.
Kweli tuko tayari kucheza na Real Madrid?
. Alifu hatujamaliza tunataka kuhitimu?
. Kuialika Real Madrid ni uvivu wa kufikiri…
Mimi ni mmoja ya Watanzania waliopatwa na furaha kusikia kuwa Rais Jakaya Kikwete akitamka kuwa kuna mipango ya kuialika timu ya Real Madrid ya Uhispania kuja kucheza nchini Tanzania.
Nafikiri tuliofurahi tuko wengi kwa sababu kadhaa lakini zikiwemo zile za kujua utukufu wa timu hiyo katika medani ya soka duniani, na jinsi timu hiyo ilivyo na wachezaji wenye majina makubwa.
Hiyo ni mbali ya uwezo wa kifedha na kibiashara iliyonayo timu hiyo, ambayo hakuna ubishi wowote ule ndio timu tajiri kuliko zote na hadi hivi sasa ikishikilia kuwa na rekodi ya kuwa ndio timu tajiri kuliko zote duniani.
Kutokana na utajiri wake, siku zote Real Madrid hutaka wachezaji walio bora ulimwenguni na ndio maana wakati mmoja ikathubutu kumnunua Zinadine Zidane kwa mabilioni ya shillingi za Tanzania na rekodi hiyo ikiwa bado haijavunjwa na timu yoyote ile duniani.
Kwa mpenzi wa soa nje ya Uhispania kwenda Bernabou, uwanja wa Real Madrid wakati wa mazoezi ni karibu ya pepo ya dunia na sikwambii kwenda wakati wa mechi itakuwa na raha ya kiasi gani.
Na iwe wachezaji wa sasa akina Ronaldo, Robinho, Beckham, Roberto Carlos na wengine hawapo hapo Real Madrid itapokuja Tanzania, lakini hao watakao kuwepo wakati huo basi watakuwa ni wa kiwango cha sawa na hao.
Ingawa kwa sasa timu ya Real Madrid inapita katika kipindi kigumu kimchezo. Pamoja na nyota lukuki ilionao, lakini inasaka mafanikio katika ligi ya ndani na sikwambii kwenye ligi ya Ulaya. Kocha baada ya kocha amefukuzwa, lakini wapi.
Kinyume na timu nyingi za Ulaya, Real Madrid haijaitambulisha sana na mpira wa Kiafrika kwa kuchukua wachezaji nguli wa Kiafrika. Ni timu ambayo bado haijaona uhodari wa wachezaji wa Afrika kama zilivyo timu nyingi za Ureno, Uingereza, Uholanzi na hata timu nyengine za Uhispania ambapo wachezaji kama Ben McCathy wa Afrika Kusini waliwahi kuchezea.
Taarifa ya Rais Kikwete ilikuja alipozungumza na waandishi wa habari na huku tukiwa tumetangulia kumuona akikabidhiwa jezi yenye jina lake wakati alipotembelea uwanja wa Real Madrid akiwa safarini kwenda zake Ulaya.
Lakini kusema kuwa nina furaha haina maana kuwa sina masuali ya kuuliza juu ya mualiko huo au tuseme ziara tarajiwa ya timu hiyo ya Real Madrid kuja ndani ya Bongo yetu, ikiwa mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa.
Nianze na hili la mambo kwenda kama inavyotrajiwa. Ziara hiyo imenitia shaka kwa Kikwete kusema kuwa kuja kwa Real Madrid kutategemea na kupata ufadhili ili kuweza kukileta kikosi hicho. Nina shaka.
Shaka yangu ni kuwa sifikiri kuwa tuna uwezo wa udhamini wa kuileta timu kama Real Madrid, kwa sababu sijui kuwa Kikwete anajua kwamba dhana nzima ya udhamini nchini Tanzania bado ni changa mno na mfano mzuri anaweza kuuona katika hizi harakati za kuiunga mkono Taifa Stars.
Real Madrid ni timu ambayo dau lake ni kubwa kupita kiasi. Kila mchezaji ana kiwango chake kinachoitwa “appearance fee” au fedha za kuitokeza mbali ya gharama ya hoteli ya nyota tano na msafara mzima ukiafiri daraja la kwanza .
