Ukizungumzia mabondia ambao wenye majina makubwa katika ardhi ya Tanzania basi hauwezi kuacha kumtaja bondia Abdallah Pazi au maarufu kama Dullah Mbabe. Bondia huyu kutoka kwenye kitongoji cha Mwananyamala jijini Dar es salaam amejizolea umaarufu mkubwa katika siku za huko nyuma. Dullah kwanza husifika kwa kujivunia asili yake uzaramo na pia huuna misemo ya mapambano yake kwa kutumia misamiati ya lugha ya kizaramo. Dullah amewika kwenye ngumi nchini Tanzania kwa mda wa Zaidi ya muongo mmoja na kuna kipindi kama mapromota walikuwa hawampi sana mapambano lakini kwa sasa amekuwa anapewa mapambano. Alipotea kwa mda kidogo kwenye midomo ya mashabiki wa mchezo wa ngumi lakini kwa hivi karibuni aliibuka baada kushindwa pambano la ngumi nchini Uingereza kwa KO.pambano lake la Machi 31 dhidi ya bondia Callum Simpson ambalo lilifanyika nchini Uingereza alienda kupigana kimya kimya lakini baada ya kupigwa taarifa zake zilishitua wafuatiliaji wa michezo mtandaoni na baadhi yao wakawa wanatoa maoni kwama bondia huyu hana jipya kwani ameshaanza kufikia ukingoni mwa kazi yake ya ubondia. Bondia Karim Said ama maarufu kama Karim Mandonga kupitia katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram alimsifu Dullah Mbabe na kasha kumwambia kwamba yeye na Dullah wakipigwa ni kama wamepiga na wakipiga ni kama wamepiga. Kauli hiyo ilizalisha maoni kwenye ukurasa wake mbalimbali na wengi wao walisema kwamba mabondia hawako makini bali wanafanya ngumi kama utani
Abdallah Pazi kwa sasa ana umri wa miaka 30 na katika hali ya kiuanamichezo umri huo mara nyingi mwanamichezo huwa anaanza safari yake ya kuelekea ukingoni mwa kucheza. Ni michezo michache duniani ambayo mchezaji anaweza kuendelea kucheza vizuri licha ya kwamba atakuwa amezidi umri wa miaka 30. Mchezo kama gofu mchezaji huweza kucheza hata akiwa amezidi umri wa miaka 40 lakini michezo mingi hawezi tena kucheza mechi za ushindani. Dullah Mbabe alicheza pambano lake la kwanza la ngumi za kulipwa mnamo tarehe tarehe 31 ya mwezi disemba mwaka 2013 na kusema kweli hapo awali aliweza kutengeneza mashabiki na wafuatiliaji wengi ambao walivutiwa na kipaji chake. Amekuwa anajipa jina la utani la kujiita kama Rais wa wazaramo kwani kiuhalisia amekuwa ni mwanamichezo ambaye anajivunia asili yake ya uzaramo. Ana jumla ya mapambano 50 ambayo amepigana toka ameanza kujishughulisha rasmi na ngumi za kulipwa. Katika idadi hiyo ya mapambano amefanikiwa kushinda mapambano 34 kwa knockout na kupigwa mapambano 14 na mapambano 2 kutoa draw.
Jina la Dullah Mbabe lilivuma Zaidi sana pale mnamo disemba mwaka 2018 alipoandaliwa pamano dhidi ya bondia mashuhuri wa wakati huo toka Morogoro bwana Francis Cheka. Pambano hilo walikuwa wanagombania ubingwa wa WBF. Pambano hilo Dullah Mbabe alimtwanga Francis Cheka na alishitua ulimwengu wa ngumi nchini Tanzania kwani wadau wengi wa ngumi hawakuamini kile kilichotokea pale ulingoni kwani Francis Cheka alipigwa tena kwa knockout. Pambano hili lilimshitua sana Cheka kwani hakutarajia kupigwa na bondia ambaye alikuwa ndiyo anachipukia kwenye ulimwengu wa masumbwi nchini Tanzania. Pambano lile lilimuathiri kisaikolojia Francis Cheka ambaye kwa wakati huo alikuwa amewabonda mabondia wote wakubwa nchini Tanzania. Cheka aliwapiga mabondia mashuhuri kama akina Rashid Matumla, Japhet Kaseba na wengineo. Baada ya pambano lile Francis Cheka alitangaza kustaafu rasmi ngumi za kulipwa nchini Tanzania.
