Ghana na Ivory Coast wamefanikiwa kuingua nusu fainali michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCPN) kwa kuwafunga kirahisi Guinea Bissau 3-0.
Kwa Ghana Christian Atsu alilianzisha dakika nne tu za kwanza, baada ya kufunga kutokana na mpira aliofinyiwa kwa nyuma na from Andre Ayew. Guinea waliwazawadia Ghana bao la pili baada ya Baissama Sankoh kushindwa kusafisha mpira na Kwesi Appiah bila ajizi akaukwamisha kimiani.
Alikuwa ni Atsu tena aliyecheka na nyavu na kuwafanya Black Stars hao watoke na ushindi mnono, tofauti na timu nyingine ambazo tangu mwanzo ushindi umepatikana kwa mbinde.
Katika mechi nyingine, Ivory Coast walifanikiwa kuwatoa Algeria waliokuwa wakipewa nafasi ya kufanya vyema kwenye mashindano haya, tena wakatoka kwa kukandamiziwa mabao 3-1.
Mshambuliaji mpya wa Manchester City, Wilfried Bony aliwaonesha kile watakachokuwa wakipata kutoka kwake, kwa kupachika mabao mawili, huku Gervinho akifunga jingine na kuwahakikishia Tembo wa Afrika kusonga mbele.
Hata hivyo, ushindi haukuja kirahisi wala mapema, kwani bao la kwanza la Bony lililopatikana dakika ya 26 lilisawazishwa na Hilal Soudani katika dakika ya 51. Awali mchezaji huyo alikaribia kufunga lakini jitihada zake zikakwama kwa kipa Sylvain Gbohouo.
Algeria walitia shinikizo kwenye lango la Ivory Coast katika dakika za mwisho, lakini hawakuweza kufanikiwa kupata bao hadi kipenga cha mwisho.
Nusu fainali ya kwanza ni baina ya Kongo Kinshasa na Ivory Coast Jumatano hii wakati ya pili ni kati ya Ghana na wenyeji Guinea ya Ikweta waliovuka kiaina. Mshindi wa tatu atatafutwa Jumamosi wakati fainali ni Jumapili.