Sitaki wala siwezi kukisia lakini naona gharama itayokuja kuhitajika inaweza ikaonekana ni kufuru kwa Watanzania. Sisi tuna taarifa kuwa Kikwete aliziona nyingi mno fedha ambazo zingehitajika kumlipa kocha wa Kibrazil wa Taifa Stars, Marcio Maximo, na ndio maana ujio wake ukachelewa sana. Sasa fedha ya Real Madrid ndio itayokujwa kishindo.
La, pili inaonekana Kikwete ama haelewi vyema au hakupata ushauri mzuri alipotoa ombi kwa Real Madrid kuja kwao kuwe mwezi wa Februari wakati wa kutarajiwa uzinduzi wa uwanja mpya wa taifa. Nimesema hivyo kwa sababu mpenzi wa soka na mfuatliaji anatarajiwa kujua kuwa mapumziko ya soka Ulaya ni kilele cha baridi mwezi wa Disemba au baina ya Julai na mwisho wa Agosti.
Hili la kupumzika wakati wa Disemba ni baadhi tu ya nchi za Ulaya, lakini la ziara za timu za vilabu vya Ulaya kufanywa wakati baada ya kumalizika msimu na kabla ya kuanza mwengine, ndio linalotumika kualika timu. Ziara nyingi ni wakati huo.
Hiyo haina maana kuwa ni sawa kwa timu za taifa, la. Tofauti na vilabu basi timu za taifa zinafuata ratiba inayotolewa na Shirikisho la Mpira Miguu Duniani FIFA, ambapo humo ndimo mataifa hutafuta mechi za kucheza na mataifa mengine.
Kwa maneno mengine ingekuwa kutafuta timu kusadifu na ufunguzi wa uwanja, basi Kikwete angetakiwa atafute timu ya taifa kuweza kuja wakati ligi za nchi zinaendelea, lakini kufanywe utafiti ni tarehe zipi ratiba ya FIFA inaruhusu ndani ya hiyo Februari yenyewe, lakini yawezekana haitakuwa Februari 5.
La tatu, kama Kikwete angekuwa ameshauriwa katika hili, pengine nchi isingegharimika au kuhangaika kutafuta wadhamini kuileta Real Madrid iwapo timu hiyo ingealikwa kupiga kambi yake ya mazoezi nchini Tanzania hapo mwakani na sio kuja tu na kucheza mechi.
Mimi naamini kama Real Madrid kuja Tanzania kutawawezesha pia kucheza mechi moja Afrika Kusini, hiyo itakuwa ndio njia njema ya kuwashawishi kucheza nchini kwetu. Na kusema kweli kwa wenzetu wa Afrika Kusini zipo klabu zenye uwezo wa kucheza na Real Madrid kama ilivyotokezea karibuni wakati wa ziara ya Manchester United.
La nne, kwangu mie ni kwa nini iwe ni Real Madrid? Suala hili limenitaabisha sana. Maana sijui kigezo cha kuichagua timu ya Real Madrid ni kipi, au kwa kuwa fursa tu ya kupita Uhispania ilitokezea?
Kuileta Real Madrid Tanzania maana yake ni kuwa icheze na timu ya taifa ya Tanzania peke yake na tusibaki tukidanganya kuwa timu nyengine yoyote inawez ikacheza nayo seuze kuwa wao wenyewe wanaweza kuwa wana nafasi ya kucheza zaidi ya mechi moja wakiwepo nchini.
Suala linakuja jee tutafaidika kiasi gani na ziara ya mechi moja ya Klabu, hata Klabu hiyo iwe ni kubwa kabisa duniani? Fedha ambayo itatafutwa kuidhamini Real Madrid, kama hoja ni kuleta vilabu, kwanini zisiweze kutumika kuleta vilabu vyengine vitatu au vinne kuja kucheza Tanzania, ambavyo vilabu kama hivyo hadhi zao hazitazuia kucheza na vilabu vyetu kama Simba na Yanga?
Real Madrid karibuni ilialikwa Saudi Arabia, matokeo yake? Matokeo yake ni kuwa Saudi Arabia ilifungwa magoli 8-0 na wachezaji wa timu hiyo walisema dakika 90 ilikuwa ni kama kutwa nzima.
