Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aipeleka Simba mahakamani..
ALIYEKUWA kocha msaidizi wa Klabu ya Simba, Jamhuri Kihwelo’ Julio’ amesema kuwa amefungua kesi mahakamani akidai fedha klabu hiyo kutokana na kutangaza kumtimua kazi wakati bado ana mkataba.
Julio aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuchukua fomu kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa klabu ya Simba inayotarajia kufanya uchaguzi mkuu Juni 29 mwaka huu.
NIPASHE iliona nakala hiyo ya mkataba wa Julio na Simba iliyosainiwa Julai Mosi mwaka jana na unamalizika Juni 30 mwaka huu.
Julio alisema kuwa yeye bado ni kocha halali wa Simba kwa sababu aliingia mkataba uliosainiwa na Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘ Kinesi’.
Beki huyo wa zamani wa Simba alieleza kwamba amefikia maamuzi hayo kutokana na kikao kilichokaa kumtimua yeye na kumsimanisha Mwenyekiti, Ismail Aden Rage, kubainika kuwa ni batili na Shirikisho la Soka Tanzania ( TFF).
Alisema pia ameamua kuchukua fomu kwa sababu ana uwezo na ameifanyia Simba mambo mengi ikiwamo kufundisha kikosi wakati uongozi unapokuwa na migogoro.
Alieleza pia anaidai Simba Sh .milioni 24 tangu ilipokuwa chini ya Mwenyekiti,Hassan Dalali.
Julio alisema pia amejipanga kuwawekea pingamizi viongozi wanaomaliza muda wao ambao wamejitokeza kuwania kutokana na kuvunja katiba ya Simba kwa kushindwa kuitisha uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ baada ya kutangaza kujiuzulu.
” Pia viongozi hao wanakosa la kumpindua Rage kitu ambacho kilikua ni cha hovyo,” alisema Julio.
Julio alifuatana na mgombea wa nafasi ya Urais, Michael Wambura, aliyekuwa anarejesha fomu jana.
Comments
Loading…