Kulikoni makocha wengi wasaidizi, au kwa namna wanavyoitwa, namba mbili, hushindwa kupanda hadi kuwa makocha kamili wenye mafanikio?
Hili ni swali la muda mrefu kwa sababu ya ukweli wa hali hiyo si tu hapa England bali hata katika nchi nyingine. Wanakiwa wazuri sana kwenye usaidizi lakini wakifikia kuteuliwa kushika namba moja wanakuwa magarasa na kuangusha klabu husika.
Dakika 10 tu tangu kuanza kikao chake cha kwanza na wanahabari tangu awe kocha mpya wa Arsenal, Mikel Arteta aliulizwa swali ambalo alijua lingekuwa linakuja; kulikuwapo umuhimu gani kwa watu kumwona kama kocha katika hadhi yake binafsi bila kuunganisha na usaidizi wake kwa Pep Guardiola (alikuwa msaidizi wake katika Manchester City).
“Haijalishi watu wananiona vipi. Jambo la muhimu ni vipi wachezaji wananichukulia, wanashawishikaje nami na wanavyoona kwamba tunajaribu kufanya mambo sahihi. Baada ya hapo, muda ndio utaonesha na kuondoa utegemezi huo,” yalikuwa majibu ya Arteta, kiungo wa zamani wa Arsenal.
Haikuchukua muda, aina ya mawasiliano ya haraka na mafupi pamoja na uamuzi wa mambo ili kubadili mfumo na kujenga nidhamu mpya kwa wachezaji katika klabu iliyoonekana wazi kuwa na kiu hiyo vilileta mabadiliko juu ya jinsi alivyokuwa akionekana; sin amba mbili tena – Arteta alikuwa amepata kile ambacho wengi walikikosa wakishapandishwa vyeo na kuwa makocha wakuu.
Hapana shaka kwamba bado ni mapema mno kwa sie kuchukulia kwamba Arteta amefanikiwa katika unamba moja wake Emirates lakini inaaminika kwamba atawavusha kwenye kipindi cha mpito na kuwaletea mafanikio, akikweka kundi la namba mbili walioaminiwa na kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
Naam, anatakiwa kuwavusha Arsenal ambao katika miaka ya mwisho ya Arsene Wenger waliingia pabaya wakiwa na unyonge mkubwa ambao haukuweza kumalizwa ipasavyo na Unai Emery – Mhispania mwenzake na Arteta, kwa muda mfupi aliokaa London Kaskazini.
Mazingira ya muda mrefu ndiyo yameuonesha ulimwengu wa soka kuwameza wale watu waliochukuliwa kama wazuri kwenye ukufunzi wa soka. Brian Kidd alitumia miaka saba akiwa msaidizi wa Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, akisaidia kulimbikiza makombe kwenye makabati ya klabu hiyo miaka ya ’90.
Alikuwa mzuri katika kuwajenga na kuwaendeleza wachezaji chipukizi wa enzi hizo kama Ryan Giggs na Paul Scholes. Hata hivyo, Desemba 1998 aliondoka kwenye kivuli cha Ferguson na kuingia kwenye kazi ya kwanza kubwa kama kocha. (Kwa muda mfupi alikuwa kocha pale Preston North End mapema baada ya kustaafu soka kisha akaamua kushika hatamu Blackburn Rovers).
“Inaweza ikakuchukua muda mrefu kupita kiasi n amie sitaki kufa nikiwa nahangaika,” yalikuwa maneno ya Kidd baada ya uteuzi wake wa kwanza. Na kweli hakuachwa kwa muda mrefu, kwani miezi 11 tu baadaye, Blackburn wakiwa wameshashuka daraja, na bado wakiwa wanashika nafasi ya 19 kwenye Ligi Daraja la Kwanza, alivuliwa madaraka. Na ndivyo muda wa madaraka yake kama kocha ulivyokwenda – shoka moja mbuyu chini.
Si yeye pekee katika hali hiyo, kwani alikuwapo mtu aliyeheshimiwa sana katika jina la Pep Lijnders, ambaye kwa sasa anashika namba mbili kwa Jurgen Klopp hapo Liverpool. Alijaribu lakini akashindwa kufikia namba moja.
Baada ya kutumia miaka minne njiani, akianzia kwenye akademia na kuwa mmoja wa watu muhimu kwenye jopo la wakufunzi wa Klopp, Lijnders aliondoka Januari 2018 na kuwa kocha wa klabu ya Udachi ya NEC Nijmegen. Lakini kiangazi kilipofika, hakuwa ten ana kazi kwani alifukuzwa baada ya NEC kushindwa kupanda kuingia daraja la kwanza.
Wengine ni kama Rui Faria, mtu aliyekuwa msaidizi wa Jose Mourinho kwa miaka 17 katika klabu mbalmbali lakini ameshindwa kuwa kocha mkuu wa mafanikio. Tena alipewa nafasi hiyo huko Qatar, akadumu kwa mwaka mmoja na siku mbili tu Al-Duhail.
Msaidizi wa zamani wa Rafa Benitez, Pako Ayestaran naye amekwama kukaa kama kocha kwa zaidi yam waka mmoja katika kazi zote sita za ukocha aliopewa tangu aachane na Mhispania mwenzake 2007. Lakini pia kuna Craig Shakespeare aliyekuwa msaidizi wa Nigel Pearson.
Baada ya kukaa kwa miaka kadhaa kama msaidizi wa Carlo Ancelotti klabuni Chelsea, Paris Saint-Germain and Real Madrid, Paul Clement aliamua kujaribu ukocha mkuu. Alikuwa na haiba kubwa kama kocha na kuchukuliwa vyema, lakini alipochukua ukocha hakuwa na lolote.
Ili kufanikiwa kama kocha kutoka kocha msaidizi, kama anavyosema Arteta na wenzake, inabidi kuwa na uwezo wa kujiweka mbali kidogo na wachezaji lakini kuweka uhusiano mzuri nao. Uweze kuchukua uamuzi mgumu dhidi ya baadhi yao lakini uwahakikishie kwmaba upo nao hasa wakati mnakabiliwa na shinikizo kubwa.
Lazima uilinde haiba yako lakini wakati wa kufurahia na kushangilia uungane kabisa na wachezaji na kuonekana unawafurahia, uwe tayari kurudi nyuma na kupumzika kidogo mambo yakibana kama alivyofanya Pep Guardiola na uwe na uhusiano mzuri na makocha wengine wanaoweza kujazia kwenye upungufu ulio nao.
Ni wazi kwamba ni muhimu kuchagua kazi sahihi kwa wakati sahihi, kwa sababu kocha akishachukuliwa kwamba hawezi na ni mzigo wanaingia kwenye eneo gumu sana na ni vigumu kurudi tena kwenye kazi hiyo kwa ufanisi, na wakati mwingine muda unakuwa umewatupa mkono na umri umekwenda.