MOJA ya habari endelevu na kubwa kwa muda sasa ni ya mashindano ya Olimpiki yanayofanyika majira ya joto jijini London kuanzia Julai 27 hadi Agosti 12, 2012.
Ni mashindano makubwa yanayoshirikisha wastani wan chi 204, ambapo 165 tayari zimefuzu, huku wanamichezo wanaotarajiwa kujumuishwa wakiwa ni 10,500, na cheche zake hazitakuwa pengine zaidi ya pale Olympic Stadium, mashariki mwa jiji la London.
Afrika ambayo daima imekuwa mbele kimichezo, nyota yake iking’aa katika kona mbalimbali za dunia, inashiriki kikamilifu michezo ya mwaka huu.
Safari hii Afrika imekuja na mfumo mpya, ujirani mwema na mkakati wa pamoja kwa kuwa na Kijiji cha Afrika, kitakachokuwa eneo la makutano kwa bara lote, kusini hadi kaskazini sawa na mashariki hadi magharibi.
Wote watakutana hapo kupeana salamu, kutiana moyo na kubadilishana mawazo na maarifa ya jinsi ya kufanya vyema michezoni na kwa ujumla kulinda hadhi na sifa ya bara tukufu la Afrika.
Mipango hii imebuniwa na Chama cha Kamati za Taifa za Olimpiki za Afrika (ANOCA), mwavuli rasmi wa kamati za nchi wanachama, ulioanzishwa Lome, Togo, Juni 28, 1981.
Kwa hiyo, wakati London ikirindima kwa yote yatakayooneshwa na wanamichezo washiriki kwenye Olimpiki, Afrika inataka kuwa tofauti, kwa kuweka mbele maslahi ya eneo hilo kwa pamoja na kuhakikisha vipaji vya wanamichezo wake vinaonekana na kudhihirika.
Rais wa ANOCA, Jenerali Lassana Palenfo ambaye ni raia wa Ivory Coast, anaona ushindani mkubwa utakuwapo, kwa sababu Kamati za Olimpiki za dunia nzima zitakuwa zinajitutumua kutaka kuonyesha makali ya washiriki wake.
Kama ilivyo ada, tamu ya ushindi kwenye mashindano yoyote ni tuzo, na kwa Olimpiki kuna medali kedekede, ambapo uwaniaji wa kwanza ni zile za dhahabu, pili fedha na tatu shaba.
Afrika itaambulia ngapi? Jenerali Palenfo anasema kinachotakiwa ni kujituma, uzalendo na ari katika mazoezi, kwa sababu kama ni vipaji, tayari Afrika imeshadhihiri kuwa navyo vingi.
Hata hivyo, kando ya michezo – pengine kabla au baada ya kila tukio, kujumuika pamoja kunaijenga sana jamii ya wana Olimpiki na ni moja ya nguzo imara za kuleta ushindi kwenye hatua inayofuata.
Kijiji hicho cha Afrika ndani ya Jiji la London kipo katika eneo maarufu la Hyde Park na kitakuwa na maeneo mawili yenye majukumu yanayopandana.
La kwanza ni Klabu ya Afrika inayokuwa eneo la mapokezi rasmi lakini binafsi, mahsusi kwa ajili ya viongozi wa chama na Kamati za Olimpiki za Afrika kuwakaribisha viongozi wa michezo, wanamichezo wanaoshiriki pamoja na wadhamini wao.
Kwa maana nyingine, hili ni eneo maalumu ambalo hata zile kamati za ufundi zitapata nafasi, baraka, muda wa kuweka mambo yao sawa kwa ajili ya kuwezesha ushindi kwa wanamichezo wa Afrika.
Klabu hii ya Kijiji cha Afrika ndani ya London haitakuwa pweke wala wanaokaa humo hawapatwa ukiwa, kwa sababu kwa utajiri wa rasilimali Afrika iliopewa na Maulana, patakuwapo na studio za redio, lakini kubwa zaidi na studio za televisheni kadhalika.
