|
||||
KATIBU mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amesema kuwa hataomba radhi kwa klabu na wanachama wa Yanga hadi hapo viongozi wa klabu hiyo watakapoomba radhi kwa kusema uongo.
“Huo ndio msimamo wangu na nitasimama imara,” alisema katibu huyo alipoongea na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu dai la viongozi wa matawi ya Yanga kutaka rais wa TFF, Leodegar Tenga kuomba radhi kwa niaba yake.
Musonye, akionekana kukerwa na kitendo cha Yanga kutoingiza timu kupambana na Simba katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu ya Kombe la Kagame, aliwatukana viongozi wa Yanga akisema kuwa ni “wapuuzi, wajinga na wapumbavu”.
“Na sikukosea. Napenda kusisitiza kuwa viongozi wa Yanga ni wapuuzi, wajinga na wapumbavu,” alisema Musonye Jumapili katika mkutano na waandishi uliofanyika mara baada ya Yanga kushindwa kuibuka uwanjani Jumapili.
Na jana, Musonye hakuonekana kulegeza msimamo wake.
“Viongozi wa Yanga walidanganya kuwa walikuwa na makubaliano na sisi na Simba kuwa klabu zipewe fedha. Hakukuwa na makubaliano hayo. Huo ndio ujinga naosema,” alisema.
“Siwezi kuomba radhi kwa kusema hivyo na sitetereki. “Sitaomba radhi hadi wao waombe radhi kwanza kwa kusema uongozi kuwa tulikubaliana nao wapewe fedha.”
Kuhusu Kombe la Kagame kutokuwa na kanuni inayoadhibu timu kutofika uwanjani, Musonye alisema: “Huo ndio ujinga naousema. Hakuna chama kinachoweza kuweka kanuni kuwa timu inaweza kutofika uwanjani, hata CAF hakuna hilo.
Cecafa, ambayo iliwahi kusigana na Yanga kutokana na baraza hilo kutoilipa Dola 10,000 ilizostahili kupata kwa kuwa mshindi wa tatu kwenye mashindano hayo mwaka 1995, imeifungia Yanga kushiriki mashindano yake matatu kwa kosa hilo.
Comments
Loading…