*Hawajapoteza mechi, wawashusha Chelsea
Klabu ya Everton imeendelea kushikilia rekodi ya kutopoteza mchezo tangu kuanza msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Everton usiku wa Jumatatu wamewafunga Newcastle mabao 3-2 na kupanda hadi nafasi ya nne ya msimamo wa ligi.
Wakicheza nyumbani, Everton walishawafunga Newcastle 3-0 hadi mapumziko na washabiki walidhani wangeshikilia pia rekodi ya kutofungwa bao lolote katika uwanja wa nyumbani msimu huu.
Baadhi ya wadau wa soka walikuwa wakiwatazama Everton kama timu nyonge, hasa baada ya kuondokewa na kocha wake wa miaka 11, David Moyes aliyejiunga Manchester United na kumchukua Roberto Martinez kutoka Wigan walioshuka daraja.
Lakini hali imekuwa tofauti, kwa Mhispania huyo kuwaongoza katika ushindi na sare pasipo kukubali kipigo, ambapo mwishoni mwa wiki watakabiliana na Manchester City katika mchezo unaotarajiwa kuwa mkali.
Beki wa kushoto wa kimataifa wa Ubelgiji, Kevin Mirallas alifanikiwa kupanda kwa kasi na kumwacha beki wa Newcastle, Davide Santon akishangaa kabla ya kumpatia pande Romelu Lukaku (20) aliyetikisa nyavu mbele ya kipa Tim Krul katika dakika ya tano tu.
Kiungo Mwingereza, Ross Barkley (19) alifunga bao la pili dakika ya 25 ambapo kwa muda mwingi wa mchezo alikuwa akiwaadhiri wachezaji wa Newcastle, Moussa Sissoko na Cheick Tiote na kocha Alan Pardew akibaki kushika tama.
Lukaku aliye kwa mkopo kutoka Chelsea alifunga bao la tatu katika dakika ya 37.
Kipindi cha pili kilianza kwa Newcastle kujipanga vyema zaidi kujaribu kurudisha mabao na walifanikiwa dakika sita tu tangu kuanza nusu hiyo ya pili, pale Yohan Cabaye alipovunja mwiko wa Everton kufungwa nyumbani.
Everton walijitahidi kuwazuia wapinzani wao hao, lakini Loic Remy aliyejiunga kutoka Queen Park Rangers walioshuka daraja, aliwaweka Everton shakani alipopachika bao la pili dakika ya 89.
Msimamo wa ligi unaonyesha kwamba nafasi ya kwanza inashikwa na Arsenal wenye pointi 15 wakifuatiwa na Liverpool na Tottenham Hotspur wanaofungana kwa pointi 13.
Wakati Everton wakipanda hadi nafasi ya nne, Chelsea wanashuka hadi ya tano wakifuatiwa na Southampton, Manchester City, Hull, Aston Villa, West Bromwich Albion, Cardiff,
Manchester United, Swansea, Norwich, Stoke, Newcastle, West Ham, Fulham, Crystal Palace na Sunderland mkiani.
Comments
Loading…