BINGWA mtetezi ameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars. Mabao ya Yanga yalipatikana mapema zaidi, kwani iliwachukua dakika 14 tu tangu kuanza kwa mchezo huo kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Clement Mzize, kabla ya mshambuliaji Mzimbabwe Prince Dube kuongeza bao la pili ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza. Mchezo huo ulichezwa kwenye dimba la KMC Complex, Mwenge jijini Dar Es Salaam. Katika mchezo huo kulikuwa na matukio kadhaa kutoka kwa wachezaji wa pande zote mbili pamoja na mabenchi ya ufundi. Mchezo huo ulikuwa gumzo kwa sababu mara nyingi timu hizo zinapokutana kunakuwa na ushindani wa hali ya juu, huku kila upande ukijitahidi kutafuta ushindi. TANZANIASPORTS inakuletea masuala muhimu yaliyoibuka kwenye mchezo huo.
Vincent Adebayor ni mwisho wa zama?
Kati ya wachezaji gumzo katika mchezo huo ni staa Vincent Adebayor. Nyota huyo amekuwa gumzo kwa sababu alikuwa miongoni mwa wachezaji waliowindwa na vigogo vya soka hapa nchini wakati akiwa wa moto. Katika mchezo dhidi ya Yanga Vincent Adebayor ambaye anasifika kwa ufundi wa hali ya juu, matumizi mazuri ya mguu wa kushoto, kasi ya mchezo na maarifa ya kuchungulia lango la adui, lakini alionekana mchezaji wa kawaida mbele ya safu ya ulinzi ya Yanga. Kila alipokuwa akipewa pasi au kushiriki katika maandalizi ya mashambulizi ya Singida Black Star hakuonekana kama yule nyota aliyeimbwa na kuwindwa kwa miaka kadhaa sasa. Adebayor huyu hana kasi, anaonekana kuongezeka uzito na uchezaji wake si ule uliotamanisha vigogo wa soka Afrika. Kama kuna jukumu ambalo benchi za Ufundi la Singida Black Stars ni kuhakikisha wanarudisha makali ya nyota huyu ambaye akikaa sawa anaweza kuitangaza Ligi yetu ya Tanzania.
Hakuna kama Clement Mzize
Washambuliaji wengi wamekuja Yanga na kuondoka. Mshambuliaji pekee ambaye alikuwa anaweza kumkalisha benchi Clement Mzize ni Fiston Mayele. Tangu kuondoka kwa Mayele klabu ya Yanga haikupata mshambuliaji mbadala, na licha ya usajili na wengine Clement Mzize ameendelea kuonesha yeye ni moto wa kutoea mbali. Katika mchezo dhidi ya Singida Black Stars ilimchukua dakika 14 tu kupachika bao la kwanza. Uchezaji wa mshambuliaji huyo pia ni kitu kingine kinachofurahisha, kwani anawez akupangwa kulia au kushoto na nafasi ya mshambuliaji wa kati. Pia ni mshambuliaji ambaye anaweza kucheza katika mfumo wa washambuliaji wawili 4-4-2. Katika mfumo huo Mzize anakuwa kama mshambuliaji huru wa pili ambaye anaweza kutokea upande wowote. Kwa mfumo huo amechezeshwa mara kadhaa na Prince Dube au Kennedy Musonda. Kila anavyocheza anadhihirisha ni kwanini kocha wa Wydad Casblanca Rhulani Mokwena anamhitaji nyota huyo kwenye kikosi chake.
Ukuta wa Djgui Diara kulikoni
Bao walilopata Singida Black Stars ni lazima litaamsha akili, kipaji na maarifa aliyonayo golikipa wa Yanga. Mshambuliaji wa Singida Black Stars, Sowah hakuwa mbali wakati Djigui Diarra alipodaka na kutema mpira uliotoka kwenye wingi ya kulia ya Singida, lakini wakati anathema mpira ili kupoza ukali wa shuti lile, Sowah aliisoma akili ya Diarra na hivyo alikuwa hatua moja tu wakati mpira ukitemwa, naye bila kufanya ajizi akapchika bao la kufutia machozi. Namna bao lenyewe lilivyofungwa ndicho kitu kinacholeta mjadala kulikoni ukuta wa Diarra hadi uruhusu bao la aina hiyo? Ingawaje mchezo wa soka ni wenye makosa lakini namna Singida walivyopata lile bao ni wazi benchi la ufundi linatakiwa kupiga kengele ya kumwmasha Diarra, kuwa mbinu ya kudaka inasomwa na wapinzani na wanaelewa huwa anaruhusu mpira umtoke kwa mita moja na nusu. Matokeo yake anakosa ‘Clean sheet’ katika mechi nyingi kwenye msimu huu.
Kuna magoli mengi ya Prince Dube
Mzimbabwe huyu alifunga bao la pili kwa Yanga. Yapo matukio akdhaa ambayo yanasababisha mashabiki wamlalamikie au wapinzani kumbeza, lakini ukweli wa mambo Dube ni mshambuliaji mzuri tu, na kama unataka kumwondoa inabidi uangalie mbadala wake analeta nini. Katika mchezo wao na Singida, wapinzani wao walikuwa Sowah, anaonekana kuwa na nguvu na mwenye mipambano mizuri na mabeki, lakini fikiria namna nyingine, hana kasi kubwa kiuchezaji kumzidi Dube. Takwimu zinaonesha Prince Dube ameshiriki katika mabao 16, pamoja na kufunga mabao 9 hadi sasa.
Kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu jina lake lipo. Ni mshambuliaji wa kigeni. Unapokuwa na mshambuliaji mwenye uhakika wa kukupa mabao si chini ya 10 kisha akawa anatengeneza mabao 16 ni dhahiri anazo nafasi 26 zenye faida kwa timu. Msimamo w aLigi Kuu kwa wafungaji Prince Dube anachuana na wenzake ndani ya Yanga na wapinzani wao. Haonekani kuwa mshambuliaji ambaye anatetereka kwani asipofunga anatengeneza na kisha anafunga mwenyewe. Dube anayo magoli mengi miguuni mwake ikiwa atatulizwa na kuimarishwa kifundi kwenye upachikaji wa mabao. Uzoefu wa Ligi anao tayari.
Comments
Loading…