Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta ni miongoni mwa mastaa wa Kiafrika watakaokosa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022. Tanzania ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi J ikiwa imejikusanyia pointi 8 nyuma ya Benin na DRC.
Kinara wa kundi hilo alikuwa DRC wenye pointi 11 akifuatiwa na Benin wenye pointi 10. Wapo nyota kadhaa kutoka bara la Afrika, Asia,Ulaya na Amerika ambao huenda wakakosa fainali hizo za kusisimua ambazo hufanyika kila baada ya miaka minne.
Nazo Italia na Ureno zinahaha kutafuta nafasi ya kucheza fainali hizo mwakani. Makala haya yameandikwa kabla ya kujua hatima ya Ureno na Italia ikiwa zitashiriki fainali hizo au la.
Hivyo kama Italia itashindwa kufuzu ina maana itakuwa mara ya kwanza bingwa wa Euro kukosa fainali za Kombe la Dunia. Hata hivyo kuna habari nyingi kuelekea fainali hizo ambazo zinatajwa kuwa za kipekee.
TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu kuelekea fainali hizo za kukata na shoka ambazo zinatajwa kuwa za gharama kubwa za maandalizi kuliko fainali nyinginezo. Yafuatayo ni mambo muhimu unayopaswa kujua katika fainali hizo.
Mosi, hizi zitakuwa Fainali za kwanza za Kombe la Dunia kufanyika katika nchi ya Kiarabu. Fainali hizo tangu zimeanzishwa hazijawahi kufanyika katika nchi ya Kiarabu, kwahiyo mwenyeji wake Qatar ndiye wa kwanza katika ukanda huo kama ilivyokuwa kwa bara la Afrika ambapo Afrika kusini ilikuwa ya kwanza kuandaa fainali za Kombe la Dunia.
Pili,kwa kawaida Fainali za Kombe la Dunia huwa zinafanyika katika miezi ya Juni na Julai. Katika fainali za mwaka 2002 nchini Japan na Korea kusini baadhi ya mechi zilichezwa asubuhi kwa saa za Tanzania.
Watanzania walikuwa wakiamka na baada ya chai wakajikuta wanatakiwa kutaza mechi za Fainali za Kombe la Dunia kutokana na tofauti ya muda. Kwa kuzingatia hilo la muda, sasa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 zitachezwa mwezi Desemba ili kuepuka hali ya hewa ya joto kali katika miezi ya Juni na Julai nchini Qatar. Itakuwa mara ya kwanza kwa fainali za Kombe la Dunia kuchezwa mwezi Desemba.
Tatu, wenyeji Qatar wamepanga kujenga vituo viwili vya umeme wa sola kama sehemu ya kuongeza nguvu za umeme mwingine katika vituo mbalimbali nchini humo.
Nne, sheria za Qatar zinapiga marafuku watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja hivyo uwezekano wa wao kuhudhuria fainali hizo ni mdogo mno. Lakini mamlaka za
serikali ya nchi hiyo zimesema hakuna mashabiki watakaozuiwa kuingia nchini humo kushuhudia fainali hizo.
Nne, uuzaji wa pombe utakuwa katika maeneo maalumu wakati wote wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022. Hivyo hazitapatikana kila mtaa.
Tano, hizi Fainali za pili za Kombe la Dunia kufanyika katika bara la Asia. Mwaka 2002 fainali hizo ziliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Japan na Korea kusini ikiwa ni mara ya kwanza.
Sita, kabla ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022, nchi mwenyeji Qatar imeandaa mashindano maalumu kwa mataifa ya Kiarabu ambayo yanatarajiwa kufanyika jumanne ya Novemba 30 mwaka huu. Mashindano hayo yanaitwa FIFA Arab Cup Qatar 2021, ambapo jumla ya mataifa 16 ya Kiarabu yatashiriki na kuchezwa katika uwnaja wa Rasu Abu Aboud 974.
Saba, staa wa zamani wa Cameroon na Barcelona, Samuel Eto’o na Cafu wa Brazil ni mabalozi wa Qatar katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022. Nyota hao wametabiri kuwa mwenyeji wa fainali hizo atafika nusu fainali.
Nane, Qatar inakuwa nchi ya kwanza kutoka mashariki ya Kati kuandaa fainali za Kombe la Dunia. Pia ni fainali za kwanza kuandaliwa na nchi ya kiarabu na yenye utamaduni wa kiiaslamu.
Tisa, fainali hizo zitachezwa katika viwanja vya Al Thumama,Lusail,Al Janoub,Qatar Foundation Stadium,Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa,Al Bayt,Ahmad Bin Ali na Ras Abu Aboud. Jumla ya viwanja nane vitatumika katika fainali hizo.
Kumi, licha ya ksuhutumiwa kuvunja haki za binadamu, Shirikisho la Soka Duniani FIFA lilikataa kuyumbishwa na kelele za wanaharakati kwa kusimama kidete kuwa Qatar ndiyo nchi mwenyeji wa fainali za mwaka 2022.
Comments
Loading…