*Man City/United nazo vitani kumnasa RVP
*Wenger bado asisitiza nia ya kumbakisha
Miamba wa soka wa Italia, Juventus wmekuja na mtego mpya, wakiwataka Robin van Persie na Luis Suarez kwa pamoja.
Juventus iliyokwishawasilisha dau la RVP kwa The Gunners, sasa inatumia mbinu za medani kuulainisha moyo wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kutoka Uholanzi.
Waitaliano hao wanajua kwamba RVP katika kufanya uamuzi wake hatatilia maanani pesa peke yake, hivyo wamemnong’oneza kwamba hatakuwa peke yake, bali atafanya kazi na Suarez anayechezea Liverpool.
Msimu wa kiangazi umeanza kwa mvutano wa usajili Kocha Mkuu wa Washika Bunduki wa London, Arsene Wenger akisisitiza anataka kubaki na RVP – mshambuliaji wake bora wa msimu uliopita.
Hata hivyo Arsenal kusema RVP hauzwi hakujazizuia klabu nyingine kumkodolea macho na hata kupeleka dau, kwani matajiri wa Manchester – Manchester City na Manchester United nao wanamtaka RVP.
Juventus, au Kibibi Kizee cha Turin, inasemekana imetoa ahadi nono kwa Van Persie, ikiwa ni pamoja na kuongeza zaidi ya maradufu mshahara wake na kumpa marupurupu mengine.
Van Persie anayechungulia umri wa miaka 29, amefunga mabao 41 katika michezo 53 ya klabu nan chi yake msimu uliopita na ndiye mchezaji wa mwaka wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa (PFA) na wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo.
Mkurugenzi wa Michezo wa Juventus, Giuseppe Marotta na Rais Andrea Agnelli wanatumia kila mbinu dakika hizi za ushindani mkubwa ili kumpeleka Van Persie Italia.
Zipo habari zisizothibitishwa kwamba anaandaliwa kitita cha Pauni 190,000 kwa wiki na iwapo atatoa jibu chanya kwao, ndipo watamgeukia Suarez.
Ili kutimiza ndoto yao, Juventus inafikiria kumuuza mchezaji wake Alessandro Matri kwa AC Milan, japokuwa Liverpool kwenyewe kuna kigingi kikubwa cha kumpata Suarez.
Inatambulika kwamba Liverpool inamtegemea Suarez katika safu yake ya ushambuliaji, na licha ya kuwa na mkataba na klabu hiyo ya bosi Brendan Rodgers hadi mwaka 2016, badi inalenga kumwongezea mkataba.
Suarez, raia wa Uruguay mwenye umri wa miaka 25 amefunga mabao 15 tangu alipojiunga Liverpool Januari mwaka 2011.
Hata hivyo, amecheza katika msimu ambao Liverpool haikuwa katika kiwango wala kushinda mechi ilivyotarajiwa.
Pia ni wakati huu alikosa mechi nane mfululizo alizofungiwa baada ya kutiwa hatiani kwa madai ya kumtukana kwa kumbagua rangi Patrice Evra wa Manchester United Desemba mwaka jana.
Rodgers ameshafanya mazungumzo ya awali na Suarez kuweka msingi wa kumwongezea mkataba mpya utakaomfunga pingu Liverpool
Hata hivyo, kwa jinsi Juventus ilivyodhamiria kuwapata RVP na Suarez, ipo tayari kuipa Liverpool kitita cha Pauni milioni 28.
Inadhaniwa ukubwa wa kitita hicho utaishawishi Liverpool kuufugua moyo wake na kuanza mazungumzo, kwani fungu hilo litawatosha kununua wachezaji wengine wazuri.
Dau kwa Liverpool linakuja muda mfupi baada ya Suarez kufyatuka, akisema adhabu dhidi yake kukosa mechi nane ilikuwa uonevu, kwa sababu Manchester United inatawala siasa za soka Uingereza na walidhamiria aadhibiwe.
Chini kwa chini, kuna mawazo kwamba uwezekano wa Juventus kupata wachezaji hao wawili ni mkubwa, licha ya nguvu za United na City. Arsenal inaweza pia kumbadilisha mawazo Van Persie abaki Holloway, London.
Awali ilielezwa kwamba mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya England (EPL) anataka suala lake limalizwe mapema na kwamba akihama hangependa kubaki Uingereza, lakini kwa ushawishi lolote linawezekana.
Arsenal walikataa dau la awali la Juventus kama ilivyokuwa kwa ombi rasmi la awali la United Ijumaa iliyopita.
Kocha Mkuu wa United, Alex Ferguson anasema klabu yake haitajiingiza kwenye sakata la ‘mnada’ la RVP, bali katika mazungumzo ya kumsajili mchezaji huyo.
Hiyo ni hatari kwao, kwani jirani zao wamwaga fedha – City, wameshaweka mezani dau la kwenye Pauni milioni 10. Hizo ni Pauni milioni 15 pungufu ya Arsenal wanavyomthaminisha Van Persie. Inadhaniwa kwamba, iwe ni kwa mazungumzo au ‘mnada’, Van Persie anaweza kuuzwa kwa karibu Pauni milioni 20.
Wenger akizungumza hadharani anasema hataki mshambuliaji huyo aondoke, kwamba lazima abaki, lakini amemzuia kwenda ziara ya kujiandaa kwa ligi Asia Kusini na China.
Kuhusu umuhimu wake katika Arsenal, Wenger alikuwa na haya ya kusema:
“Kwangu mie, Van Persie ni mmoja wa washambuliaji bora zaidi duniani, kama yeye si bora kuliko wote, nataka kumbakisha klabuni hapa.
“Kuhusu (wachezaji) wengine, nitafanya kile chenye manufaa makubwa zaidi kwa Klabu ya Soka ya Arsenal. Kwa sasa hapo ndipo tulipo. Hakuna mengi ya kusema zaidi ya hayo.”
RVP amebakisha mwaka kwenye mkataba wake, na ikiwa anashinikiza kuondoka, ni wazi kwamba Arsenal isipomuuza sasa, ataondoka kama mchezaji huru wakati kama huu mwakani. Arsenal inatarajia kujadiliana na mchezaji huyo mapema iwezekanavyo kujua hatima yake.
Comments
Loading…