Duniani kuna michezo mingi sana ila kwa Bara la Afrika michezo inayopendwa zaidi ni miwili mpira wa miguu na mchezo wa ngumi.
Tangu enzi na enzi mchezo huu umekuwa ukipendwa kutokana na msisimko wake.
Ilifika wakati hadi pambano moja kubwa limefanyika nchini Kongo katika ya Mohamed Ali na George Forman ambalo limepewa jina la ‘The Rumble in the Jungle’ .
Walio wengi mchezo huu wanaujua kwa juu juu kuna vitu vidogo hawavichukulii kwa ukubwa unaostahili.
Hawajui namna ngumi inavyohesabiwa wapi panatakiwa wasipaguse wakati wanapigana.
Leo hii tunakupatia kipengele kidogo cha ‘TKO’ na ‘KO’, kisha tunakupa mabondia kadhaa walioweza kuzifnya ‘KO’ na ‘TKO’ kuwa tamu zaidi kuziangalia na kuhadithia.
Ngumi au ndondi kama ambavyo wengi hupendelea kuita hivyo, ni moja ya michezo iliyojikusanyia mashabiki wengi karibu ulimwenguni kote, kutokana na namna ambavyo mchezo huu huchezwa hasa pale wapinzani wawili wanapokutana ulingoni kuoneshana ubabe.
Pale mabondia wanapanda ulingoni aidha katika pambano la kuwania ubingwa au hata kumaliza ubishi, mashabiki wengi hupenda kuona bondia mmoja akipigwa kwa ‘KO’ au ‘TKO’, ingawaje baadhi yao hupenda kushuhudia pambano likimalizika kwa raundi zote, ili waendelee kuona ngumi zikipigwa.
Pamoja na hayo, ukweli usiopingika kwamba wengi wao hawafahamu maana ya ‘KO’ na ‘TKO’ uhalisia na pengine hata jinsi inavyopatikana au bondia anavyoshinda kwa aina hiyo ya ushindi.
Leo tutaangazia mabondia bora wa muda wote duniani ambao wanaongoza kwa kushinda mapambano yao kwa KO, baadhi yao wamefariki dunia lakini rekodi zao bado zinaendelea kusalia kwenye historia ya mchezo huu wa masumbwi duniani.
Lakini kabla hatujakwenda kuangalia listi ya mabondia hao, ni vyema tukafahamu maana halisi ya neno ‘KO’ na jinsi bondia anavyoweza kushinda kwa ‘KO’ lakini pia tofauti iliyopo kati ya ‘KO’ na ‘TKO’ katika mchezo huu pendwa duniani.
NINI MAANA YA ‘TKO’ NA ‘KO’
Tuanze na neno ‘KO’ ni kifupisho cha neno la kizungu (Knockout), ambayo hutokea iwapo bondia atadondoshwa kwenye turubai la ulingoni (Canvas), na kisha akashindwa kunyanyuka kwa miguu yake mwenyewe ndani ya muda maalamu uliowekwa kisheria, kawaida kwa sababu ya Uchovu, maumivu au kuchanganyikiwa.
Iwapo bondia ataangushwa chini na akashindwa kuendelea na pambano ndani ya sekunde kumi baada ya kuhesabiwa na mwamuzi wa pambano hilo, basi bondia huyo atahesabika kwamba amepigwa kwa ‘KO’ na mpinzani wake atazawadiwa ushindi wa ‘KO’.
Kwa upande wa ‘TKO’ ambayo pia hufahamika kama ‘Stoppage’, ni kifupisho cha neno la kizungu kwa hii ‘TKO’ ni ‘Technical Knockout’, hii hutokea pale mwamuzi wa pambano husika ataamua kukatisha pambano wakati raundi ikiendelea baada ya kujidhihirishia kwamba bondia husika hawezi kuendelea na pambano, kutokana na sababu za kiusalama kwa bondia huyo huku akaona iwapo bondia huyo ataendelea kupigana kuna uwezekano mkubwa wa kudhurika zaidi au hata kupoteza maisha, basi bondia huyo atahesabika kwamba amepigwa kwa ‘TKO’.
