Uzazi utenganishwe na wajibu wa kazi uliopo kwenye mkataba. Masuala ya taasisi na uzazi lazima vitenganishwe, na hayo yatafanikiwa ikiwa wataalamu wa sharia, habari na utawala watasimama kwenye nafasi zao.
MPIRA wa miguu Tanzania unawahitaji wataalamu wa fani mbalimbali ili kuwawezesha wachezaji kutumikia fani yao kwa ufanisi mbali ya kuwa na vipaji. Wachezaji wanahitaji msaada mkubwa ili kunufaishwa na vipaji vyao. Hivi ndivyo unavyoweza kuhitimisha baada ya kusikiliza mahojiano ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Feisal Salum na kipindi cha Power Breakfast cha Clouds F.M. Nyota huyo ana mgogoro na klabu ya Yanga.
TANZANIASPORTS imefanya uchambuzi na kubaini masuala muhimu ambayo wachezaji wa mpira wa miguu Tanzania wanakabiliana nayo. Lengo la uchambuzi huu ni si kuelezea maudhui ya kile kilichojadiliwa kwa undani bali kupanua dhima yake na kuwafikia wasomaji,viongozi,wachezaji na wataalamu wengine kwa ujumla wake.
Wanasheria wameitwa kwenye mpira
Kama kuna jambo ambalo Feisal Salum amefichua ni hali mbaya ya wachezaji wakati wa kusaini mikataba yao. Jambo hili pia liliwahi kumkuta nyota wa Tanzania, Simon Msuva wakati akichezea klabu ya Wydad Casablanca ambako alipewa mkataba wenye lugha ya Kifaransa ambayo yeye haifahamu hivyo kutogundua vipengele vya kisheria.
Feisal Salum amekiri kuwa huwa anasaini mkataba lakini hajui lugha ya Kiingereza. Kutojua lugha si dhambi lakini kusaini mkataba ambao hujui vipengele vyake ndilo tatizo kubwa linalowakabili wachezaji wetu. Wanasheria wanatakiwa kuwatafuta wachezaji hawa na kuwageuza kuwa fursa ili waweze kunufaika kwa pamoja. Wanasheria wasisubiri kutafutwa na wateja, badala yake imedhihirika wateja wengi wapo eneo la mpira wa miguu.
Hivyo wanasheria wanaweza kuwatafuta wachezaji na kupata undani ikiwa wanao wanasheria na kuwaomba nafasi ya kufanya nao kazi. Wataalamu wa sharia watatoa mchango mkubwa kwa kuwasimamia wachezaji pamoja na kuangalia namna vipengele vya mikataba vinavyosema pamoja na masharti yote muhimu.
Shime wanasheria masuala ya mikataba ya wachezaji ni jambo nyeti na ambalo wenyewe wanatakiwa kufahamu hisia binafsi zisiathiri taratibu za kisheria pale zinapohusiana na taasisi zozote.
Wataalamu wa mawasiliano wasijifiche
Mwanamuziki mmoja nguli nchini Tanzania huwa hafanyi mahojiano pasipo msimamizi wake ambaye ni gwiji wa masuala ya habari na mawasiliano. Mwanamuziki huyo husimamiwa na kuelekezwa masuala muhimu ya kuzungumza mbele ya vyombo vya habari na yapi si ya kuzungumza.
Mtaalamu huyo anamtafutia vyombo vya habari vya kumfanyia mahojiano mteja wake na kanuni na taratibu anazoziongoza. Mashauriano kati ya mwanamuziki huyo na mtaalamu wa habari yamemwezesha kuwa mmoja wanamuziki wanaozungumza vitu vya msingi pekee.
Feisal Salum ameonesha wachezaji wetu wanatakiwa kusaidiwa katika masuala ya habari. Mwanahabari anasimamia mawasiliano ya kimkakati kwa umma, anahakikisha ujumbe wa mchezaji unakwenda pasipo kuvurugwa, anampatia fursa ya mahojiano kwenye vyombo vya habari au aina ya waandishi ambao wanajulikana hawana mambo meusi.
Mtaalamu huyu ndiye mtu anayetakiwa kusaidiana na mwanasheria kuhakikisha maelekezo na mafunzo ya namna ya kuzungumza kwenye vyombo vya habari pasipo kuvunja sharia yanakuwa na ufanisi na ujumbe unafika kwa walengwa. Lazima wachezaji wawe na wasemaji rasmi wa masuala yao, bila kujali vipato wanavyopata au watakavyowalipa bali lazima suala hili lipewe kipaumbele.
