*Di Matteo apewa tuzo maalumu
Alex Ferguson amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa Mwaka na Chama cha Makocha wa England (LMA), baada ya kuwaongoza Manchester United kutwaa ubingwa wao wa 20.
Fergie (71) anastaafu rasmi baada ya kuwatumikia Man U kwa miaka karibu 27, akakusanya jumla ya vikombe 38 na mwenyewe anasema kwamba anafurahia kufikia mwisho wa kazi nzito zilizoambatana na shughuli na hafla nyingi, akisema zilikuwa za kuchosha.
“Kwa kweli yalikuwa mambo makubwa kwa muda wote huu…ni klabu ya aina yake, lakini natoa pongezi za pekee kwa West Bromwich Albion kwa jinsi walivyogangamala kwenye mechi yetu ya mwisho (sare ya 5-5) na naamini hata Steve Clarke (kocha wa West Brom) anahitaji tuzo,” akasema Fergie.
Makocha na wasaidizi wao katika ligi ya England walikuwa na hafla ya kikazi baada ya kumalizika msimu wa 2012/13, ambapo United walitwaa ubingwa, Manchester City wakashika nafasi ya pili wakifuatiwa na Chelsea na Arsenal waliofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wigan, Reading na QPR walishuka daraja.
Mwenyekiti wa LMA, Howard Wilkinson anasema Fergie alistahili tuzo hiyo na kwamba wanatumia vigezo vya kisayansi zaidi na kwamba hakuna majaji bora kuliko wao katika kubaini kocha yupi alikuwa bora.
“Ni vigumu kupata maneno ya kufaa na kutosha kumwelezea mtu wa aina ya Ferguson na jinsi alivyoujenga mchezo huu wa soka…ameacha rekodi ya aina yake na hatukuwa na shida kabisa ya kumchagua yeye kwa mara ya nne,” alisema Mwenyekiti Wilkinson.
Mrithi wa Fergie, David Moyes aliyekaa Everton kwa miaka 11, ameshinda tuzo hiyo mara tatu, na Jumatatu aliwasili Old Trafford na kukutana na baadhi ya wafanyakazi atakaokuwa nao kuanzia Julai mosi, kabla ya kuondoka kurudi Everton kumaliza kazi na kufanya makabidhiano.
Katika tuzo nyingine za msimu huu, Kocha wa Cardiff. Malky Mackay alikabidhiwa ile ya Championship (ligi ya ngazi ya pili) kwa kuipandisha timu hiyo hadi Ligi Kuu; Gary Johnson akatwaa tuzo ya League One; Martin Allen kwa League Two wakati Roberto Di Matteo aliyewaongoza Chelsea kutwaa ubingwa wa Ulaya na Phil Parkinson wa Bradford walipewa tuzo maalumu. Di Matteo alifukuzwa kazi baada ya kufanya vibaya kwenye mashindano yaliyofuata ya Ulaya.
Kocha wa Timu ya Taifa ya England, Roy Hodgson alichaguliwa kocha bora miongoni mwa wale waliokwishasimamia mechi zaidi ya 1,000, ambapo wamechanganya na mechi za kimataifa,
Hodgson amefundisha timu za nchi nane tofauti, alisema kazi ya ukocha inazidi kuwa ngumu kadiri miaka inavyokwenda, na kwamba mwenye bahati tu ndiye atasalimika na mawimbi yanayowandama makocha kila kukicha.
Comments
Loading…