Wakati mwingine huenda amekatika juu ya jicho hivyo inaweza kumletea madhara nayo inaweza kuwa sababu ya ‘TKO’.
Rejea pambano la septemba 9,2018 kati ya Bondia Mtanzania Hassani Mwakinyo dhidi ya Sam Eggington, ambalo Mwakinyo alishinda kwa ‘TKO’ ya raundi ya pili.
Sehemu nyingi ‘TKO’ hutokea pia iwapo bondia ataangushwa chini mara tatu katika raundi moja ya pambano husika.
Kitu muhimu cha kuzingatia hapa ni kwamba, iwapo bondia ataangushwa chini na akashindwa kuinuka mwenyewe ndani ya sekunde kumi basi atakuwa amepigwa kwa ‘KO’, na iwapo bondia atapigwa na mwamuzi akajitosheleza kwamba bondia huyo hawezi kuendelea na pambano kwa usalama wake basi atakuwa amepigwa kwa ‘TKO’.
Nadhani hadi kufikia hapo utakuwa umepata mwanga wa maana na tofauti ya ‘TKO’ na ‘KO’ hata ukikaa kijiweni kubishana na watu kuhusu hilo utakuwa unazungumza au kubishana juu ya kitu ambacho unakifahamu, nah ii ndio raha ya kijiwe cha ndondi, sasa turudi kwenye wakali wa ‘KO’ wa muda wote duniani.
ROCKY MARCIANO
Jina lake kamili anaitwa Rocco Francis Marchegiano wengi wanamfahamu kwa jina la Rocky Marciano, ni bondia bora na mkali wa ‘KO’ katika historia ya masumbwi duniani, katika historia yake amecheza mapambano 49, 43 akishinda kwa KO, na ndiye Kinara wa ‘KO’ dunini, inagwaje wataalamu wengi wa ngumi wanajaribu kutompa hadhi anayostahili yeye binafsi na hata rekodi yake hiyo.
Kwa kigezo kwamba wakati anachezea uzito wa juu miaka ya nyuma, ambapo inaelezwa kilikuwa ni kipindi ambacho mabondia wengi wa uzito huo walikuwa dhaifu sana, inagwaje aliwafanikiwa kuwapiga kwa ‘KO’ mabondia wakubwa, Kama vile Joe Louis, Jersey Joe Walcott, Ezzard Charles na Archie Moore, ambapo alifariki Agosti 31,1969 Newton,lowa Marekani.
MIKE ‘IRON’ TYSON
Mwanzoni mwa miaka ya 1985, Mike Tyson alikuwa ni bondia bora na mkali wa ‘KO’ ambaye dunia ilipata kumshuhudia, ni bondia aliyekuwa na kasi, nguvu na ngumi zenye madhara, alicheza jumla ya mapambano 58, akashinda mapambano 50, 44 kati hayo alishinda kwa KO, na alipoteza mapambano 6, 5 kati hayo alipigwa kwa ‘KO’ na mawili ni (contest) yaani hayakupata ushindi au hayakumalizika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vurugu.
Wengine wakali wa hayo mambo ni mfalme hayati Muhamad Ali, huyu alikuwa anakuchapa huku anaongea na wewe, alikuwa mkali sana na alipata heshima kubwa katika mapambano ya ngumi.
Mimi binafsi namkubali Mike Tyson maana alitupa raha sana huyu mwamba. Mapambano yake hayakuwa yanachukua muda mrefu ukichelewa kukata tiketi ukiingia ulingoni unakuta mwana siwako yaani kashapiga ndani ya dakika moja na mpambano umeisha.
Alianza kupoteza dira alipopigwa na Lenox Lewis mwaka 2002 baada ya hapo ndio akaanza kuchapwa sana.
Tyson mwenyewe alipenda aina ya ngumi za huyu mwamba na aliwahi kusema kuwa anamkubali sana.
Hayo machache tuyaonje tu tutakuja na mengine mengi yajayo hadi tufike mabondia kumi.
Lakini wewe nani unayemkubali zaidi katika mapambano ya ngumi unaweza kuungana nasi kwa kutoa maoni yako chini.
Comments
Loading…