Kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola anadaiwa kukubaliana na wamiliki wa Manchester City kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrini Etihad msimu ujao.
Habari zilizonukuliwa na mtandao wa beIN Sports unaomilikiwa na jamaa wa Qatar umetoa taarifa zikisema vyanzo vya uhakika vinaonesha kwamba kimsingi Mhispania huyo amekubaliana na wamiliki wa Man City wanaotoka Mashariki ya Kati kuwafanyia kazi yao.
Wakati si siri kwamba mabosi wa City, Ferran Soriano na Txiki Begiristain kwa muda sasa wamekuwa wanataka Guardiola awafundishe City, Mhispania huyo bado ana mkatabana Bayern hadi mwaka kesho.
Pengine anaweza kuondoka, ikizingatiwa amekuwa na matokeo mabaya katikati ya wiki baada ya kutandikwa na Barcelona 3-0 kwenye mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Kadhalika Bayern wametolewa kwenye nusu fainali ya Kombe la Ujerumani kwa penati na Borussia Dortmund, ambapo Bayern walikosa penati zao zote. Kwenye Ligi Kuu, baada ya kutwaa ubingwa wamekuwa wakifungwa, ambapo Jumamosi hii walipoteza mchezo wan ne mfululizo.
Pellegrini amekuwa katika wakati mgumu, akichagizwa na wengi kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya City katika baadhi ya mechi, ikiwa ni pamoja na kuutema ubingwa aliowapatia msimu uliopita na kubaki nyuma ya mabingwa wapya – Chelsea – kwa zaidi ya pointi 10.
Hivi karibuni watu walio karibu na Pellegrini walisema kwamba binafsi alikuwa na wasiwasi juu ya hatima yake na wanafamilia wake pia walikuwa wakihisi yupo kwenye siku za mwisho za kuwanoa matajiri hao wa Manchester.
Hata hivyo, Man City katika taarifa yao wamekana, wakidai kwamba hawajatoa ofa ya kazi kwa mtu yeyote tofauti na kocha aliyepo sasa anayeendelea na kazi na kwamba hata msimu ujao atakuwa yeye kwenye ukocha.
Zipo habari pia kwamba Ac Milan wa Italia wanataka kumpa Guardiola kazi kwa ajili ya msimu ujao, wakilenga kujiimarisha na kutisha barani Ulaya.