in

Hatutaki kuona michezo ikiendeshwa kwa mazoea

WAKATI Waziri Mkuu wa Tanzania aliyejiuzulu, Edward Ngoyayi Lowassa anaingia madarakani, alikwenda ofisini na kuwaambia wafanyakazi wa ofisi yake kubadilika, na hataki kuona wakifanya kazi kwa mazoea.

Huo ulikuwa ujumbe wa kwanza wa Lowassa kwa wafanyakazi wake. Waziri Mkuu huyo ametema kibarua chake kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Richmond. Hayo ni masuala mengine, hatutaki kwenda huko.

Hapa tunamwangalia Leonard Thadeo, Katibu Mkuu wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa, BMT ambaye aliwahi kuwa Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu.

Thadeo kwa sasa amepanda cheo baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania. Tunampongeza Thadeo kwa uteuzi huo kwani ni moja ya hatua kubwa ya maendeleo katika maisha ya kila siku.

Kimsingi, wako wengi wenye uwezo katika michezo, lakini kutokana na uadilifu, uchapakazi na umakini wa kazi, serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imemuona Thadeo kuwa ndiye anayefaa kushika nafasi hiyo nyeti ya Ukurugenzi wa Michezo Tanzania.

Ni wazi kuwa Thadeo ana uzoefu mkubwa. Pamoja na rekodi zake, itakumbukwa umakini wake alipokuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu ambako baadaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, BMT baada ya kufariki kwa aliyekuwa Katibu Mkuu, Mohamed Lutta.

Itakumbukwa baada ya kuteuliwa, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa changamoto kubwa inayomkabili mbele yake ni kuhakikisha michezo inasimama kama ambavyo kila Mtanzania na hasa mpenda michezo anataka kuona.

Akijitathamini baada ya uteuzi, anasema, katika uteuzi wake, kimsingi, wapenzi wengi wa michezo wanatarajia kuona mabadiliko makubwa katika sekta ya michezo kwa kuona michezo mingine mbali na soka inafanya vizuri. Mimi naongezea, tunataka tuone kweli kuna mtu kaingia Kurugenzi ya Michezo.

Thadeo pia alishukuru kwa kuteuliwa na kusema uteuzi wake haukuja vivi hivi tu, bali ni kutokana na jitihada zake katika utawala wa michezo na kuona kuwa mchango wake ni muhimu hasa katika suala la kuendeleza michezo Tanzania.

Kwa kuwa uteuzi wake umeanza katikati ya utawala wake, BMT, itakuwa vema akazimaliza kwanza, yale aliyoyaanzisha ikiwemo ya kuzunguka katika badadhi ya mikoa na wilaya zake kuangalia shughuli za michezo zinakwendaje na zaidi kupitia sera ya michezo.

Akiwa huku juu, kwanza ni kusimamia na kuyaendeleza yale ambayo yameanzishwa na viongozi waliopita, Henry Ramadhani ambaye amestaafu.

Sasa, kwa kutumia ukurugenzi, tunaamini atakuwa na nguvu kwa hili la kuendeleza michezo. Kwa hapa tunataka kumwonyesha hawa wenye mlengo wa Michezo ya Olimpiki, Madola na Michezo ya Afrika.

Katika mtiririko wa michezo ya Olimpiki ama Madola na ile ya Afrika kuna vyama ambavyo ni wazi vinaangukia katika michezo hiyo.

Pamoja na kwamba tunaambiwa umasikini umetawala katika vyama vya michezo, kuna haja ya kuwa na muundo mpya ili kuendana na sera ya michezo na utawala wa vyama vya michezo.

Muundo mpya wa vyama utaviwezesha kujitengenezea mazingira ya kuwa na viongozi bora na hata kulingana na elimu ya michezo na utawala na ambao wataweza kuwa na vitega uchumi vya chama ikiwa ni mojawapo ya njia za kuingiza chama mapato kwa maendeleo yake.

Hii itasaidia katika mambo makubwa matatu. Kwanza vyama vitakuwa vinajiendesha na hapo vitaweza kujipangia taratibu zake za kujiendesha ikiwemo kufanya uchaguzi na mashindano na kushiriki mashindano ya kimataifa.

Pili, vyama vitaipunguzia mzigo serikali, kwani inapofika wakati wa mashindano, lawama huelekezwa serikalini wakati vyenyewe ni vyama vya hiari na vinatakiwa kujipanga, kwakuwa serikali inasaidia tu.

Tatu vyama kujikamilisha katika masuala ya kifedha na utawala wake, vitakuwa vimejitengenezea mazingira mazuri ya kuwa na program endelevu na zaidi ni kuwa na vijana.

Katika michezo ya Afrika, Madola na Olimpiki, kwa nchi kama Tanzania ingeweza kupeleka wanamichezo wengi, lakini ni kutokana na kutokuwa na umakini kujipanga katika hili, tumeshindwa kufanya vizuri. Hapa wazi tunawatupia lawama viongozi kwa kuwa si watendaji halisi.

Kwa kutumia rungu la Ukurugenzi, tunadhani Thadeo angeanza kukipekua chama kimoja baada ya kingine, kujua huko waliko wanafanya nini, program zao zikoje, viongozi waliopo madarakani wanawajibika kikamilifu ama ndiyo wale walioingia madarakani kwa kupata ’ujiko’? na je katiba zao, msajili yuko makini nazo?

Hatutaki kuona viongozi wako madarakani kwa kujaribu wakati hawawezi. Viongozi wengi wanaingia madarakani wakisubiri safari za mikutano ya kimataifa lakini hawataki kufanya kile kilichowaingiza madarakani pamoja na kuangalia fedha za kujinufaisha.

Kwa ujumla, wanakuwa watengenezaji wazuri wa maneno pindi wanapoomba kura kutoka kwa wajumbe lakini hakuna kitu. Serikali ilitangaza sera ya michezo, lengo ni kuhakikisha michezo inasambaa Tanzania na ukamilishwaji wake ni kupitia vyama vya michezo ambavyo baadhi yake kwa sasa havina mwelekeo katika majukumu yake.

Naamini kuingia kwa Thadeo katika eneo nyeti la michezo, kutaleta sura mpya na mabadiliko katika vyama vya michezo kama yeye mwenyewe alivyosema kuwa tunaomtazama, tunataraji kuona mabadiliko.

Ifike wakati walioingia madarakani wajutie nafasi zao, kuwa kwanini waliamua kuwania uongozi na wakaingia madarakani? Ama vinginevyo waachie ngazi wawapishe wengine ili tuanze moja kwa kupata viongozi wa kweli wenye mwelekeo katika maendeleo ya michezo.

Kamwe hatuwezi kupiga hatua kwa viongozi walioingia madarakani kwa fasheni ama kutafutia ujiko, hatuwezi kupiga hatua kwa viongozi wasiokuwa na misheni wala visheni katika michezo pamoja kutojua utawala wa michezo. Kiongozi lazima ajue a, b, c za uongozi na utawala wa michezo.

Tunarejea kauli ya Waziri Lowassa kuwa hatutaki kuona mambo yanafanyika kwa mazoea. Ni wazi tukitaka kuendelea lazima hayo na mengine yamulikwe na tuondokane na kufanya kazi kwa mazoea, lazima tutapiga hatua.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Singapore lights way to F1 future

Wenger proud of attacking legacy