Homa ya nani atakuwa kocha Manchester United kuanzia kiangazi kijacho
imeanza kupanda, huku kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho
akipewa nafasi kubwa miongoni mwa washabiki.
Habari zinasema kwamba ameshaanza mazungumzo na Mashetani Wekundu kwa
ajili ya kuchukua mikoba ya Louis Van Gaal ambaye ameshikilia msimamo
wa kuendelea na kazi hadi mkataba wake umalizike.
Homa nyingine ni juu ya nani atachukua mikoba ya Guus Hiddink ambaye
ni wa mpito Chelsea, aliyeingia kwa ajili ya kufanya ‘ukarabati’ baada
ya Mourinho kuanza vibaya msimu na kuingia Desemba akiwa hoi na vijana
wake.
Joto linapanda zaidi kutokana na ukweli kwamba Manchester City
wameamua kuachana na Manuel Pellegrini mwisho wa msimu na kumtangaza
mapema kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola kwamba atawanoa vijana
wao.
Hali hiyo inawafanya Manchester United kufikiria mara mbili,
ikizingatiwa kwamba katika uongozi na wakongwe wa klabu kulipata
kuwapo mgawanyiko iwapo Mourinho apewe nafasi hapo, wakiona kwamba
atabadili chapa ya klabu na mtindo wa timu.
Tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson bado Old Trafford hapajatulia,
baada ya Ryan Giggs kupewa mikoba kwa muda kisha akaingia David Moyes
aliyeshindwa au kutopewa nafasi ya kufanya vyema, ama na wachezaji au
na uongozi akafukuzwa.
Van Gaal amekuwa anakosa uendelevu ambapo pia mtindo wake wa soka
hauwapendezi Old Trafford, kiasi kwamba hata wachezaji waandamizi
wamepata kumvaa na kumtaka abadili mfumo, ili wacheze soka ya
kushambulia.
Wakati City wameshatulizana, wakimpata mmoja wa makocha bora na
wanaosakwa zaidi duniani, United na Chelsea bado wamebaki na alama za
kuuliza, huku Arsenal wakiwa hawatarajii jipya zaidi ya kuendelea na
mkongwe Arsene Wenger.
Habari za sasa ni kwamba kuna mwelekeo wa Mourinho kupewa nafasi
United, kwa maelezo kwamba ndiye mwenyewe uwezo wa kukabiliana na
mbinu za Guardiola na hata kukifunga kikosi chake, kama alivyopata
kufanya enzi za The Specia One akiwa Real Madrid na Inter Milan.
Tetesi zinakwenda mbali zaidi sasa na kutaja hata mshahara, zikieleza
kwamba Mreno huyo atalipwa pauni milioni 15 kwa msimu, zikiwa ni pauni
milioni sita pungufu ya Guardiola. Mourinho, 53, inaelezwa kwamba
atamwagiwa fedha hadi pauni milioni 300 kwa ajili ya usajili.
Wasivyokuwa na dogo, wachunguzi wanasema kwamba tayari Mourinho
amemwambia Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa United, Ed Woodward kwamba
anataka kuwauza viungo Juan Mata, 27 na Marouane Fellaini, 28.
Ikumbukwe kwamba Mourinho ndiye alimweka kando Mata akiwa Chelsea
kisha kumuuza United.
Mgawanyiko upo bado United, na kuna madai kwamba kocha msaidizi Giggs
ataondoka ikiwa Mourinho atapewa nafasi hiyo, akiamini kwamba ama
wangepaswa kuendelea na Van Gaal wakati yeye akijifunza zaidi au apewe
timu mwenyewe Giggs. Zipo habari pia kwamba, Mourinho yupo tayari
kufanya kazi nje ya Ligi Kuu.