Tembo wa Afrika, Ivory Coast wamepambana dhidi ya Japan waliotangulia kupata bao na kuwashinda 2-1.
Ivory Coast walioneka na kuelemewa katika sehemu ya mwanzo ya mchezo na Keisuke Honda aliwapaisha Japan kwa kiki nzuri ya dakika ya 16.
Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha pili, ambapo kocha Sabre Lamouchi alikuna kichwa juu ya kipi cha kufanya hadi alipoamua kumwingiza Didier Drogba.
Kuingia kwake kulionekana kama hirizi ya Ivory Coast, kwani haikuchukua muda mabeki wa Japan wakaanza kulainika.
Wilfried Bony wa Swansea alifunga bao katika dakika ya 64 na Gervinho akapiga la pili dakika mbili tu baadaye, mabao yaliyotosha kuwapatia alama tatu muhimu kwenye kundi lao.
Bony alisawazisha baada ya kupata majalo ya Serge Aurier, beki wakulia anayecheza Toulouse ya Ufaransa na anayetarajiwa kujiunga na Arsenal kuziba pengo la Bacary Sagna aliyehamia Manchester City.
AlikuwaniAurier tena aliyemimina majalo dakika moja na ushee baada ya ile ya kwanza na kumkuta Gervinho, mchezaji wa zamani wa Arsenal, aliyetia mpira kimiani pasipo ajizi.
Mbinu za kumwingiza Drogba bila kumtoa Bony ziliwafanya Japan wababaike juu ya nani hasa wamkabe, na katika kufanya hivyo wakajikuta wakizidiwa maarifa.
Tembo hao sasa wapo sawa kwa pointi na Colombia kwenye kundi C, lakini Colombia wapo mbele kwani waliwacharaza Ugiriki 3-0 kwenye mechi ya mapema.
Hizi ni fainali za tatu kwa Ivory Coast kushiriki katika Kombe la Dunia lakini hawajapata kuvuka hatua ya makundi, jambo ambalo sasa wamedhamiria, wakitumia wachezaji wakongwe wa kimataifa wanaowika Ulaya.
Ilishangaza kuona Drogba, mchezaji wa Galatasaray aliyepata kuwika na Chelsea akiachwa benchi tangu mwanzo, na wawakilishi hao wa Afrika wakaanza kufungwa.
Japan ndio mabingwa wa Asia na ndiyo timu ya kwanza kufuzu kwa fainali hizi, na kwa hakika walionekana kuwa wenye kasi.