Mchakato wa uchaguzi wa kamati mpya ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) unatarajiwa kutangazwa kesho (Agosti 13 mwaka huu).
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni atakutana na
Waaandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF saa 6 kamili mchana ambapo mbali
ya mchakato utakavyokuwa anatarajia kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi huo
ambao awali ulitarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilikutana Jumapili (Agosti 11 mwaka huu) na
inatarajia kuwa na kikao kingine leo (Agosti 12 mwaka huu) ambapo pamoja na
mambo mengine itazungumzia maandalizi ya uchaguzi huo.
Mbali ya Mbwezeleni, wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Moses Karuwa (Makamu
Mwenyekiti), Mohamed Sinani, Chabanga Dyamwale na Kitwana Manara.
* *
*MAGORI, LINA WAINGIA KAMATI ZA CAF*
Watanzania Crescentius Magori na Lina Kessy wameteuliwa kuwa wajumbe kwenye
kamati ndogondogo (standing committees) mpya za Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) zilizotangazwa juzi na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo
Hicham El Amrani.
Magori na Lina ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF watakuwa
kwenye kamati hizo kwa kipindi cha miaka miwili (2013-2015). Magori
ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Mpira wa
Miguu wa Ufukweni (Beach Soccer) wakati Lina ameingia kwenye Kamati ya
Maandalizi ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake.
TFF tunawapongeza kwa uteuzi huo ambao umetokana na uwezo ambapo ni imani
yetu kuwa wataiwakilisha vizuri Tanzania na uzoefu watakaopata kupitia
kamati hizo utakuwa msaada mkubwa kwa ustawi wa mchezo wa mpira wa miguu
nchini.
Naye Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani ameteuliwa tena kuwemo kwenye
Bodi ya Rufani ya CAF yenye wajumbe 12 kwa kipindi kingine cha miaka
miwili. Nyamlani alikuwepo kwenye bodi iliyopita, na itaendelea kuwa chini
ya uenyekiti wa Prosper Abega kutoka Cameroon.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
CAF yuko kwenye kamati tano za Shirikisho hilo. Kamati hizo ni Kamati ya
Fedha ambayo ni Makamu Mwenyekiti na Kamati ya Maandalizi ya Fainali za
Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Kamati nyingine ni Kamati ya Masoko na Televisheni ambayo ni Mwenyekiti,
Kamati ya Ufundi na Maendeleo, na Kamati ya Ushauri na Vyama Wanachama wa
CAF.
* *
*KAMATI YA SHERIA KUPITIA USAJILI*
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex
Mgongolwa inakutana leo jioni (Agosti 13 mwaka huu) na kesho (Agosti 14
mwaka huu) kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa wachezaji wenye matatizo.
Hatua ya kwanza ya usajili imeshamalizika wakati hatua ya pili ya usajili
inaanza kesho (Agosti 14 mwaka huu) ikihusisha wachezaji ambao watakuwa
hawajasajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na wale kutoka nje ya
Tanzania.
Hivyo, dirisha la uhamisho kwa wachezaji wa kimataifa litafungwa baada ya
hatua ya pili ya usajili kumalizika Agosti 29 mwaka huu.
Comments
Loading…