*Ancelotti kuvaa viatu vyake
Kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola ataondoka klabuni hapo mwisho wamsimu huu.
Guardiola (44) ameweka wazi hatima yake iliyokuwa ikisubiriwa kwa
hamu, na nafasi yake itachukuliwa na Carlo Ancelotti ambaye alikuwa
kocha wa Real Madrid kabla ya kufutwa kazi kiangazi kilichopita.
Ancelotti alikaririwa majuzi akisema kwamba alikuwa akijifunza
Kijerumani, lugha aliyoeleza kwamba ni ngumu na kuzua hisia kwamba
angehamia kwa miamba hao wa Bavaria.
Guardiola amekuwa akihusishwa na kuhamia kwa ajili ya kufundisha ama
Manchester City, Manchester United, Chelsea au Arsenal. Inajulikana
kwamba Guus Hiddink aliyetangazwa kuwa kocha wa Chelsea juzi, atashika
nafasi hiyo kwa muda hadi mwisho wa msimu.
Guardiola alikuwa kocha wa Barcelona kabla ya kuamua kuondoka na
kupumzika kwa mwaka mmoja akijinoa upya na amewapa Bayern ubingwa wa
Ujerumani mara mbili na Kombe la Ligi tangu ajiunge nao kiangazi cha
2013.
Kwa upande mwingine, Ancelotti (56) aliyepata pia kuwafundisha Chelsea
amekuwa nje ya kazi tangu Mei mwaka huu.
“Tunamshukuru Guardiola kwa yote aliyotendea klabu na tunatumaini
tutasherehekea mafanikio zaidi msimu huu,” Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Bayern, Karl-Heinz Rummenigge alinukuliwa na gazeti la Bild la
Ujerumani.
Akimzungumzia kocha mteule atakayeanza kiangazi kijacho, kiongozi huyo
alisema: “Kwa Ancelotti tumepata kocha mwingine aliyefanikiwa sana
anayekuja Bayern na tunasubiri kufanya kazi pamoja.”
Hadi sasa wadau wa soka wanabaki wakiwaza wapi atakwenda Guardiola,
lakini pia wapi atakwenda Jose Mourinhoaliyefukuzwa na Chelsea wiki
iliyopita na wakala wake kunukuliwa akisema hatapumzika kwa sababu
hajachoka na anajiandaa kuendelea na kazi kwenye klabu kubwa Ulaya.
Hali hii pia inamweka katika wasiwasi kocha wa Manchester United,
Louis van Gaal ambaye sasa amepoteza mechi tatu mfululizo na amekiri
kwamba anahofia kibarua chake. Mawazo mengine yanayoibuka ni kwamba
huenda kocha wa Arsenal, Arsene Wenger anakaribia kustaafu au Manuel
Pellegrini wa Man City atafutwa kazi ili mmoja wa makocha hao wawili
achukue mikoba yake.