*Niger pointi ya kwanza ya kihistoria
Ghana imechupa nafasi ya kwanza ya kundi B kwenye michuano ya 29 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Nyota hao weusi wa Ghana wamewafunga kwa tabu Tai wa Mali, katika mchezo mgumu wa kuviziana.
Yalikuwepo maswali mengi kabla ya mechi za pili kwa kundi hili Alhamisi hii, ikiwa ni iwapo Ghana ingeweza kujiimarisha mgongoni mwa Mali, au ingeaibika.
Kadhalika palikuwapo sintofahamu juu ya mwelekeo Chui wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyokuwa na pointi moja mkononi, huku Swala wa Niger wakiwa wamepoteza mechi ya kwanza kwa Mali.
Mali walihitaji kushinda ili kwanza kubaki juu kwenye kundi, lakini pia kulinda heshima dhidi ya Ghana.
Kongo walitaka kushinda kuweka hai matumaini ya kusonga mbele, wakati Niger walikuwa wakisaka ushindi wa kwanza kwenye mashindano haya.
Walikuwa ni Ghana waliocheka zaidi, kwani walifanikiwa kufikisha pointi nne, wakiwaacha Mali na pointi tatu.
Kongo na Niger walitoka sare, hivyo Wakongomani wakabaki nafasi ya tatu kwa pointi zao mbili na Niger nafasi ya nne kwa kuambulia pointi moja.
Ushindi wa Ghana ulipatikana kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Mubarak Wakaso katika dakika ya 38.
Penati hiyo ilitolewa baada ya Emmanuel Agyemang-Badu kuangushwa na Adama Tamboura kwenye eneo la hatari.
Mali wangeweza kutangulia kufunga au kuibuka washindi baadaye, kwani katika dakika ya tano tu ya mchezo, golikipa wa Ghana, Fatau Dauda alidaka mpira nje ya eneo lake.
Mwamuzi alimpa kadi ya njano, Mali wakidhani angepewa nyekundu. Mali walipewa mpira wa adhabu, lakini nahodha Seydou Keita alipiga nje, akabaki akiijutia nafasi hiyo.
Mchezo ulitawaliwa na kukamiana na kuchezeana rafu, hivyo kumlazimu mwamuzi kutoa kadi nyingi za njano.
Wa kuingia robo fainali na wa kufungasha virago kurudi nyumbani ataamuliwa kwenye mechi za mwisho, ambapo Ghana wanaopewa nafasi kubwa, watacheza na Niger, huku Mali wakipambana na Kongo.
Pamoja na Niger kuwa na pointi moja tu, wana kubwa la kushangilia, kwa sababu, kwa sababu ndiyo mara ya kwanza kupata pointi tangu mashindano haya kuanzishwa.
Yaweza kuonekana ni kitu kidogo kutoka sare na kupata pointi moja, lakini kwa Niger ni hatua kubwa na mwelekeo sahihi wa soka yao.
Katika mchezo wenyewe, Wakongomani walijitahidi kufungua vyumba na kujaribu kufunga, lakini Niger waligangamala na kuhakikisha hawaachii.
Golikipa wa Niger, Kassaly Daouda alikuwa kigingi kikubwa kwa Wakongomani hao, kwani alizuia mashuti ya wachezaji wengi, wakiwamo Dieumerci Mbokani anayechezea Anderlecht.
Ijumaa hii ni kundi C, aZambia wanapepetana na Nigeria wakati Burkina Faso wakichuana na Ethiopia. Kila timu kati ya hizi ina pointi moja, goli moja kwa kutoka sare mchezo mmoja.
Comments
Loading…