*Ni baada ya ukame wa miaka 18
*AFC Leopards wakaribia ya pili
Klabu ya Gor Mahia imetwaa ubingwa wa soka nchini Kenya, na kuwatia furaha maelfu ya washabiki wake.
Gor Mahia wametwaa ubingwa huo baada ya kukumbwa na ukame wa kuusubiri wka kipindi cha miaka 18 na pointi walizofikisha sasa haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote katika KPL msimu huu.
Gor Mahia wamepata ubingwa huo baada ya Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka la Kenya kuamua kuwapa Gor Mahia pointi tatu na mabao matatu kutokana na mechi yao dhidi ya Sony Sugar kuvunjika.
Mechi hiyo iliyofanyika Septemba mosi mwaka huu kweney uwanja wa Awendo ilisambaratika baada ya washabiki kuvamia uwanjani dakika ya 84.
Awali iliamuliwa mechi irudiwe, lakini Alhamisi hii kamati iliwapa ushindi Gor Mahia, kwa vile Sony Sugar ndio timu wenyeji na ndio walisababisha mechi kumalizika kabla ya muda wake.
Klabu hiyo wametawazwa rasmi kuwa mabingwa Alhamisi lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Jack Oguda alisema itabidi watasubiri hadi siku ya mwisho ya msimu kukabidhiwa mwali wao.
“Tumeshaanza maandalizi ya kumtoa mwali na tunafanya mkutano na wadhamini wetu wiki ijayo kujadili suala hili, kombe litatolewa siku ya mwisho ya ligi na si kabla ya hapo,” akasema Oguda.
Gor Mahia watacheza mechi yao ya mwisho dhidi ya Ulinzi Stars mjini Nakuru, na ni huko kombe litakabidhiwa wakati washabiki wao wengi wangependa sherehe ziwe Nairobi waliko.
Uamuzi wa kamati umetoa sababu za kuwapa Gor Mahia pointi tatu kuwa ni benchi la ufundi la Sony Sugar, wakiongozwa na kocha na nahodha wao walimzonga na kumshambulia mwamuzi msaidizi kupinga bao la Gor Mahia.
“Tumebaini kwamba tangu benchi la ufundi lilipomvamia mwamuzi msaidizi, mechi haikuchezwa tena na haingeweza kuchezwa tena hata kama timu zote zingetaka hivyo, kutokana na vurugu zilizokwishaanzishwa,” imesema sehemu ya uamuzi wa kamati.
Gor Mahia, kwa uamuzi huo wamefikisha pointi 56 ambazo ni 15 zaidi ya wapinzani wao wa jadi, AFC Leopards na kwa hesabu za kawaida, AFC hawawezi kuwafikia tena Gor Mahia, maarufu kwa jina la k’Ogalo.
AFC Leopards wakishinda mechi zao nne zilizobaki watafikisha pointi 12 hata kama Gor Mahia watashindwa zao zote.
Gor Mahia na AFC ndizo klabu kongwe zilizokuwa na ushindani mkubwa kwa miaka mingi, lakini soka yao iliporomoka na kuzipisha timu nyingine mpya, ila sasa zinarejea kileleni.
Gor mahia wanafundishwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda, Bobby Williamson na kuna wachezaji maarufu kama Waganda Dan Sserunkuma, Israel Emuge na Ivan Anguyo.
Comments
Loading…