BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga wametangaza kumfuta kazi kocha wao Miguel Gamondi kisha kutangaza mpya kuchukua nafasi yake. Kocha mpya wa Yanga ni Sead Ramovic ambaye anajiunga na Yanga akitokea Ligi Kuu ya A frika kusini alikokuwa kikiongoza kikosi cha TS Galaxy. Uamuzi wa yanga umekuja baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 toka Tabora United. Katika makala haya TANZANIASPORTS inakufahamisha zaidi kuhusiana na mwalimu huyo mpya katika Ligi Kuu Tanzania.
TS Galaxy inashika nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu Afrika kusini maarufu kama PSL (Premier Soccer League). Hii ni timu iliyokuwa inafundishwa na kocha Sead Ramovic raia wa Ujeerumani. Msimu uliopita TS Galaxy ilimaliza Ligi ya PSL ikishika nafasi ya sita. Mbele yake kuna miamba kama vile Mamelodi Sundowns, Kaizer Chiefs,Orlando Pirates, Stellenbosch,Supersport United, Polokwane. Msimamo wa Ligi hiyo unaongozwa na Orlando Pirates wenye pointi 21 kutokana na michezo 7 ya Ligi. Nafasi ya pili wapo Mamelodi Sundowns wakiwa na pointi 18, Polokwane (13),Stellenbosch(12),Sekhukhune(10),Chippa United (10),Supersport United (8),Kaize Chiefs (7), Royal AM(7), Golden Arrows(7),Magesi(6),Richards Bay (5),Cape Town City (5),Marumo Gallants((4),Amazulu(4) na TS Galaxy (4). Hiyo ina maana kwamba TS Galaxy inmashikilia mkiani mwa Ligi ya PSL.
Hata hivyo kocha wake Sead Ramovic aliachana na timu hiyo wiki iliyopita ambapo alibainisha kuchoshwa na kufundisha timu inayouza wachezaji wake mahiri. Akizungumza wakati akijiuzulu, kocha Sead Ramovic alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Nimelazimika kuondoka katika klabu ya TS Galaxy kwa sababu kuu moja; siwezi nimeshindwa kuendelea kuwa kocha wa kuzalisha vipaji na wachezaji wazuri halafu wanauzwa kwenda Orlando Pirates,Kaizer Chies au Mamelodi Sundwons. Natamani kuwa na timu yenye dhamira ya ushindani, timu inayofikiria kutwaa mataji kwa kulinda silaha muhimu za mafanikio,”
Sifa kwa Yanga
Ikumbukwe kocha huyo aliwahi kufanya mahojiano na vyombo vya habari wakati wa maadnalizi ya msimu mpya 2024/2025 na kukisifia kikosi cha Yanga. Sead Ramovic alisema kuwa “Young Africans wana wachezaji wazuri sana hasa hasa hawa walioingia kipindi cha pili. Moja ya wachezaji niliovutiwa nao zaidi ni yule aliyeingia amevaa jezi namba 8 na jezi namba 10, ni wazuri mno,”. Maneno hayo yalimtoka baada ya mchezo kati ya TS Galaxy na Yanga uliofanyika huko Afrika kusini ambako vijana wa Jangwani walialikwa kwenye mchezo maarufu dhidi ya Kaizer Chiefs ya nchini humo.
Rekodi zake TS Galaxy
Tangu alipochukua jukumu la kuinoa TS Galaxy, Sead Ramovic ameiongoza katika michzo 76, ampeta ushindi mara 27, kutoka sare mechi 22, amefungwa mechi 27,amefunga mabao 82 na kufungwa mabao 68. Rekodi nyingine ni kumaliza Ligi Kuu akiwa nafasi ya 6.
Maisha ya uchezaji
Alizaliwa Machi 14, 1979 mjini Stuttgart na ana umri wa miaka 45. Miaka ya baadaye alikuja kuwa mchezaji wa nafasi ya golikipa. Wakati wa maisha ya uchezaji alisajiliwa na klabu ya FC Feuerbach na baadaye kujiunga SpVgg Feyerbacj akiwa kijana mdogo. Kuanzia mwaka 1999 hadi 2001 alikuwa mchezaji wa timu ya Stuttgarter Kickers na kucheza mechi 45.
Mwaka 2001 hadi 2004 alijiunga na VFL Wolfsburg na kucheza mechi 36. Mwaka 2004 hadi 2005 alijiunga na Borussia M’glabach ambako alicheza mechi 4. Mwaka 2005 hadi 2006 alikuwa mchezaji wa Kickers Offnbach na kucheza michezo 26. Mwaka 2006 hadi 2010 alichezea klabu ya Tromso katika michezo 110. Mwaka 2010 alikuwa mchezaji wa timu ya Silvaspor na kucheza mechi 10. Mwaka 2011 alijiunga na Metalurh Zaporizhzhia na kucheza mechi 2. Mwaka 2011 hadi 2012 alikuwa mchezaji wa klabu ya FK Novi Pazar alikocheza mechi mbili. Mwaka 2012 alicheza klabu ya Lillestrom katika mechi 29. Mwaka 2013 asajiliwa na Vendsyssel na kucheza mechi 4. Mwaka 2014 alijiunga na Stromsguodset na kucheza mechi tano tu. Jumla amecheza mechi 273 katika ngazi ya klabu.
Kazi ya ukocha
Sead ramovic alianza rasmi kazi ya ukocha mwaka 2021 baada ya kujiunga na klabu ya TS Galaxy ya Ligi Kuu Afrika kusini. Amedumu kwa klabuni hapo miaka mitatu na nusu, ambapo Yanga ya Tanzania inakuwa klabu yake ya pili. Kimsingi huyu ni kocha mchanga, ni tofauti na watangulizi wake kama Miguel Gamondi au Nasreddine Nabi,Cedric Kaze au Mwinyi Zahera. Rekodi zinaonesha Yanga ni klabu yake ya pili katika kazi ya ukocha.
Wasifu wake na wachezaji
Kimsingi wasifu wa kocha mpya ni mdogo kuliko ule wa wachezaji wake anaotakiwa kuwafundisha. Wachezaji hao wana sifa nyingi ikiwemo kutinga fainali ya Kombe la shirikisho. Na zaidi ni kocha mdogo sana mbele ya wasifu wa Yanga.