaki pointi 10 nyuma ya vinara lakini wana mechi
moja mkononi. Wanazo pointi 47 sawa na jirani na mahasimu wao
Manchester United. Mkiani mwa ligi wapo Aston Villa wenye pointi 16
wakipewa nafasi kubwa ya kushuka daraja, kwani wanaowafuatia juu ni
Newcastle, Norwich na Sunderland, wote wakiwa na pointi 24. Swansea
wanazo pointi 30 na kwa kuwafunga Arsenal wanaelekea kwamba
watajinasua kwenye kushuka.