Utaratibu wa jezi za wachezaji uliowekwa na shirikisho la mpira la kimataifa (FIFA), sheria namba 2 kifungu 35, unasisitiza mavazi mawili tofauti. Vazi la kwanza lazima liwe rangi nzito iliyokolea, na jingine nyepesi. Hazitakiwi zifanane. Utaratibu huu ulifuatwa wakati wa kombe la dunia Juni, nchini Brazil.
Ukiangalia timu 32 zilizoshiriki utagundua mshawasha maaalum kabla michuano kuanza.
Uingereza mathalan baadhi ya wachezaji walipigwa picha na suti na jezi mpya zenye nembo ya simba watatu. Wachezaji wa Ivory Coast na Uruguay walilalamika jezi za kubana sana. Furaha ya Waingereza kwa nembo ya simba au malalamishi ya Wa Ivory Coast na Uruguay ni msisimko unaoambatana na hamu ya kwenda vitani.
Jezi huchangia sana motisha. Mfano mzuri ni mwaka 1996 Manchester United ilipoamua kubadili jezi toka rangi kijivu kurudi nyekundu baada ya kushindwa sana uwanjani maana wachezaji walidai hawaonani.
Tanzania je? Miaka mingapi toka tuliposhiriki kombe lolote kubwa?
Juu ya hapo ongeza tangazo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)kukaribisha mawazo ya jezi mpya kwa timu yetu ya taifa. Zingatia sababu zilizotolewa kwamba rangi samawati nyeusi na kijani haikushikirisha wabunifu. Au sababu za TFF kwamba jezi, “ hazina mvuto na hazionyeshi rangi halisi ya bendera yetu.”
Ni mazungumzo ya kuvutia maana kuna motisha wa kumlipa mshindi wa ubunifu huo shilingi milioni moja. Sawa. Lakini kwa nini hoja imepingwa sana?
Hakuna baya lililosemwa. Ila usongo wa kila Mtanzania ni ushindi. Zingatia mambo yalivyokuwa kabla ya kocha Marcio Maximo kuajiriwa,2006. Hatukuwa na fahari ya timu. Maximo alileta mabadiliko ya kisaikolojia ikiwepo mapenzi ya jezi na utaratibu mpya wa mafunzo. Mwaka 2009 Taifa Stars ilifika michuano ya kombe la Afrika nchini Ivory Coast.
Tukafungwa na Senegal, sare na Zambia na kuichapa Ivory Coast, 1-0. Bao la Mrisho Ngassa.
Kipindi hiki cha Maximo kiliisisimua soka Tanzania lakini baada ya muda vuguvugu limefifia.
Wenzetu wenye dhiki na vita kutuzidi, mfano Wakongo walioshinda michuano hiyo ya Ivory Coast, 2009, wanasonga mbele. Badala ya kujiuliza kwanini tunashindwa kufika kokote tunazungumzia suala la sura, jamani? Tazama maoni ya mtandao wa Facebook.
Wadau wanafoka. “Jezi hazichezi mpira juhudi za wachezaji wa TZ zimefikia ukomo hawafundishiki kama unakubaliana na maneno yangu…”
Au : “Mnataka asilimia 5 ya vilabu kumbe pesa mnazo au mlikuwa mnataka nongwa? Hatukuelewi Malinzi…”
Mwingine: “ Naona hizo hela hazina kazi kwani kubadili jezi ndiyo watacheza mpira mzuri?”
Ama. Sentensi ndogo ndogo.
“Hawana mpya”, “watengeneze za bati”, “wabadilishe mchezo si jezi.”
Na pia “tatizo si rangi wabadili matirio na mvuto.”
Ubadilisjhaji wa muundo wa timu na namna mpira unavyoondeshwa Tanzania
ndiyo fikra inayotakiwa kufanyiwa ubunifu na mashindano. Si suala la mavazi. Ningependa kumalizia kwa maoni ya mdau aliyeoonyesha jazba na hamasa ya nchi. Maoni yanyothibitisha hisia na uchungu wa wengi.
“Jezi hazibadili kitu tunataka wachezaji wajitume kwa nguvu na akili zote. Sio kila mchezo matokeo mabaya mnatuumiza sana na rekodi chafu hata mechi za kirafiki. Hola. Tunakuwa wakiwa bwana. Ahh badilisheni mfumo. Mchezaji anapofundishwa inatakiwa azingatie na ajiongezee kwa juhudi zake binafsi tumechoka. Hakuna furaha bwana.”
Comments
Loading…