KILIMANJARO Stars imefufua matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano ya Chalenji baada ya kuichapa Somalia kwa mabao 3-0 mbele ya maelfu ya mashabiki wake walioingia bure kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Kili Stars wapo nyuma ya Chipolopolo ya Zambia na Intamba ya Burundi, ambazo jana zilitoka suluhu 0-0 na kufikisha pointi nne kila moja, zikiitangulia Kili Stars ambayo itamaliza ngwe hiyo kwa kazi pevu dhidi ya Burundi. Ndugu zao, Zanzibar Heroes walioanza vizuri Jumapili kwa kuilaza Sudan 2-0, wana kibarua kingine dhidi ya Ivory Coast katika mchezo wa Kundi B. Timu hiyo iliyoanza mchezo kwa kasi na kukosa nafasi lukuki, ilipata bao la kuongoza kwa penalti ya kipindi cha kwanza iliyofungwa na Henry Joseph ambaye kama Mrisho Ngassa, aling’ara katika mchezo huo. Mabao mengine ya Kili Stars yalifungwa wachezaji waliotokea benchi, John Boko aliyechukua nafasi ya Thomas Ulimwengu ambaye mbio zake zilishindwa kumsaidia baada ya kukosa mabao mengi katika mchezo huo. Naye kiungo Nurdin Bakari aliyeingia badala yaMohammed Banka aliyekuwa butu, alikamilisha ushindi kwa bao zuri baada ya krosi safi ya Ngassa, ambaye alipokea pasi ya Joseph. Katika mchezo huo, mabeki wa Stars, Kelvin Yondani na Juma Nyosso walifanya makosa kadhaa ambayo laiti Wasomali wangekuwa makini, wangeweza kupata bao kupitia mshambuliaji wake Yassi Mohammed Idrissa. Kocha Jan Poulsen alisema baada ya mchezo kuwa vijana wake walipata nafasi nyingi, lakini walishindwa kuzitumia, hata hivyo amefurahi kuona wameshinda. Alisema mchezo dhidi ya Burundi utakuwa mgumu, kwani amewaona dhidi ya Zambia, wanacheza vizuri na atajipanga kuwakabili. “Si mechi ya kubeza, Burundi nimewaona, ni wazuri, nitakutana na wachezaji wangu kuweka mkakati wa jinsi ya kuwakabili,” alisema. Naye Doris Maliyaga anaripoti kuwa Ivory Coast ambayo ilichapwa na Rwanda 2-1 imeshika mkononi tiketi ya Zanzibar Heroes kusonga mbele katika mechi ya leo. Mchezo mwingine utakuwa baina ya Rwanda na Sudan saa 8 mchana. Hata hivyo, Watanzania leo huenda wakamwona kiungo Abdi Kassim ‘Babi’ akiwa na Zanzibar Heroes aliyetarajiwa kuwasili jana saa 9.00 mchana akitokea katika majaribio kwenye klabu ya Long Tang ya Vietnam, ambayo anaichezea pia Danny Mrwanda. Kikosi hicho ambacho kinasifika kuwa na ulinzi mkali unaongozwa na nahodha wake Nadir Haroub na Aggrey Morris wakati safu ya ushambulizi ikiimarishwa na mshambuliaji mpya wa Simba, Ally Ahmed Shiboli. Ivory Coast inaundwa na chipukizi wengi na ina kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Wanyarwanda. Stewart aliiambia Mwananchi kuwa Ivory Coast ni wazuri, lakini anaamini kikosi chake ni kizuri zaidi ya hao kutokana na maandalizi waliyoyafanya kabla ya michuano pamoja na jana akiisisitizia beki yake kuwa makini zaidi ili isiruhusu mabao. ‘’Naamini itakuwa mechi nzuri, lakini ngumu kwa sababu Ivory Coast ni wazuri pia wana kasi ya mchezo,nasi pia tumejiandaa vilivyo kuona tunakabiliana nao,’’alisema kocha huyo. |
Comments
Loading…