Kuna kumbukumbu nyingi sana ambazo kocha wa zamani wa Yanga , George Lwandamina alizowahi kutuachia. Kila mtu anaweza kumkumbuka kwa vitu vingi vizuri na vibaya.
Kuna wengine watamkumbuka namna alivyofanikiwa kuingia kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya vilabu barani Afrika. Alama ambayo haiwezi kufutika kwa urahisi kwa sababu ni alama ya mafanikio.
Kuna wengine watamkumbuka kwa kuleta kiungo mkata umeme kwenye kikosi cha Yanga, kiungo ambaye alituaminisha kuwa angekuja kumaliza matatizo yote ya Yanga katika safu ya kiungo cha kuzuia.
Binafsi mimi namkumbuka George Lwandamina na kikosi chake cha mwisho mwisho kabla hajaondoka kwenda Zambia baada ya kushindwa kuendelea na kikosi cha Yanga.
Kwenye kipindi cha George Lwandamina kuliwahi kuwepo wachezaji nyota ambao waliwahi kuibeba Yanga na kuifikisha kwenye mlima mafanikio, ndicho kipindi ambacho Yanga iliwahi kuwa na Donald Ngoma wa moto na Obrey Chirwa wa kutisha.
Lakini kwa bahati mbaya kwenye msimu wa mwisho wa George Lwandamina, Yanga ilianza kuishi maisha magumu ya kuunga unga kuanzia kwenye mishahara mpaka ndani ya uwanja, ndicho kipindi ambacho Yusuph Manji ameondoka.
Na ndicho kipindi ambacho wachezaji wengi nyota wa Yanga walikuwa na majeraha sana kitu ambacho kilisababisha wasipate muda wa kucheza kwa asilimia kubwa ukilinganisha na mwanzoni.
George Lwandamina hakuwa na kila mchezaji nyota aliyekuwa anamtegemea kwenye kikosi chake na hapo alikuwa anashiriki mashindano ya kimataifa ya kombe la shirikisho barani Afrika.
Akili ya George Lwandamina ilimtuma kuwaamini vijana wadogo ambao walikuwa hawajawahi kupewa nafasi kwenye kikosi cha Yanga na yeye akaamua kuwapa nafasi kubwa kwenye kikosi chake.
Ndipo hapo alipoamua kuwapandisha wachezaji wa timu ya vijana ya Yanga ya wachezaji walio chini ya umri wa miaka 20 na kuwapandisha mpaka kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
Lilikuwa jambo gumu sana ambalo wengi walilishangaa lakini George Lwandamina aliliamini sana kwa kiasi kikubwa kwa kujipa imani kuwa jambo hili litafanikiwa na linaweza kuwa na matunda mengi kwenye taifa .
George Lwandamina aliwalisha sumu wachezaji hawa wenye umri mdogo, sumu ya mafanikio. Aliwaonesha njia ya kupita na kuwahimiza kuwa huo wakati ndiyo ulikuwa wakati sahihi kwao wao kuyapigania mafanikio.
Aliwahimiza umuhimu wa wao kutumia nafasi ambayo wamepewa na hapo ndiyo ukawa mwanzo mzuri kwa baadhi ya vijana kuonesha vipaji vyao vikubwa ndani ya klabu kubwa Tanzania.
Moja ya vijana ambao walionesha umahiri wao ni Yusuph Mhilu, mchezaji ambaye alikuwa na sifa nyingi sana za mchezaji wa kisasa , yani mchezaji wa kileo ambaye anaendana na mahitaji ya mpira wa kisasa.
Yusuph Mhilu alikuwa anatokea pembeni mwa uwanja na kuingia ndani karibu na eneo la wapinzani . Alikuwa anafunga kwa kutokea pembeni kitu ambacho timu nyingi duniani kwa sasa kinahitaji wachezaji wa aina hiyo.
Kabla ya Yusuph Mhilu, Yanga iliwahi kuwa na Mrisho Khalfan Ngassa na Simon Msuva. Hawa ni wachezaji ambao walikuwa na uwezo wa kufunga magoli mengi wakitokea pembeni mwa uwanja.
Wengi tulijua huyu ndiye atakuja kuwepo kwenye mwendelezo wa Yanga kuwa na wachezaji wa aina ya kina Mrisho Ngassa na Simon Msuva lakini Yanga waliamua kumuuza Yusuph Mhilu katika timu ya Kagera Sugar.
Timu ambayo imemsaidia sana kupata muda mwingi wa kucheza . Muda ambao amefanikiwa kuutumia vizuri mpaka sasa hivi ana magoli 11 nyuma ya Meddle Kagere mwenye magoli 19 ambaye ndiye anayeongoza orodha ya ufungaji bora kwenye ligi kuu Tanzania bara.
Ameshakomaa tayari, siyo mtoto tena ni mtu mzima ambaye ana nafasi kubwa ya kulinda himaya kubwa kama akiaminiwa kwa kiasi kikubwa. Miguu yake inastahili kuitetea tena Yanga kwa mara ya pili kwa sababu imeshakomaa.
Achana na ukomavu wa miguu yake, Yusuph Mhilu ni kijana ambaye kalelewa pale Yanga anaujua utamaduni wa Yanga , anajua mahitaji ya Yanga kwa hiyo ni rahisi kwake yeye kuitimizia Yanga mahitaji ambayo Yanga wanayahitaji.
Yusuph Mhilu kwa sasa ana umri ambao unampa nafasi kwake yeye kuitumikia Yanga kwa kipindi kirefu kwa manufaa makubwa . Wakati napata taarifa za urejeo wa Makambo nafsi yangu ikatamani niwashauri Yanga wamrejeshe na Yusuph Mhilu.