in , ,

HIKI KITABU CHA GEORGE WEAH TUTAKIANGALIA NA KUKIPUUZA.

HIKI KITABU CHA GEORGE WEAH TUTAKIANGALIA NA KUKIPUUZA.

Liberia ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na raisi mwanamke.

Raisi ambaye aliifanya Liberia kujivunia kwa rekodi hiyo.

Bi. Elen Jonhson mshindi wa tunzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel.

Tunzo yenye heshima kubwa duniani, ambapo alifanikiwa kuileta nyumbani
kwao Liberia.

Kwenye ardhi ambayo ilimwamini na kumpa jukumu kubwa la kuliongoza
Taifa hilo kwa kumfanya kuwa Mwanamke wa kwanza kuongoza nchi katika
bara la Afrika.

Heshima ambayo pia kapewa George Weah kuwa mwanasoka wa kwanza
kuongoza nchi katika bara la Afrika.

Mshindi wa tunzo ya Ballon D’or na FIFA player of the year.

Akiwa Mwafrika pekee kuchukua tunzo ya mchezaji bora wa dunia, ni
historia ya kujivunia aliyoiweka wakati anacheza mpira.

Kila mtu alifurahia kuona na kujivunia akiweka historia hii ambayo
itaishi kizazi hadi kizazi.

Akiwa uwanjani alipigana ili ahakikishe kuwa atakumbukwa na vizazi
vingi duniani.

Ndiyo maana alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa klabu bingwa barani ulaya ( UEFA)

Hii yote ilikuwa ni kutumia nafasi aliyokuwa nayo kwa wakati huo
kufanya kitu bora , kitu ambacho kitaishi.

Alifanikiwa kwenye hilo, historia yake ya soka iliweka kitu ambacho
kinaishi mpaka leo, kitu cha kuheshimika na jamii nzima duniani.

Akili yake ilipokuwa uwanjani ilikuwa inawaza atafanya nini baada ya
kutundika viatu vyake?

Alijua ipo siku moja hatoweza kucheza mpira katika kiwango bora
alichokuwa anakionesha kipindi kile.

Alijua nguvu za kukimbia na mpira kuna siku zitamwishia.

Jicho lake la kufunga magoli litatiwa upofu siku moja.

Akili yake ikawa inaumiza kupata njia sahihi ya kujikimu baada ya yeye
kustaafu soka.

Akaanza kujitengenezea mazingira mazuri ya kwenda shule ili akapate
elimu ambayo ataitumia baada ya kufanikiwa kumaliza kucheza mpira.

Elimu ambayo imemwezesha leo hii kuwa mwanasoka wa kwanza Afrika kuwa
raisi wa nchi.

Hakikuwa kitu chepesi ila ni malengo ambayo alijiwekea ili asitaabike
baada ya kumaliza kucheza mpira.

Hii hadithi ni tofauti na hadithi za wachezaji wetu.

Wachezaji wetu hapa nyumbani wanacheza katika mazingira ambayo ni duni.

Mazingira ambayo hata kipato wanachokipata kupitia mpira ni kipato kidogo.

Kiasi kwamba wakistaafu huangaika sana, huwa na maisha magumu mtaani.
Maisha ambayo hata hela ya kujitibu maradhi wanayokuwa wameyapata
inakuwa ngumu.

Kukosa pesa nyingi baada ya kustaafu hakukupi ufinyu wa wewe kufikiria
kuwaza kufanya kitu cha ziada ambacho kitakusaidia katika maisha yako.

Kila siku tumekuwa tukilia kuwe na vituo vya kuibua, kulea na kukuza
vipaji vya mpira ili tufike sehemu ambayo tunaitamani kufika katika
mafanikio ya mpira wetu.

Lakini wachezaji wetu baada ya kustaafu hushindwa hata kwenda kuchukua
kozi za ukocha kwa ajili ya faida yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Hubaki vijiweni na kujisifu kuwa walikuwa mahiri kipindi walipokuwa
wanacheza mpira huku kahawa ikipita kooni mwao.

Kujisifu pekee hakutoshi, cha muhimu ni namna gani unatumia jina lako,
akili yako ya mpira na ya kawaida kujiingizia pesa baada ya kustaafu
mpira.

Tuko katika dunia ambayo kila kitu ni biashara na kuna biashara nyingi
sana ambazo zimeibuliwa kipindi hiki.

Na moja ya njia ya kukuza biashara ni kuitangaza, na huwezi kuitangaza
katika mazingira ambayo hayatokupa nafasi ya biashara hiyo kukua na
kumfikia mteja kwa wepesi.

Njia nzuri ya kumfikia mteja kwa wepesi ni kutumia jina maarufu
kutangaza bidhaa yako, wachezaji wetu hutengeneza majina maarufu
kipindi wanapokuwa wanacheza.

Wanashindwa kuwa na wasimamiza wa majina yao, wasimamizi ambao
watahakikisha majina ya wachezaji wao kutimika kibiashara kwa
kuwatafutia nembo za bidhaa mbalimbali ili watangaze.

Hakuna kampuni isiyotaka bidhaa yake ifike mbali , hakuna kampuni
isiyopenda kuona mtu mwenye jina kubwa akiwa balozi wa bidhaa yake.

Tunashindwa mpaka na bongo movie ambao wameamua kuchukua mpaka
matangazo ya makampuni ya michezo ya kubashiri katika michezo.

Makampuni ambayo kiuhalisia wanamichezo ndiyo walitakiwa kutawala kama
mabalozi wa hayo makampuni.

Lakini inakuwa kinyume chake kwa sababu wengi wao hawajiandai namna ya
kuishi baada ya mpira.

Tusiishie kumsifu George Weah tunachotakiwa na sisi tujiulize
tutafanya kitu gani kikubwa baada ya kumaliza kucheza mpira?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MICHAEL CARRICK KWENYE UBETI MMOJA NA FUNDI AKILI

Tanzania Sports

KIPI KIMEISIBU CHELSEA?