Wakati tukiendelea kusubiri kuona pira Biryani, pira Sambusa na pira Baga la kocha mpya wa Yanga Cedric Kaze bado tunaendelea kuangalia matukio pamoja na wachezaji wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Bila shaka kila mmoja anapenda kuona mchezaji gani ambaye amefanya vizuri katika raundi tano zilizopita wakati huo tumeanza raundi ya sita ikiwa mechi tano zishapigwa tayari.
Pale tulipoishia kwa raundi tano tuliona magoli 74 yakifungwa kwa timu zote 18, tutakuwa wachoyo wa fadhila kama tusipochagua wachezaji bora 11 ambao wamefanya vizuri hadi sasa pamoja na kocha wao atakaye iongoza orodha hiyo.
Bila kuchelewa tuanze na goli kipa ambaye amefanya vizuri kabisa kwa raundi tano.
Metacha Mnata wa Yanga
Kwa michezo mitano ambayo Yanga imecheza Metacha na jopo lake la ulinzi ameruhusu goli moja pekee huku akikusanya ‘Clean Sheets’ nne.
Metacha sio mzuri katika matumizi mazuri ya mguuni lakini kazi anayoifanya ni kubwa mno kuokoa michomo pamoja na hatari nyingine.
Unaweza ukahoji kwanini asingekuwa David Kisu wa Azam FC ? au Aishi Manula, huyu Kisu amecheza michezo sita tayari lakini katika rekodi ya michezo mitano ambayo ndio hasa tunaiongelea hapa ameruhusu magoli mawili katika nyavu zake.
Wakati huo naye ana ‘Clean Sheets’ nne lakini nimemtoa katika nafasi ya kwanza kwakuwa amefungwa magoli mengi zaidi kuliko Mnata.
Manula yeye ana ‘Clean Sheets’ tatu amekubali kuruhusu magoli 2 katika mechi mbili tofauti ile ya Ihefu FC ambayo Simba ilishinda 2-1 na ile ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar hivyo bado Mnata atabakia kuwa namba moja katika kikosi changu.
Shomary Kapombe wa Simba
Inawezekana ningekuwa mchoyo kabisa kutomtaja Kapombe ni beki bora kabisa kuwahi kutokea hapa Tanzania.
Msimu huu hakuweza kufunga bado kwa mechi tano lakini madhara yake kwa wapinzani haina haja ya kuwakumbusha kwakuwa inaonekana uwanjani.
Alistaafu kuichezea timu ya taifa lakini baadae mambo yakawekwa sawa na akarudi kikosini. Sio kwa upendeleo bali uwezo binafsi wa nyota huyo.
Aliwahi kufunga magoli 7 akiwa Azam FC ni hatari sana kwa nafasi yake kuweza kushindana na washambuliaji.
Nafasi yake ya usaidizi nampatia bwana mdogo Israel Patrick, huyu nyota wa Kinondoni Municipal Council (KMC) alizua gunzo baada ya Ndayiragije kumuita katika kikosi cha Stars lakini kocha huyo aliwaambia waliokuwa wanahoji kuwa aliweza kutoa nafasi za magoli nne kwa mechi nne alizocheza hivyo alistahili kuitwa na mimi namuingiza kikosini.
Aina ya kupanda na kushuka huku akicheza vizuri na kulinda jukumu lake.
Ni mchezaji mzuri ambaye anaweza kuisaidia taifa siku za mbele akicheza katika kiwango hiki hiki.
Bruce Kangwa wa Azam FC
Nyota wa kushoto wa Azam FC licha ya umri wake unaonekana wa jioni lakini ana uwezo mkubwa sana huyu jamaa hajawahi kuniangusha tangu atue Tanzania naye anawekwa katika kikosi hiki kwa raundi tano.
Bakari Nondo Yanga
Mwamnyeto ni nyota wa Yanga na inasadikika kuwa ndiye aliye nunuliwa kwa pesa ndefu sana.
Ukuta wake umeruhusu goli moja tu pamoja na yote bado wanacheza vizuri na pacha wake Moro.
Lamine Moro
Nahodha mpya wa Yanga Lamine Moro amefunga magoli 2 ameisaidia Yanga kupata alama sita kwa kutumia kichwa chake, alifunga dhidi ya Mbeya City kwa kichwa na Mtibwa Sugar.
Anacheza pacha na Nondo uwezo wake ni mkubwa mno hakuna mashaka kuwa msimu huu ameanza na moto sana.
Hapa najua nitaramba matusi wakihoji vipi kuhusu Onyango ama Abddallah Heri wa Azam.
Hao wote wamefanya vizuri lakini wameruhusu magoli 2 kila mmoja lakini pia katika vigezo vingine wanafanana ikiwa pamoja na ‘Saves’ za hatari.
Jonas Mkude
Umuhimu wake unajulikana tu pale anapookoa mpira ila watu hawamuangalii kwa jicho lingine, huyu jamaa ananifurahisha sana kwani yeye hana uchu wa kufunga anatimiza majukumu yake ya ulinzi ila ikitokea anafunga.
Feisal Salum ‘Fei Toto’
Kiungo hodari kabisa wa Yanga yeye atacheza kiungo namba nane anaufanya mpira uonekane kuwa bora machoni mwa watu.
Uwezo wake kila mmoja anauona uwanjani anaweza sana kufanya vizuri kwa michezo mitano.
Clatous Chama
Kiungo bora kabisa kuwahi kutokea hapa Tanzania amefunga magoli mawili hadi sasa na ametoa nafasi mbili za magoli.
Huyu haina haja ya kumuelezea kila mmoja atakuwa anakubali kuwepo katika kikosi hiki.
Atacheza katika shimo kwa maana ya namba kumi ili atupe udwambwi na tuziangalie zile pasi za visigino.
Prince Dube wa Azam FC
Mechi sita amefunga magoli sita, na kwa mechi tano ambazo tunazichambua leo amefunga magoli matano.
Amefunga magoli 8 katika mechi saba moja ya kirafiki zilizobaki za mashindano.
Ana kipaji cha hali ya juu sana hadi zimetoka tetesi kuwa Raja Casablanca wanahitaji huduma yake kwa mkwanja mrefu sana.
Kwa hakika hapa Azam wameramba dume sana kumpata mchezaji kama huyu anaonekana anauwezo mkubwa na hata akikata umri hajakata sana huenda kakata miaka miwili au mitatu.
Atakaa namba tisa ili atupie magoli mengi katika kikosi hiki cha maajabu.
Meddie Kagere Simba
Licha ya kutopata nafasi ya mara kwa mara kutokana na ubora wa kikosi cha Simba msimu huu bado amefunga magoli 4.
Hakuna namna ya kumsimamisha mshambuliaji huyu anaweza kufunga kwa namna yoyote ile.
Luís Miquissone
Huyu mtu hatari sana huenda Simba wakamuuza kwa bei ghali sana kwa kiwango chake.
Kila mmoja anaweza kukubali uwezo wake baada ya makubwa ambao ameyafanya hadi sasa akiwa na Simba.
Msimu uliopita alikuwa miongoni mwa washindani wa kinyang’anyiro cha goli bora.
Msumu huu hadi sasa ameshafunga goli moja pamoja na kutoa nafasi moja ya goli.
Kocha mkuu wa kikosi hiki ni Aristica Ciaoba wa Azam FC msimu huu amekuja kivingine kabisa.
Haya ni maoni yangu hata wewe unaweza kuunda kikosi chako na ukakitolea ufafanuzi zaidi.