Kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza anazidi kung’arisha nyota yake Ligi Kuu Tanzania Bara. Nyota huyo kutoka nchini Burundi amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga tangu alipoanza kusakata kabumbu kwenye klabu yao kwenye mchezo wa kirafiki kati ya mabingwa hao wa zamani na Singida United ya mkoani Singida. Makala haya yanaeleza mambo muhimu kuhusu nyota huyo.
1. Bao la Stars lampa ujiko
Kama kuna siku ambayo itakumbukwa na mashabiki wa Tanzania ni pale waliposhuhudia timu yao ya taifa ya Taifa Stars ikinyukwa bao 1-0 na Burundi katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam. Katika mchezo huo Saido Ntibazonkiza alipachika bao pekee la Burundi kwa njia ya adhabu ndogo, maarufu. Ni bao hilo ndilo lililompa ulaji wa kusajiliwa na Yanga akiwa mchezaji huru.
2. Umri mkubwa, kasi ya kijana
Nyota huyo raia wa Burundi ana miaka 33 kwa sasa, lakini ana uwezo mkubwa wa kucheza kwa kasi kama kijana wa miaka 25. Kasi, upigaji wa chenga na namna anavyomudu kukaa na mpira ni vionjo ambavyo vimewavutia mashabiki wengi wa soka. baadhi ya wachambuzi wanaamini Yanga walipaswa kumpata nyota huyo mapema kuliko sasa ambako uwezo wake unaelekea ukingoni. Hata hivyo wanatolea mfano Zlatan Ibrahimovic kuendelea kucheza mpira akiwa na umri mkubwa, ama alivyo Cristiano Ronaldo mwenye umri wa miaka 36 kwa sasa akiwa haonekani kuacha soka siku za karibuni.
3. Bao mbili siku ya kwanza.
Katika mchezo wake wa kwanza kuichezea Yanga ulikuwa dhidi ya Singida United ya mkoani Singida. Yanga walicheza mchezo kama sehemu ya kuimarisha kikosi chao. Saido Ntibazonkiza alifunga mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya Singida United. Katika mchezo huo Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-0. Kiwango cha Saido kiliwakosha wengi na kutajwa kuwa silaha nyingine ya kutaka kutwaa ubingwa msimu huu. Ndoto za nyota huyo zipo wazi kuwa anatamani kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Yanga.
4. Kujinadi YoTube.
Saido ni mchezaji wa kipekee ambaye amewekeza kutangaza kazi zake za uwanjani kupitia mtandao wa YouTube. Katika video hizo kuna matukio mbalimbali anapokuwa dimbhani na namna anavyoonesha ubora kwenye mchezo wenyewe. Jambo hili limekuwa adimu kwa wachezaji wengi wa kitanzania. Hiyo ni mbinu mojawapo ya kujitangaza kama mwanasoka. Kupitia ukurasa wake wa Facebook anawaomba wafuasi wake kutembelea chaneli ambayo anaweka video hizo ili wajionee ufundi wake.
5. Kipaji na maamuzi ya haraka.
Ukizungumza na mashabiki wa soka nchini huwa wanatamka maneno mawili mawili muhimu kumwelezea Saido Ntibazonkiza; ‘Kipaji’ na ‘maamuzi’ ya haraka. Anatajwa kuwa mchezaji mwenye kipaji na maamuzi ya haraka, anajua wapi aupige mpira ili kutoa pasi za mabao au kufunga mabao kwa njia ya mipira ya adhabu ndogo. Hana uchoyo wa kutoa pasi. Yanga walikuwa wanakosa mchezaji wa kupigapasi za mwisho za uhakika na kusaidia washambuliaji kupachika mabao. Kwa mashabiki wa kandanda wanaona nyota huyo ameleta elimu mujarabu kwa wanasoka wazawa.
6. Upara kama mastaa wa Ulaya
Saido Ntibazonkiza ni kundi la wachezaji maarufu duniani ambao wana upara na ambao wamewahi kutamba katika vilabu vyoa na mataifa mbalimbali duniani. Nyota huyo ni miongoni mwa wachezaji wenye upara, ambaye anafananishwa hali hiyo na mastaa wengine wenye upara kama vile Arjen Robben,Andres Iniesta,Zinedine Zidane,Estaban Cambiasso,Jaap Stam,Fabien Barthez,Pablo Zabaleta,Lee Carsley, Sir Bobby Charlton,
7. Mkali wa ‘Free kick’
Nyota huyu anasifika kwa uwezo wa juu wa kupiga mipira ya adhabu ndogo, ambayo kwa kimombo imezoeleka na mashabiki kama’ free kick’. Saido alipachika bao la kwanza la Ligi Kuu Tanzania bara kwenye mchezo wa Yanga dhidi ya Dodoma Jiji uliofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Baada ya mpira kutinga wavuni katika pambano hilo wengi walirudisha kumbukumbu zao katika mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Burundi ambako nyota huyo alitumbukiza mpirani wavuni kwa free kick. Kwahiyo Yanga wamekuwa hatari kwenye eneo la mipira ta faulo karibu na lango la adui kwa sababu wana uhakika wa kufunga kutokana na kikosi chao kuwa na mchezaji mwenye uwezo huo.
8. Rollingstone na Ulaya
Wanahistoria ya soka wanatueleza kuwa Saido Ntibazonkiza si mgeni katika ardhi ya Tanzania. Wanasema nyota huyo amewahi kushiriki mashindano ya mpira wa miguu ya Roollingstone yanayofanyika jijini Arusha miaka kadhaa iliyopita. Kwa mantiki hiyo Saido anaijua Tanzania, anafahamu hamasa za soka zilivyo nchini. Katika soka la kulipwa amewahi kucheza soka katika nchi za Uholanzi, Ufaransa, Poland na Uturuki.