Eneo la pili kijijini hapo ni Ardhi ya Afrika. Waafrika na ardhi huna cha kuwaambia, na sasa wameimega London na kutwaa ardhi yao kwa ajili ya kujitambulisha vyema mbele ya mabara na mataifa mengine.
Katika ardhi hii patakuwapo mabanda na mabango mbalimbali, yakiwakilisha utamaduni na usanii mtawanyiko unaopatikana katika Bara la Afrika.
Hawa wataonyesha mila, desturi na kwa ujumla wake utamaduni kutoka maeneo kama Afrika Mashariki, Kati, Kusini, Kaskazini bila kusahau Afrika Magharibi.
Fursa hii inatumiwa kama dirisha la Afrika kwa dunia, ambapo mabanda yatakuwa na ukubwa wa mita 16 za mraba kila moja na kuonyesha utajiri wa bara katika utamaduni.
Ardhi hii itakuwa maalumu kwa ajili ya maonyesho ya mambo ya Kiafrka na katika kukata mzizi wa fitna kwa wapendao kuonja au hata kula na kushiba, basi patakuwa na mgahawa unaotoa huduma ya vyakula vya Kiafrika.
Havitakuwa tu ni vyakula vya Kiafrika, bali ukamilisho wake ni kwamba vitapikwa Kiafrika na moshi ukilihanikiza anga la London, bila shaka ukisambaza kwa majirani harufu nzuri ya chakula kinachopikwa na kualika wengi kutoka pande tofauti. Eneo hili litakuwa wazi kwa mtu yeyote kutoka bara lolote.
Kana kwamba hiyo haitoshi, ni katika hii Ardhi ya Afrika patakuwa pia na maonyesho ya watu maalumu, walau tuseme picha za wanamichezo mahiri wa zamani wa Afrika waliowika kwenye mashindano yaliyopita ya Olimpiki na kuacha alama zisizofutika kwenye medani ya michezo.
Hizi zitakuwa picha kubwa zitakazolipamba eneo la ardhi hii, hivyo kualika watu wa asili tofauti kuivumbua Afrika na utajiri wake.
Yote tisa, kumi ni kwamba kila jioni, Kijiji cha Afrika kitarindima kwa muziki mzito wa Kiafrika kupasua anga, muziki utakaoporomoshwa moja kwa moja (live) na kundi la wanamuziki maarufu wa Afrika.
Haya ni maeneo mawili, majukwaa tofauti lakini ndani ya kijiji kimoja na yenye nia moja ya kuitangaza Afrika na yatakuwa wazi kwa watu wote muda wote wa Michezo ya Olimpiki.
Afrika inataka kutumia Kijiji cha Afrika ndani ya London kuifanya michezo hii ya aina yake kuwa sehemu ya mawasiliano muhimu yatakayodumisha udugu na urafiki, lakini zaidi kuwafunda zaidi wanamichezo kwa kuwafumbulia kwamba michezo ni zaidi ya mikwaruzano kwenye dimba.
Afrika inatarajia kushinda medali nyingi zaidi ya zile ilizopata Beijing, China mwaka 2008 na sasa inataka iunganishe nguvu kudhihirisha nguvu ya umoja, kisha kwenda kufurahia pamoja kijijini Afrika.
Kijiji hicho pia kitakachojumuisha viongozi wa michezo mbalimbali, kitatoa mwanya kwao kubadilishana uzoefu na maarifa na kupeana mbinu za kuepuka mizozo michezoni kwa waliogubikwa nayo.
Penye nchi nyingi kama hizi 53 za Afrika zinazoshiriki, patakuwa na hazina ya viongozi, wadhamini na wafadhili wenye mengi ya kuinua michezo katika Afrika na kuweka msingi imara, ili ushindi uwe daima wimbo wa Afrika.
[email protected]
Comments
Loading…