in

Fahamu mambo matano kuhusu bondia Ibrahim Class

Ibrahim Class

Mwishoni mwa mwezi uliopita bondia wa Tanzania Ibrahim Class alipanda  ulingoni kupambana na mpinzani wake Simon Ngoma raia wa Zambia katika uzani  wa Junior Lightweight wa GBC.  

Kwenye mchezo huo Ibrahim Class alitwaa ubingwa wa Dunia wa GBC kwa  ushindi wa majaji wote watatu. Jaji wa kwanza alimpa pointi 95 dhidi ya 91 za  Mzambia. Jaji wa pili alimpa Class pointi 98 dhidi ya 88 za Mzambia.  

Jaji wa tatu alimpa Classa pointi 98 dhidi ya 88 za Mzambia katika pambano kali  lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es salaam. Licha ya  ushindi huo kuna mambo matano muhimu ambayo bondia huyo,makocha na  wadau wa mchezo huo wanatakiwa kuyafahamu. 

1. Kocha mpya kuboresha ufundi. 

Ibrahim Class anahitaji maarifa mapya kutoka kwa mwalimu mpya. Mtindo wake  wa upiganaji ni mzuri, lakini amekuwa na kasoro mbalimbali katika upiganaji.  Inawezekana bondia wa Zambia akalaumiwa kwa mtindo wake wa upiganaji wa  ngumi za holela na kupiga popote kiasi cha mwamuzi Pendo Njau kumuonya mara  kadhaa, lakini Class anahitaji walimu ambao watakuza kipaji chake na kuongeza  maarifa. Kifundi Ibrahim Class anategemea zaidi kipaji, hivyo kujikuta akishindwa  kumdhibiti mpinzani anayeshambulia muda wote kwa kasi na ngumi za kila  upande. Kocha mpya atamwezesha kuimarisha upungufu unaojitokeza kwenye  mapambano mengine. 

2. Stamina 

Class alianza pambano hilo kwa kasi na kumdhibiti mpinzani wake katika raundi  ya kwanza, ambapo alifanikiwa kumkalisha chini Mzambia huyo. Hata hivyo  uhodari na uwezo wa bondia huyo ulichangia pambano kuendelea hivyo kumpa  wakati mgumu Class.  

Katika raundi ya tatu bondia Ibrahim Class aliangushwa chini kutokana na ngumi  kali za mpinzani wake. Hata hivyo suala la kuanguka chini mara kwa mara  lilikuwa jambo la kawaida kwa mabondia wote. Class alikuwa anakosa balansi au 

uwiano katika kupambana na kulinda stamina yake kwenye mchezo. Kukwepa  konde na mpinzani kisha kupepesuka na kuanguka chini ni kukosa balansi.  

Hivyo anatakiwa kuimarisha kiwango chake cha stamina. Jinsi anavyoangushwa  angushwa kirahisi ni hatari kwake. Kuwa bondia wa kimataifa kitendo cha  kuangushwa angushwa kina madhara kisaikolojia. Sio wote wanaweza kurudi  mchezoni kama alivyofanya Antony Joshua dhidi ya Vladimir Klitscho pale  Wembley. 

Lennox Lewis alipigwa ngumi ya taya pale Afrika kusini na Hashim Rahman  akapoteza balansi na kuanguka, hakuyrudi tna mchezoni. Kwahiyo Ibrahim Class  anatakiwa kujua mabondia wa kimataifa wanatakiwa kuondokana na mianya kama  kukosa stamina ili kuwa na ubora. 

3. ‘Focus’ yake iko chini.  

Mfano mpinzani wake alikuwa anatafuta nafasi ya kumpiga makonde ya ‘Upper  cut’ yaani kutokea chini ya kidevu, ili kumaliza mchezo. Kwa upande wake  Ibrahim Class hakuwa na makonde yale yanayolenga sehemu moja, yaani yenye  ‘focus’ mahali fulani penye udhaifu wa mpinzani wake.  

Kwa mfano anapokuwa amemuumiza bondia iwe juu ya jicho,jichoni au akiwa  amempasua sehemu inabidi awe anapalenga zaidi hapo kuongeza maumivu na  kichapo. Tunaweza kumsifia Ibrahim Class kwa uwezo wake mzuri wa kukwepa  makonde, na mojawapo ni yale ya ‘Upper cut’ kwani yangetua barabara mambo  yangekwua mabaya zaidi kwake.  

Hiyo ni ishara kuwa bondia anatakiwa kuwa na ‘focus’ya eneo au mbinu fulani ili  kummaliza mpinzani wake. Hata kwenye ,mpira wa miguu iko hivyo, ukiona  udhaifu kwa mabeki wa pembeni basi unatakiwa kutumia mianya hiyo kupitia  maeneo hayo na kuwachapa mabao wapinzani. 

4. ‘Timing’ ni nzuri 

Hili ni eneo analostahili sifa bondia wetu Ibrahim Class kwa sababu ana makonde  mazuri, anaweza kukwepa na kumzunguka mpinzani. Ngumi za ana kwa ana nazo  anatakiwa kuzimudu na aongezewe ufundi. Ingawaje wengi wanaziita ngumi za 

kuvizia, lakini ukweli Ibrahim Class alikuwa anapiga ngumi za kiufundi zaidi,  badala ya kuhangaika kupigana kama ngumi za mitaani alizofanya mpinzani wake.  

Kupiga ngumi kimahesabu ndiko anakotakiwa kuboresha zaidi. alifanya ‘timing’  nzuri kwa kumchapa makonde katikati ya uso wa mpinzani na kichwani. Zilikuwa  ngumi nzuri na hili eneo anaweza kuongezewe maarifa kwa vile ameonesha uwezo  mzuri.  

5. Kapeti la Ulingoni 

Miongoni mwa sababu zinazolalamikiwa ni ubaya wa ulingo waliotumia mabondia  hao. Ulingo huo ulikuwa kikwazo kwa Ibrahim Class katka ruandi za 8,9, na 10  ambako angeweza kushinda kwa KO kama siyo kapeti la ulingoni kuteleza.  Mabondi wote wawili walipatwa nah ii shida ambao waandaaji wanatakiwa kubeba  mzigo wa lawama kuweka kapeti linaoharibu mchezo. 

Mwisho aapenda jitihada za bondia Ibrahim Class lakini lazima pafanyike kitu. Pengine ni kwa sababu ya pambano kuhwa la kwanza kwake kimataifa, hivyo  anaweza kutafuta uzoefu kutokana na mchezo huo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Diego Maradona

Diego Armando Maradona:

Neymar

KOMBE LA DUNIA 2022