Utovu wa nidhamu umeendelea kusumbua timu za mataifa ya Afrika, na sasa Ghana wamewafukuza kambini wachezaji wao wawili muhimu.
Kutokana na utovu wa nidhamu, Kevin-Prince Boateng na Sulley Muntari wamesimamishwa kwa muda usiojulikana kuchezea Black Stars.
Chama cha Soka (FA) cha Ghana kimewaondoa mara moja kwenye hoteli walimokuwa na wenzao nchini Brazil na kuwapatia tiketi za ndege kurudi nyumbani.
Hatua hii inakuja Ghana wakiwa na mechi muhimu na ya mwisho ya makundi dhidi ya Ureno huku Marekani wakicheza na Ujerumani.
Ghana walipewa nafasi ya kuendeleza rekodi ya kuwafunga Wamarekani kwa mara ya tatu lakini wakafungwa, kisha wakaenda sare na Ujerumani.
Boateng (27) anayechezea Schalke 04 ya Ujerumani alitumia lugha ya matusi dhidi ya kocha Kwesi Appiah wakiwa mazoezini Jumanne na wala hakuonesha kujutia kosa lake.
Muntari (29) anayekipiga AC Milan ya Italia, alimpiga mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FA, Moses Armah pasipo hata kuchokozwa.
Tayari Ghana walihusishwa na malalamiko kwenye kikosi chao juu ya malipo waliyotaka kwa kucheza mechi zao mbili na Serikali ya Ghana ilituma pauni milioni 1.8 kwa ndege ya kukodi kuwalipa wachezaji hao.
Kikosi hicho kilitishia kugoma kucheza mechi yao hii ya mwisho dhidi ya Ureno ikiwa hawangelipwa fedha zao.
Ili kufuzu, Ghana wanatakiwa kushinda mechi hii na kuomba apatikane mshini baina ya Marekani na Ujerumani. Bado Ghana watatakiwa wawe na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.
Cameroon walikumbwa na mzozo wa posho na kugomea kuondoka nchini mwao kwenda Brazil dakika za mwisho hadi wakalipwa, wakafika Brazil na kufungwa mechi zote, bado wachezaji wakaonesha utovu wa nidhamu uwanjani.
Alex Song alimpiga ngumi kwa nyuma Mario Mandzukic wa Croatia na kupewa kadi nyekundu wakati Benoit Assou-Ekotto alimpiga kichwa mwenzake, Benjamin Moukandjo uwanjani.
Comments
Loading…