Wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wanatakiwa kufanyia marekebisho katika katiba zao kwa kuingiza ibara ya Kamati za Maadili.
Maagizo hayo yanatokana na kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF iliyoketi Novemba 23 mwaka huu jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jamal Malinzi ambapo pamoja na mambo mengine ilijadili umuhimu wa wanachama wake kuunda kamati hizo.
Wanachama wa TFF ambao muda wao wa uchaguzi umekaribia, wanatakiwa kufanya marekebisho hayo kwanza kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi.
TFF ina aina tatu za wanachama. Wanachama hao ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na Klabu za ligi Kuu.
FAINALI YA KOMBE LA UHAI CHAMAZI
Mechi ya Fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu itachezwa keshokutwa (Jumapili) kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Coastal Union ndiyo itakayocheza fainali hiyo kuanzia saa 9.30 alasiri dhidi ya mshindi wa mechi ya nusu fainali ya pili kati ya Yanga na Mtibwa Sugar inayotarajia kuchezwa baadaye leo.
Mechi ya fainali itatanguliwa na ile ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Azam na timu itakayoshindwa katika mechi ya pili ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu iliyoanza katika viwanja vya Karume na DUCE kabla ya kuhamia Chamazi.
Comments
Loading…