“Ali Kiba kasajiliwa na Coastal Union”. Ndilo neno la kwanza ambalo nililisikia, nilibaki kimya sikutaka kusema chochote kuhusu usajili wake kwa sababu niliipa akili nafasi ya kutafakari.
Sikutaka kujipa majibu ya maswali mengi yaliyokuwa yanakuja kichwani kwangu kwa sababu niliamini sitokuwa na majibu bora. Muda niliupa nafasi, na akili yangu ikapata nafasi ya kutafakari mengi sana.
Tafakuri ambayo ilibeba maswali mengi sana, moja ya swali kubwa ambalo lilikuwa linazunguka katika kichwa changu ni “namna gani ambavyo anaweza kufanya muziki huku akicheza mpira wa miguu bila kushuka kwenye mpira na kwenye muziki.
Kipi walifikiria wasimamizi wa kazi zake za muziki mpaka wakampa ruhusa ya yeye kucheza mpira wa miguu? Hawakuona madhara hasi ambayo yanaweza kuutokea muziki wake kipindi ambacho atakuwa anaitumikia Coastal Union?
Maswali haya yalikuwa mazito kwangu na yalifanya kichwa changu kiwe kizito, sikuta kutoa majibu ya maswali haya kwa sababu majibu yake yangeonesha hitimisho la Ali Kiba litakuwaje kwenye kazi yake ya muziki.
Fundo moja la maji lilihitajika kuutuliza moyo wangu ili ujazwe na vazi la subira, macho yalifunika mboni zangu, sauti ikapita sikioni mwangu ikiniuliza kwetu sisi mpira tunafanya biashara au kama kujifurahisha nafsi zetu?
Hii habari ya Alikiba kucheza katika ligi kuu Tanzania bara tumeipokeaje?. Hakuna kitu chochote tulichokifikiria kuhusu ukubwa wa jina wa Alikiba?
TFF wamejipangaje kulitumia jina la Alikiba katika kuitangaza ligi yetu katika sura ya kibiashara?. Au kwetu sisi kazi yetu ni kutengeneza ratiba, kuandaa waamuzi na kuhakikisha ligi yetu inachezwa?
Tunaitengenezaje ligi yetu iwe na mvuto?, tunafikiriaje kuongeza hamasa ya kufuatiliwa kwa ligi yetu ?, au tulipo ndipo tulipoishia na hatutakiwi kuiandaa miguu kwa ajili ya kupiga hatua nyingine?.
Akili zetu zinatakiwa zitambue kuwa kutangaza bidhaa yako ni sawa na kitendo cha mwanadamu kuvuta pumzi. Havuti pumzi mara moja tu na kuacha, pua zake hutakiwa kuvuta pumzi mara kwa mara ili kuongeza urefu wa uhai wake.
Hii ndiyo picha halisi ya kutangaza bidhaa yako, unatakiwa kufikiria kila muda jinsi ya kutangaza bidhaa yako katika hali ya ukubwa na upya kila siku.
Uwepo wa Ali Kiba katika ligi kuu Tanzania bara ni jambo kubwa ambalo linachukuliwa katika ukawaida usio wa kawaida.
Bango la ukawaida linatakiwa likunjwe na libebwe bango la umuhimu wa Alikiba kwenye ligi yetu. Tutumie nafasi hii kuhakikisha mashabiki wa muziki wake ambao hawakuwa wapenzi wa mpira wa miguu waweze kuwa wateja wa bidhaa ya ligi kuu Tanzania bara.
Siyo dhambi kwa bodi ya ligi na shirikisho la soka Tanzania bara TFF kumpa Alikiba ubalozi wa ligi yetu.
Ubalozi ambao atautumia yeye kuwaambia mashabiki wake ubora na uzuri wa bidhaa ya ligi kuu ili wateja wapya wapatikane kwenye hii bidhaa ya mpira wa miguu.
Kombe la dunia limekuja na mafunzo mengi lakini moja ya funzo kubwa ambalo tulipata na jinsi ambayo wanawake warembo walivyokuwa wanaingia kwa wingi katika viwanja vya mpira wa miguu.
Kuwahamasisha watu kama hawa kunahitajika watu ambao wanasura za kibiashara zenye mvuto kwao. Hapana shaka Ali Kiba yuko kwenye hii nafasi, nafasi ambayo imemfanya awe na mashabiki wengi wa kike kwenye muziki wake. Mashabiki ambao wanaweza wakageuzwa kama wafuasi wa Alikiba, kila aendapo na wao wapo na hii itakuwa na msaada mkubwa kwenye bidhaa yetu ya ligi kuu.
Inawezekana Ali Kiba asifanye kitu kikubwa ndani ya uwanja ila akitumika vizuri atafanya vizuri sana nje ya uwanja.
Hata Coastal Union wanatakiwa kufikiria kwa upana. Ule wakati wa kumtumia mchezaji ndani ya uwanja peke yake umepita. Huu ndiyo wakati wa kulitumia jina la mchezaji ndani na nje ya uwanja.
Mkwakwani panaweza kufanyika utambulisho wa Ali Kiba na Coastal Union kuingiza fedha ambazo zitakuwa na msaada kwao.
Ali Kiba ana mashabiki wengi nchi nzima. Huu ndiyo mtaji kwa Coastal Union kupata mashabiki na wanachama wengi kupitia jina la Alikiba.
Ushawahi kuona mtu anahama timu na kwenda timu fulani kwa sababu ya mchezaji fulani?. Huu ndiyo udhaifu ambao mashabiki wengi wa mpira wako nao. Kupenda kupitiliza!, wengi hupenda na wako radhi kwenda kila sehemu ambayo mchezaji fulani anapoenda.
Ndipo hapo hili litakuwa faida kwa Coastal Union kupata mashabiki wapya, mashabiki ambao watakuwa mtaji mkubwa kwao wao kwa sababu watakuwa na uwezo wa kuuza bidhaa zenye nembo ya klabu kwa sababu ya Ali Kiba. Tujifunzeni kuwa na mapato mbadala tena kipindi ambacho tunapokuwa na watu wenye majina makubwa kwenye timu zetu.