Baada ya pambano hilo Dullah alizidi kupata mapambano na hata kupata mapambano ya kimataifa ambapo alialikwa kwenda kupigana nchini Urusi alienda akapigana na kisha kupigwa na baada ya kupigwa akatangaza kwama anastaafu ngumi. Pambano hilo alipambana na bondia wa kirusi anayeitwa Pavel Silyagin na pambano hilo lilipigwa mnamo mei 21 mwaka 2021. Licha ya kutangaza kwamba ataacha ngumi baada ya kupata kipigo kikubwa kutoka kwa mrusi huyo ila haikupita mda mrefu sana akarudi tena ulingoni kupambana ngumi.hiyo ilikuwa mnamo Agosti 21 mwaka 2021 yaani miezi mitatu tu baadaye Dullah Mbabe akarudi ulingoni na akapata mojawapo ya pambano kubwa la mwaka huo wa 2021. Alipambana pambano dhidi ya bondia Twaha Rubaha wa Morogoro ama maarufu kama “Twaha Kiduku”.pambano hili lilisisimua sana mashabiki wa mchezo wa ndondi ndani ya nchi na hilo lilichangiwa na zawadi ambayo mshindi wa pambano hilo alilipata pamoja na tambwe za bondia huyo.
Zawadi ambayo mshindi wa pambano hilo alikuwa anapata gari aina ya crown. Pambano hilo Dullah alijitapa sana kwamba atashinda na pia atachukua gari hilo. Dullah alifikia hatua ya kuita wapiga ngoma za kizaramo mtaani kwake na wakapiga ngoma hadi kukesha na kutangaza hiyo ni sherehe kabla ya kwenda kuchukua gari ya Crown. Usiku wa pambano Dullah hakuamini macho yake alipigwa na bondia wa Morogoro. Kupigwa huko na bondia huyo wa Morogoro kukamfanya Twaha Kiduku akawa ni nembo mpya ya ngumi ya Morogoro kwani aliwalipia kisasi kwa Dullah ambaye alimpiga mwana morogoro mwenzie Francis Cheka. Pambano hilo lilimfanya Twaha kiduku kuwa ni staa wa Morogoro kwani wakati aliporudi Morogoro alipkewa kifalme na wakazi wa Morogoro na siku alipopokelewa mapokezi yake yaliyashinda haya ya Afande Sele pale aliposhinda ushindi wa mashindano ya mfalme wa rhymes mwaka 2004.
Baada ya hapo akapata mapambano mengi ambayo mengi kati ya hayo alipigwa hususani yale makubwa na ya kimataifa ila ameweza kushinda mapambano ya ndani. Akapoteza pambano mara mbili dhidi ya bondia kutoka nchi ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo aitwaye Erick Katompa na pambano la pili baada ya kupigwa na kushindwa kabisa akiwa nje alitaka kufanya fujo ili kurudi ulingoni kwa ajili ya kuendelea na pambano ila mabaunsa walimzuia kufanya hivyo. Na baada ya hapo tena akapoteza pambano la kimataifa dhidi ya Callum Simpson. Dullah Mbabe ni bondia ambaye alibebea matumaini ya watanzania wengi ambao ni mashabiki wake kwama siku moja atakuja kuwa nembo ya Tanzania kwenye medani za kimataifa ila hajatimiza kiu ya mashabiki wake. Swali linabaki je anaweza kutimiza hilo au amefikia kikomo cha uwezo wake?
Comments
Loading…