Manchester United wameendelea kuonesha matumaini ya kuwafukuza majirani zao Manchester City kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England baada ya kuwatandika Watford 4-2 kwenye mchezo wa Jumanne uliopigwa ndani ya dimba la Vicarage Road. Ni alama tano pekee zinazowatenganisha na vinara Manchester City ambao wanao mchezo mkononi utakaopigwa leo Jumatano dhidi ya Southampton ndani ya Etihad.
Mchezo wa ugenini dhidi ya Watford ulikuwa kati ya vipimo viwili vigumu walivyo navyo United ndani ya kipindi cha siku hizi nne wakiwa wana mchezo mwingine Jumamosi dhidi ya Arsenal ndani ya Emirates. Uwezo walioonesha kwenye mchezo dhidi ya Watford na mingine ya karibuni ya Ligi Kuu ya England inaonesha kuwa wanao uwezo wa kupambana na Manchester City na wababe wengine kuwania taji la EPL.
Lakini kuonesha mchezo mzuri na kupata matokeo kwenye michezo dhidi ya timu za katikati na zile za mkiani pekee hakuwezi kutosha kumpa ubingwa Jose Mourinho aliye kwenye msimu wake wa pili tangu alipojiunga na klabu hiyo ya Old Trafford jijini Manchester. Kujihami zaidi anapocheza dhidi ya timu za juu na kushindwa kuzitawala timu za namna hiyo kunaweza kuwa sababu itakayoweza kuwakosesha ubingwa Manchester United msimu huu.
Wakiwa wamecheza michezo 14 mbaka sasa, mabingwa hawa mara 13 wa Ligi Kuu ya England tayari wamecheza na Liverpool, Spurs na Chelsea kati ya zile zilizo kwenye nafasi sita za juu. Wameshinda 1-0 dhidi ya Spurs, wametoa sare ya bila kufungana kwenye mchezo wao dhidi ya Liverpool na kupoteza mchezo wa Chelsea kwa 1-0.
Mbinu za kujihami zaidi za mwalimu Jose Mourinho anapocheza na timu za juu zimekuwa sababu kuu ya kushindwa kukusanya alama za kutosha anapokutana na timu hizo. Oktoba 14 United walipiga shuti moja pekee lililolenga lango dhidi ya Liverpool kwenye dakika zote tisini huku wapinzani wao wakiwa na mara tano ya idadi hiyo ya mashuti yaliyolenga lango. Jose Mourinho alichagua kujihami zaidi na kwa bahati aliambulia sare.
United walibadilika na kushambulia zaidi Oktoba 28 kwenye mchezo wao dhidi ya Spurs ambapo waliibuka na ushindi mwembamba wa 1-0. Pengine kucheza nyumbani ndiko kulikompa Mourinho hali ya kujiamini na kujaribu kufunguka na kutengeneza nafasi nyingi zaidi. Hata hivyo bado Spurs ndio waliotawala zaidi mchezo. Walipiga mashuti mengi zaidi na walikuwa na asilimia nyingi zaidi za umiliki wa mpira.
Takwimu za mchezo dhidi ya Chelsea ambao United walipoteza ndani ya Stamford Bridge mapema mwezi huu zinaleta picha ileile. Ingawa walijaribu kufunguka na kutengeneza nafasi kwa kiasi fulani, lakini bado walikuwa nyuma ya Chelsea kwenye vipengele vyote muhimu vya takwimu. Chelsea waliotawala mchezo zaidi walistahili ushindi walioupata.
Aina ya mchezo wanaocheza Manchester United wanapokutana na timu za juu mara nyingi utaendelea kushindwa kuwapatia matokeo. Unapokuwa na kikosi kinachotajwa kuwa cha pili kwa thamani kubwa zaidi ndani ya Ligi Kuu ya England huna sababu kucheza mchezo unaoashiria kuwa unawaogopa mno wapinzani wako. Aina hii ya mchezo si aina inayoweza kukupatia ubingwa kutokana na uwepo wa Manchester City walio kwenye ubora wa hali ya juu.
Vinara Manchester City wamekuwa wakionesha kiwango kizuri wakitawala mchezo na kupata matokeo mazuri dhidi ya timu zote za juu walizocheza nazo mbaka sasa. Wameshinda nyumbani 5-0 dhidi ya Liverpool, ugenini 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Chelsea na 3-1 nyumbani dhidi ya Arsenal. Kupambana na timu hii kwenye mbio za ubingwa unahitaji kujaribu kutawala wapinzani wako hata kwenye michezo migumu kama wafanavyofanya wao.
Mchezo wa ugenini wa Jumamosi hii dhidi ya Arsenal ni mtihani mgumu kwa Jose Mourinho. Kutokana na pengo la alama lililopo kati yao na vinara Manchester City, Mourinho analazimika kupata matokeo mazuri dhidi ya Arsenal. Mchezo wa kujihami zaidi na kutegemea mashambulizi ya kustukiza ni vigumu kuwapa matokeo Manchester United. Wanahitaji kuwatawala Arsenal ili watengeneze nafasi za kutosha na hatimaye kuibuka na ushindi muhimu.