La tano, ambalo linafuatia hoja hiyo hapo juu, ni kuwa Tanzania bado inaweza kufaidika kuzialika timu kubwa za Taifa za Afrika ambazo ziko sana mbele yetu na ambazo tungezialika ingekuwa vyema zaidi kuliko kwenda kufuata jina kwa Real Madrid.
Timu kama zilizoingia Kombe la Dunia mwaka huu za Ghana, Angola, Tunisia, Togo na Ivory Coast na timu kama za Cameroon, Nigeria, Zimbabwe, Afrika Kusini hapana shaka zinaweza kutupa changamoto ya kimchezo na uwezo wa wachezaji wetu kuonekana na sio kwa kucheza na “bwamtimu” kama Real Madrid.
Tunapozialika timu ambazo ziko mbele kisoka kuliko sisi ina maana kiwango chetu katika orodha ya FIFA kinapanda. Kwa mfano Tanzania ilikuwa nafasi ya 165 mwezi wa Julai, lakini mechi zake mbili tu dhidi ya Rwanda iliposhinda bao 1-0 na 2-1 dhidi ya Burkina Faso iliinyanyua Tanzania hadi nafasi ya 105.
Na sare ya juzi na Kenya bila ya shaka Tanzania itakuwa ndani ya nafasi 100 za orodha ya FIFA na kuiweka nchi katika nafasi ya kuonekana na kuheshimika na hivyo kupata mialiko kucheza na timu za taifa nyengine duniani.
Kwa maana hiyo hizi ndizo timu muhimu za kucheza nazo, na sio klabu ya Real Madrid kwa ajili ya kufuata umaarufu, hadhi na utajiri wake. Imekuwa kama vile mtu anataka kuhitimu wakati ndio kwanza amemaliza alifu na hilo kusema kweli ni gumu mno kutokea ingawa tunasikia kuna baadhi ya watu ambao uwezo wao wa kiakili unakuwa mkubwa kupita umri wao.
Klabu kucheza na timu ya taifa si vyema na ndio maana nadra mno kusikia Real Madrid kucheza na timu ya taifa ya Uholanzi, au Liverpool kucheza na timu ya taifa ya Uhispania, mambo hayo huyafanya wakubwa wakia huku kwetu.
Jengine, ni kuwa kuialika timu kama Real Madrid ni lazima tuwe na uhakika na suala zima la muundo mbinu. Kuja kwa timu kama Real Madrid kutakuwa na na maana kuja kwa kundi kubwa la waandishi wa habari, wafuasi sugu wa timu hiyo lakini pia watu kutoka nchi za jirani
Na wengi wa hao watakaotoka Ulaya watakuwa ni watu wenye uwezo wao wa kifedha na tabaan makaazi yao yatakuwa ni hoteli za nyota tano na nne. Je tunazo za kutosha na katika mazingira mazuri?
Linaloambatana na hilo ni uwanja wenyewe yaani ile sehemu inayochezewa mpira. Real Madrid hawachezi tu katika kila kiwanja.Wanacheza katika viwanja vyenye hadhi yao, hawajui kukosa wala kasoro ya kiwango walichokizoea.
Kwa maana nyengine suala la kuwa kualikwa Real Madrid kunatokana na kuzindua uwanja huo mpya, kwa maana ya sehemu ya kukalia, ni jambo la wazi kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha kiwanja cha kuchezea kinakuwa na aina ya majani yanayostawi Afrika lakini pia yanayoweza kukubalika na timu kama Real Madrid, ili wachezaji wa watu wasije wakachunika kana wanavyochunika wetu kila siku.
La mwisho ni kuwa dili ya Real Madrid kama itaweza kufanikishwa basi ni njia nzuri ya kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kufaidika wakati wa michuano ijayo ya Kombe la Dunia itayofanyika nchini Afrika Kusini hapo mwaka 2010.
Maana kama timu ya Real Madrid imekuja na kucheza hapa kwetu kutakuwa na sababu gani timu za kimataifa nazo zisiweze kuutumia uwanja huo?
Comments
Loading…