Pengine hawa ndiyo walikuwa wamefanikiwa kukaa karibu na kona ya mioyo ya mashabiki wengi wa hivi vilabu viwili. Walifanikiwa kujenga makazi ya kudumu kwenye mioyo ya mashabiki.
Haruna Niyonzima alikuwa akipendwa sana na mashabiki wa Yanga, mashabiki wa Yanga walikuwa na mahaba mazito sana juu yake!. Ungemwambia nini baya la Haruna Niyonzima shabiki yeyote akukubalie?.
Ni ngumu sana, huyu alikuwa fundi haswaa, alijua kuupendezesha mpira, miguu yake ilimiliki kila aina ya rangi kwa ajili ya kupendezesha mpira. Alijua ni wapi mahali sahihi pa kupaka rangi ya njano, na sehemu gani ikipakwa rangi ya kijani itapendezesha.
Kwa kifupi alijua jinsi ya kuweka tabasamu kwenye nyuso za mashabiki wengi wa mpira. Huwezi kununa wakati ambao Haruna Niyonzima yuko ndani ya uwanja. Ataufanya mchezo wa mpira wa miguu kuwa sehemu ya burudani tamu zaidi ya burudani zinazopatikana Casino.
Huu ndiyo ulikuwa mwanzo wa yeye kujijengea makazi ya milele kwenye mioyo ya mashabiki wa Yanga. Makazi ambayo mpaka sasa yapo, makazi ambayo hajabomolewa wala kupangishwa kwa mtu yeyote ilihali kwa sasa Haruna Niyonzima yuko Simba.
Sehemu ambayo Yanga ilifanikiwa kumchukua kipenzi cha mashabiki wengi wa Simba, Ibrahim Ajib “Migomba”. Huyu naye hadithi yake haitofautiani na hadithi na Haruna Niyonzima. Ni kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi.
Huyu naye alifanikiwa kujibanza katikati ya mioyo ya mashabiki wa Simba. Na mashabiki wa Simba hawakuwa na hiyana yoyote. Walimpokea na kumpa kumbato katika mioyo yao kwa sababu ya ufundi wa miguu ya Ajib.
Miguu yake ina ufundi wa hali ya juu, ufundi ambao unaweza kusanifu majengo imara na bora duniani. Alikuwa akitoa burudani katika mbuga ya Msimbazi mpaka Simba wakawa wanashuka chini, hasira zao zilikuwa zinapoa, mbele ya Ajib , Simba hakuwa na uwezo wa kuwa Mfalme, Ajib ndiye aliyekuwa Mfalme wa Msimbazi.
Mfalme ambaye aliondoka na kwenda kwa mahasimu wao wakubwa (Yanga). Ambao na wao msimu huo huo waliondokewa na kipenzi chao Haruna Niyonzima.
Kitu hiki kilisaidia sana kila upande kisijihisi na maumivu kwa sababu wote walijifariji kumchukua mtu ambaye alikuwa muhimu kwenye vilabu hivi.
Maisha hayakuwahi kusimama hata sekunde moja, yaliendelea kwenda mbele na hayakutaka kusubiri mtu, kasi yake ilikuwa ile ile, yani kasi ya kutumia masaa 24 kukamilisha safari ya siku moja katika maisha.
Maisha hayakuwahi kubadilisha chochote kile, hata tambo za mashabiki wa pande hizi mbili zilibaki pale pale. Kila mtu alibaki kujivunia alichonacho na kukibeza ambacho hakuwa nacho.
Simba alijivunia kuinasa miguu ya fundi rangi Haruna Niyonzima na Yanga alijivunia kuinasa miguu ya msanifu mkubwa wa majengo imara na bora (Ibrahim Ajib).
Simba waliwabeza Yanga kusajili mchezaji mvivu, Yanga nao wakawabeza Simba kusajili mchezaji mzee ambaye alikuwa anaelekea mwisho wa kipaji chake. Kwa kifupi zilikuwa kebehi ambazo zilikuwa haziondoi uhalisia kuwa pande zote mbili ziliumia kuondokewa na hawa wachezaji wawili!.
Swali moja ambalo lilibaki ni nani ambaye amelamba dume?. Nani ambaye atanufaika na sajili hizi mbili. Msimu wa pili huu, mpaka sasa kila kitu kiko wazi ni nani ambaye amenufaika kwa kiasi kikubwa na sajili hizi mbili.
Wakati msimu huu Yanga wakiwa wanajivunia na kiwango cha Ibrahim Ajib “Migomba”, Simba bado wanajiuliza ni lini watàmuona kiwanjani Haruna Niyonzima.
Hajafanikiwa kucheza mechi nyingi msimu huu, amekuwa na kutoelewana na viongozi wa Simba. Yani mechi nyingi anazicheza nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja. Hii ni tofauti kabisa na kwa Ibrahim Ajib ” Migomba*.
Amehusika kwenye magoli 11 mpaka sasa msimu huu kati ya magoli 14 waliyoyafunga Yanga msimu huu. Ni magoli matatu pekee ambayo miguu yake haijahusika nayo!.
Ni mhimili wa timu?, hapana shaka huwezi kusita kusema NDIYO. huyu ni mhimili wa timu kwa sasa ndani ya klabu ya Yanga. Anaisaidia sana Yanga. Anatengeza nafasi nyingi za magoli, anafunga magoli , mpaka sasa amefanikiwa kufunga magoli matatu.
Kwa kifupi mpaka sasa Yanga wamenufaika zaidi na usajili wa Ibrahim Ajib “Migomba” kuliko ambavyo Simba walivyonufaika na usajili wa Haruna Niyonzima. Hofu yangu ni moja, kuna uwezekano mkubwa kwa Haruna Niyonzima kuondoka Simba bila mashabiki wa Simba kuonja utamu wa miguu yao.
Mpaka sasa hawajamfaidi kabisa, hawajajivunia naye kabisa, wanatamani aoneshe ufundi wake ambao alikuwa anauonesha katika klabu ya Yanga lakini ndivyo hivo muda haumpi nafasi na cha kusikitisha zaidi mkataba wake unaenda kuisha bila kufanya chochote cha maana katika timu ya Simba!.