BAADA ya ya timu zao kutolewa kwenye michuano ya klabu Afrika na baada ya mechi za jana za Ligi Kuu ya Vodacom, wachezaji wa Simba na Yanga wanaochezea timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, wanatarajia kuingia kambini leo kujiunga na wenzao kujiandaa na mchezo dhidi ya Kenya.
Stars inajiandaa kurudiana na Kenya katika mechi ya kuwania kucheza Fainali za Afrika, kwa wachezaji wanaocheza soka katika klabu za nyumbani.
Meneja wa timu hiyo, Leopold Taso Mukebezi alisema: Wachezaji wote wako kambini isipokuwa wa Simba na Yanga ambao walikuwa wakikabiliwa na michuano ya Kimataifa pamoja na mechi za ligi, kesho (leo) wanaripoti, alisema.
Wachezaji wa timu hiyo wanaokipiga Yanga ni Amir Maftah, Nadir Haroub ,Cannavaro, Fred Mbuna, Mrisho Ngassa, Jerry Tegete na Abdi Kassimu wakati Simba ni Emmanuel Gabriel, Henry Joseph, Kelvin Yondani na Ulimboka Mwakingwe.
Meneja huyo alisema kuwa, baada ya wachezaji hao kuripoti kambini Kocha Mkuu wa timu hiyo Marcio Maximo atafanya mabadiliko kwa ajili ya mechi za Jumamosi dhidi ya Kenya.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Kenya, Stars ilijikuta ikichapwa bao 1-0 na Harambee. Endapo Stars itashinda mchezo huo, itapambana na mshindi kati ya Uganda na Eritrea.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Frederick Mwakalebela alisema kuwa, waamuzi watakaochezesha pambano la Stars wanatarajia kuwasili nchini leo.
Mwakalebela aliwataja waamuzi hao kuwa ni, Mohamed Ali, Abdallah Ali na Hassan Yassin wanaotoka Djibouti.
Comments
Loading…