Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania, TBF, limemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete nao kuwaletea kocha wa kigeni kwa ajili ya kuinoa timu ya taifa ya mchezo huo.
Kauli ya TBF imekuja baada ya Kikwete katika hotuba yake kwa Wabunge wiki iliyopita kuwaahidi wadau wa riadha kuletewa kocha wakigeni kama alivyofanya kwa timu ya taifa ya soka.
Rais wa TBF Richard Kasesera alisema katika suala hilo nao wanaomuomba rais awaletee makocha hata wa kujitolea ili waweze kuwasaidia kutengeneza timu itakayokuwa ikishiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.
“Tunamuomba rais atusaidie na TBF, sababu suala la kocha ni tatizo sugu katika chama hicho,“ alisema Kasesera.
Aliongeza kusema kwa upande wa mchezo wa kikapu, wanashindwa hata kushiriki katika michuano ya Olimpiki, kutokana na kukosa kocha ambaye atainoa timu ya taifa, itakayoshiriki michuano ya kikapu.
Wakati huo huo, Kasesera aliupongeza mkoa wa Dar es Salaam kuandaa mashindano ya kikapu ya shule za Sekondari yanaoendelea katika uwanja wa ndani wa taifa.
Akizungumza jana, alisema michuano hiyo inasaidia kupata wachezaji chipukizi watakaojiunga katika timu ya taifa ya baadae.
- SOURCE: Nipashe