*Swansea watwaa Capital One Cup
*Man City wawachapa Chelsea 2-0
Huku hisia zikiwa bado juu Arsenal, nyota wake wa zamani, Thierry Henry anatarajiwa kurudi kama kocha.
Henry ambaye mkataba wake New York Red Bulls unamalizika baadaye mwaka huu, atafanya kazi chini ya Arsene Wenger.
Pamoja na kwamba mabosi wa MLS wanataka Henry abaki Marekani kwa soka, Henry ambaye ni mfungaji bora katika historia ya Arsenal amedhamiria kurejea Emirates.
Habari hizi zinakuja wakati nahodha aliyempokea kijiti, Cesc Fabregas anayekipiga Barcelona ya Hispania, naye akisema ikitokea akaondoka Camp Nou haendi popote zaidi ya Arsenal.
Tangu kuondoka kwa Henry kwenda Barcelona, amekuwa na mawasiliano ya karibu na Wenger ambapo mwaka jana alirejea kwa mkopo Arsenal kucheza.
Inasemekana Wenger amempangia Henry kunoa kikosi cha timu ya vijana, japokuwa majukumu yake kamili bado hayajajulikana.
Bodi ya Arsenal, chini ya kibopa mwenye hisa zaidi, Stan Kroenke inatarajiwa kumpa Wenger kitita cha pauni milioni 70 kwa usajili majira ya kiangazi.
Katika tukio jingine, Swansea City wametwaa Kombe la Ligi (Capital One Cup) baada ya kuwacharaza Bradford City mabao 5-0.
Ilikuwa fainali ya kihistoria kwenye uwanja wa Wembley, ikikutanisha timu zilizofika hatua hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Swansea walitawala mchezo huo tangu mwanzo, tofauti na mechi zilizopita za Bradford kuangusha vigogo, ikiwa ni pamoja na Wigan, Arsenal na Aston Villa.
Mabao ya Swansea yalifungwa na Nathan Dyer (mawili), Michu na Jonathan De Guzman mawili. Palitokea ubishi mkubwa kati ya De Guzman na Dyer, wakigombea kupiga penati baada ya golikipa wa Bradford, Matt Duke kumwangusha De Guzman aliyeng’ang’ania mpira ili apige penati.
Dyer alilalamika akitaka kupiga, ili aweke rekodi kwa kufunga mabao matatu (hat-trick), lakini De Guzman naye alitaka kuonekana, akapiga na kufunga.
Katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL), mabingwa watetezi, Manchester City wamewafunga Chelsea mabao 2-0, huku golikipa Joe Hart akiokoa penati ya Frank Lampard, baada ya kipa huyo kumwangusha Demba Ba aliyempoteza maboya beki Kolo Toure.
Mdogo wake Kolo, Yaya Toure aliwatanguliza mbele City kwa bao safi kabla ya Carlos Tevez aliyeingia kipindi cha pili kupigilia msumari wa mwisho kutoka umbali wa yadi 20.
City sasa wamepunguza pengo dhidi ya vinara wa EPL, Manchester United kutoka pointi 15 hadi 12 wakati Chelsea wanaweza kutupwa nafasi ya nne Jumatatu hii ikiwa Tottenham Hotspurs watawafunga West Ham United.
Katika mechi nyingine ya EPL, Newcastle United wanaopigana kuondoka maeneo ya chini ya jedwali la msimamo wa ligi, wamewafunga Southampton kwa mabao 4-2.
Newcastle wamefikisha pointi 30 na wanashika nafasi ya 14 wakati Southampton wamebaki na pointi zao 27 na kushuka hadi nafasi ya 16.
Comments
Loading…