NILISUBIRI mechi za Kimataifa kuona umahiri wa Kocha wa Simba, Fadlu Davids. Kwenye mechi za maandalizi ya msimu zilikuwa za kawaida kwani timu ilikuwa inasukwa upya. Kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, ndipo ushindani wa wachezaji na kimbinu ndipo unapoweza kuona mkakati na mipango ya kocha wa timu. Kila kocha anayo mbinu na aina ya wachezaji anaohitaji katika kikosi chake.
Fadlu Davids amekabidhiwa Simba iliyokuwa na mahitaji makubwa ya kujijenga upya baada ya misimu ya mafanikio na baadaye kupatwa na ugonjwa ule wa timu mbalimbali dunia. Ni ule ugonjwa wa kulinda mafanikio ambao mara nyingi timu zinashindwa kwa sababu ya kushuka kiwango kama timu, kocha kuishiwa makali, kuondokewa na baadhi ya wachezaji muhimu na mbinu za kocha kugundulika hivyo kuzidiwa na wapinzani.
Bila shaka Simba wana hasira ya kupoteza ubingwa misimu minne mfululizo toka kwa watani wao wa jadi Yanga. Kwa msimu huu Simba wamekingia na sura nyingi mpya. Sura za wachezaji ambao wameingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja bila kusubiri mchakato wa kuelewa falsafa na mbinu. Simba imeanza na wachezaji wengi wapya, kocha mpya na pia imeondokewa na mchezaji wake muhimu sana Cletous Chota Chama.
Hata hivyo usajili uliofanywa na uongozi wa Simba umeonesha dalili nzuri za kuleta ushindani mbele ya Yanga kwenye Ligi Kuu. Sidhani Simba hii inaweza kukubali kipigo cha mabao 4-1 toka kwa Yanga tena. Ndiyo maana mchezo wa mwisho Yanga waliambulia ushindi1-0, na kudhihirisha Simba ikijipata vizuri inaweza kushindana vikali na Yanga.
Simba wamecheza mechi mbili za Kimataifa za ushindani katika hatua za awlai za kuwania kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho dhidi ya miamba ya Libya, Al Ahli Tripoli. Katika michezo miwili kocha Fadlu David alikuwa na mikakiati tofauti, ugenini na nyumbani. Ukitazama Simba inayocheza Ligi Kuu hadi sasa utaona wapo katika hatua ya kusafisha nyota zao kwa kuhakikisha wautafuta ushindi kwa nguvu zote.
Matokeo ya ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli kwenye dimba la Benjamin Mkapa ulionesha jinsi Simba wanavyoweza kuingia tofauti katiika mechi na kuibuka na ushindi ama kutafuta matokeo yenye maslahi kwao. Katika mchezo wa kwanza kule Libya, Simba waliingia na mkakati ambao unakwenda kumpa sifa kocha wao Fadlu David.
Simba hawakutaka kubaki nyuma, walikuwa wakicheza kwa kasi kwa kutumia maeneo matatu makuu; winga wa kulia, winga wa kushoto na katikati ya dimba. Bahati nzuri waliyonayo Simba kwa sasa ni kumsajili mshambuliaji Leonel Ateba toka Cameroon.
Mshambuliaji huyu amewahi ahueni Simba. Kwa kawaida kama timu haifungi mabao, inajiweka katika shinikizo la kufungwa. Presha kubwa wanayopata timu pale inakosa mabao au mfungaji huwa ni chungu na inaleta matokeo mabaya. ‘kosa kosa’ bila kutikisa wavu ni janga linalorudisha nyuma tim,u nyingi.
Hata kama timu itakuwa na mbinu za kipekee kuwashinda wapinzani wake lakini ukweli unabaki kwamba mshambuliaji mwenye ujuzi na umahiri wa kupachika mabao ni muhimu sana. kwenye michezo miwili ya Kimataifa, kuanzia kule Libya, Simba walikuwa na mchezo wa aina tatu; walicheza kama Waholanzi na mbinu zao za ‘Total football’.
Kisha wakageukia mbinu za Jose Mourinho za ‘kupaki basi’ (kujilinda au kujihami zaidi kila unapoona adui analiandamana lango) na walipunguza ukubwa wa kiwanja kwa kujazana katikati ya dimba, lakini wangeweza kushambulia kwa kasi sana. Jinsi timu ilivyoupiga mwingi kule Libya lilikuwa suala la muda tu kwenye mchezo wa marudiano kwamba Simba wangeshinda.
Leonel Ateba ameiwezesha safu ya ushambuliaji kupambana na mabeki kwa nguvu,kasi na maarifa. Ateba ameweka mpira mguuni, anapambana kwa nguvu za mwili na kasi yake huwachosha. Fadlu David amempa uhuru Ateba kunyukana na mabeki kadiri anavyoweza.
Eneo analozunguka ni kubwa na anasaidiwa na wachezaji wengine wenye kasi kama yeye, Ahoua,Kibu Denis na Edwin Balua. Umahiri wa kocha Fadlu David ulikuja pale alipofanya uamuzi sahihi wa kumweka benchi Edwin Balua katika mchezo wa marudiano na Ahli Tripoli, na kumwanzisha Kibu Denis. Kipindi cha pili alimwingiza Edwin Balua, ikiwa na maana wapinzani wao waliingiziwa wachezaji wenye kasi zaidi muda wote wa mchezo.
Katika mchezo wa marudiano ndipo Ateba na Balua walifumania nyavu. Kwa maana hiyo Fadlu David anatumia mfumo wa mshambuliaji wa kati mmoja na mawinga wawili katika mchezo mmoja au mawinga wawili wanapishana katika mchezo mwingine kulingana na wapinzani. Kwahiyo ule uamuzi wa kukipanga kikosi kwa mifumo tofauti tofauti katika mechi moja ndicho kitu ambacho kinaipa uimara Simba kwneye mechi za Kimataifa.
Fadlu David pia ameonesha anaweza kujifunza. Katika mecho wa kwanza pale Tripoli alimpanga Edwin Balua kikosi cha kwanza badala wa Kibu Denis. Katika mecho wa marudiano akamwanzisha Kibu Denis na kumweka kando Balua. Ni dhahiri kocha huyu anatumia mifumo miwili hadi mitatu katika mechi moja. Matokeo ya uamuzi wake kwenye dimba la Mkapa, aliibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku Ateba na Balua wakitupia wavuni.
Simba ni timu kubwa kimataifa, inavutia wengi na inaonekana kuwa sehemu sahihi kwa makocha au wachezaji kutangaza vipaji vyao. Lakini Fadlu David amelinda ‘brand’ ya Simba na kukuza wasifu wake kutoka kocha msaidizi hadi kocha mkuu ni hatua kubwa. Kwa Simba ya sasa jinsi inavyobadilika itakuwa ni uchoyo kutomsifia Fadlu David.
Timu kufungwa mechi moja au kutoka sare haina maana ni mbaya. Fadlu David amepokea timu ambayo ni mpya kwa asilimia 51, na anakijenga kikosi chake kwa hisia kali maana jinsi anavyoshangilia mabao ya wachezaji wake inaashiria ‘passion’ aliyonayo kubwa sana na ndicho kitu kinachowavutia wachezaji wa sasa. Kuanzia hapo unaweza kuona nini anachoweza kukifanya mbele ya timu walizopangwa nazo kwenye kundi moja; CS Sfaxien, CS Constantine na FC Bravos Do Maquib kwenye Kombe la Shirikisho.
Comments
Loading…