LIGI Kuu ya England (EPL) imeingia mzunguko mwingine baada ya
mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa, ambapo viwanja vitatu
vilishuhudia timu zikitoa kichapo cha mabao 4-0 kila moja.
Chelsea, Arsenal na Manchester City ndio waliokuwa na kicheko, huku
maumivu yakienda kwa Aston Villa, Watford na Bournemouth.
Tottenham Hotspur nao walishinda kuendelea kuwatia shinikizo vinara wa
ligi, Leicester, baada ya kupunguzwa nguvu kwa mchezo wake kumalizika
kwa sare dhidi ya Liverpool.
Chelsea, katika mchezo wa mapema muda wa chakula cha mchana Jumamosi
hii walianza furaha kutokana na bao la mchezaji Alexandre Pato
aliyekuwa akicheza kwa mara ya kwanza tangu kusajiliwa.
Bao jingine lilifungwa na Ruben Loftus-Cheek huku Pedro akifunga mabao
mawili. Ushindi huo umezidi kuwakandamiza Villa chini katika msimamo
wa ligi, huku washabiki wake wakionesha hasira kwa mmiliki.
Arsenal walifufua matumaini ya kupata ubingwa ikiwa wawili walio mbele
yao watateleza; baada ya kufunga idadi hiyo hiyo ya mabao dhidi ya
Watford.
Walianzisha maumivu kwa Watford waliowatoa kwenye robo fainali ya
Kombe la FA katika dakika ya nne tu kupitia kwa Alexis Sanchez na
mengine kupitia kwa makinda Alex Iwobi, Hector Bellerin kabla ya Theo
Walcott kukamilisha karamu ya mabao akitokea benchi.
Manchester City walimpa faraja kocha wao anayejiandaa kuondoka, Manuel
Pellegrini kwa kuwakandika Bournemouth mabao hay ohayo manne kwa bila.
Kevin de Bruyne aliyerejea baada ya kuwa nje kwa maumivu kwa miezi
miwili alikuwa nyota, aking’aa vilivyo.
Fernando alifungua kitabu cha mabao cha matajiri hao wanaomsubiri
kocha Pep Guardiola kiangazi hiki.
Mabao matatu ya City yalifungwa katika dakika 18 za mwanzo, wakionesha
kuwa na uchu kama fisi mwenye njaa. Wafungaji wengine walikuwa De
Bruyne, Sergio Aguero na Aleksandar Kolarov.
Katika matokeo mengine, Norwich waliwafunga Newcastle 3-2, wakizidi
kuwaacha kwenye eneo la kushuka daraja.
Hata hivyo, kocha mpya wa Newcastle, Rafa Benitez alisema kwamba bado
wanao muda na anaamini kwamba atawaepusha na zahama ya kushuka daraja.
Stoke walitoshana nguvu na Swansea kwa kufungana mabao 2-2, zikiwa ni
kati ya timu zisizokuwa na shinikizo la kutwaa ubingwa wala kushuka
daraja.
Sunderland wanaotakiwa kuondoka eneo la kushuka daraja walishindwa
kutumia vyema nafasi ya kucheza nyumbani kwa kwenda suluhu na West
Bromwich Albion.
West Ham wanaopigania kuingia kwenye nne bora ili kushiriki Ligi ya
Mabingwa Ulaya walibanwa na Crystal Palace kwa sare ya 2-2.
Leicester wanocheza Jumapili hii wamebaki kwenye usukani kwa pointi
zao 66, Spurs wakifuatia na pointi 62, Arsenal 58 na Man City 54.
Mkiani kwa muda mrefu wameendelea kuwapo Villa na pointi zile zile 16,
Newcastle 25, Sunderland 27, Norwich 31 na Palace 34.