Timu ya Kilimanjaro Stars ya Tanzania leo ilivuliwa rasmi ubingwa Kombe la Afrika Mashariki na Kati Cecafa baada ya kutandikwa magoli 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kilimanjaro Stars ilikubali kuvuliwa ubingwa katika mechi ya nusu fainali licha ya kujikakamua kwenye mchezo wa robo fainali ambapo iliifunga Malawi goli 1-0.
The Cranes ya Uganda ndiyo iliyoidondosha chini Taifa Stars kwa na kufanye iungane na Rwanda iliyoichabanga Sudan kwa magoli kama hayo na kutinga fainali pia.
Kwa matokeo hayo Tanzania nasubiri kuambulia ushindi wa tatu ama patupu katika mchezo utakaofanyika Jumamosi kabla ya fainali yenyewe.
Mshindi wa kwanza atazawadiwa dola za Marekani 30,000 wakati wa pili atapata 20,000 na wa tatu dola 10,000.
Kipigo kwa Kilimanjaro Stars kiliendeleza mtindo wa timu za Tanzania kusindikiza michuano ya soka katika Bara la Afrika baada ya timu nyingine ya vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes kuondolewa kwenye michuano ya vijana wa aina hiyo iliyoshirikisha nchi 10 chini ya Usimamizi wa Shirikisho la soka la nchi za Kusini mwa Afrika Cosafa.
Hata hivyo, Kilimanjaro Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Mrisho Ngassa ,mshambuliaji mwenye kasi aliyepachika goli baada ya kumnyang’anya mpiga kipa wa Uganda.
Lakini Uganda ilijibu pigo hilo dakika ya nane ya kipindi cha pili kupitia kwa Andrew Mwesigwa aliyefunga goli kwa kichwa.
Timu ya Tanzania ambayo iliingia kwenye robo fainali kwa ndondokela ilifanikiwa kumaliza dakika 90 kwa sare ya goli 1-1.
Ndiposa muda wa nyongeza ulipoanza na katika dakika ya saba ya kipindi cha kwanza Emannuel Okwi wa Uganda alipachika goli lingine kwa kichwa na lingine lilipatikana kwa penati.
Okwi ambaye anachezea timu ya Soka ya Simba hakuona aibu kumfunga golikipa wa Simba Juma Kaseja ambaye kwa mechi hiyo alikuwa langoni akidakia Kilimanjaro Stars.
Kuhusu mechi ya kwanza, Rwanda ilifanikiwa kuitandika Sudan magoli 2- 1 katika mchezo mkali uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Itakumbukwa kwamba Rwanda iliingia robo fainali baada ya kuichapa Zanzibar magoli 2-1 pia wakati nayo Sudan iliivurumisha Kenya magoli 2-0.
Comments
Loading…