Magwiji wa uongozi na utawala wameitwa
Kila mchezaji anahitaji Menejimenti. Inafahamika kuwa si kila mchezaji anaweza kugharamia masuala ya Menejimenti lakini kwa upande mwingine kufanya jambo kulingana na uwezo wao inawezekana.
Siamini kuwa mchezaji hawezi kumtumia mtu mwenye utaalamu wa uongozi akamsaidia masuala kadhaa wa kadhaa ili aweze kujisimamia vizuri katika fani yake. Wataalamu wa uongozi ni muhimu kwa sababu wanawezesha wachezaji kujitambua, kutengeneza mipaka,kuzingatia wajibu wa kazi na masuala mengine yatokanayo.
Wazazi wawekwe mbali na mikataba
Mojawapo ya suala linagonga vichwa vya habari Tanzania ni suala la mama Feisal Salum kuwa msemaji wa masuala kadhaa. Chukulia suala la mchezaji kama Cristiano Ronaldo, huwezi kumwona mama yake anazungumzia masuala ya kimkataba wa mwanaye hadharani.
Ikiwa wanazungumza ni nyuma ya pazia (nyumbani) kushauriana hili au lile, lakini linapofika suala la kwenda hadharani wazazi wawekwe mbali na amsuala ya mikataba ya wachezaji hao. Pengine Ronaldo ni mfano wa mbali, lakini haya masuala ya utawala si rahisi kuwaona wachezaji wa ng’ambo ama hata nchi zilizotupiga bao kimaendeleo ya mpira hapa Afrika huwezi kuona mchanyato huo (haina maana ni lazima kufanana na wengine lakini mipaka ni lazima).
Uzazi utenganishwe na wajibu wa kazi uliopo kwenye mkataba. Masuala ya taasisi na uzazi lazima vitenganishwe, na hayo yatafanikiwa ikiwa wataalamu wa sharia, habari na utawala watasimama kwenye nafasi zao.
Walimu wa lugha wameitwa
Feisal Salum amezungumzia suala la lugha ya Kiingereza. Kutojua lugha hiyo haina maana kuwa kipaji chake kitatoweka bali akiijua hata ya msingi inamwezesha kupata vitu vya msingi wakati wa kusaini mikataba. Walimu wa lugha ya Kiingereza wameitwa hapa.
Kumbukumbu zinaonesha baadhi ya wachezaji wanaotoka mataifa ya Amerika kusini na kwenda EPL hawajui lugha ya Kiingereza, lakini baadhi huchukua masomo hayo. Wapo waliowahi kukataa mfano Carlos Tevez, lakini haibadilishi kuwa lugha ya Kiingereza ni mali ya dunia sio ya Waingereza tena.
Ni lugha ya kibiashara,kisheria,kiuchumi na masuala mengine. Wachezaji mbalimbali katika Ligi kubwa duniani wanahangaika kutafuta walimu wa kuwafundisha angalau mambo ya msingi ya lugha ya Kiingereza. Hivyo Feisal Salum amewaita walimu, amewaomba waje kwenye mpira wa miguu kufanya masomo hayo.
Natambua ni gharama sana, lakini kwenye maendeleo iwe binafsi au taasisi lazima gharama zichukue nafasi yake. Walimu wa lugha waje kwenye mpira kuna fursa, ikiwezekana hata klabu zetu zinasohiriki mashindano ya kimataifa zichukue walimu hao kwa makubaliano na wachezaji ili wakatwe fedha kupitia mishahara yao kwa kulipia masomo ya lugha.
Udhaifu wa mameneja wa wachezaji
Wachezaji wanawahitaji mameneja wao ili kufanikisha mambo mbalimbali. Mchezaji anapokwenda hadharani kukiri hajui masuala ya msingi ya kimkataba, lugha na mengineyo, inaleta swali kuwa meneja wake haoni hayo?
Ni muhimu kufahamu meneja anatakiwa kumshauri mchezaji vipaumbele vya muhimu kuboresha kazi yake. Kwamba ikiwa mchezaji anashiriki mashindano ya kimataifa anatakiwa kutanua uwezo wake kwa kuhakikisha anajifunza masuala muhimu. Sifa isiwe kuitwa meneja tu, bali anaingiza nini katika kazi ya mchezaji wake (mteja wake). Kinyume cha hapo Feisal ameonesha kuwa mameneja ni dhaifu.