Na: Israel Saria
—————–
Euro 2012 imeacha gumzo kubwa baada ya kumalizika kwa mfululizo wa mechi zilizopokewa tofauti na washabiki kuendana na timu zilivyokuwa.
Wapo waliotarajiwa timu zao kufanya vizuri lakini ziliishia kwenye ngazi ya makundi, wakati kuna wasiotarajiwa waliokwenda mbali na kushangaza wengi.
Hatimaye, hitimisho limekuwa historia, Hispania wakikata ngebe za wapinzani wao kwamba walikuwa wamefika njiapanda ya soka na kuchoka.
Kwa wastani, washabiki waliotoa maoni katika ngazi za makundi hawakuwa wamevutiwa na aina ya soka ya Hispania, kwani walitarajia burudani kubwa, lakini na mabao mengi.
Sivyo ilivyokuwa katika fikara ya Kocha Mkuu wa Hispania, Vincente Del Bosque, aliyesema alikuwa akifundisha soka ili kujenga timu na wachezaji waelewe na kamwe si kwa ajili tu ya kushinda.
Akakiri kwamba pamoja na uchezaji wao, bahati ilichangia wao kufika nusu na hata fainali, lakini baadaye akasema kizazi cha sasa cha soka cha Hispania si cha kawaida.
Hiyo ilikuwa baada ya Hispania au La Roja (Wekundu) kama wanavyojiita kuwakung’uta Italia – Azzuri kwa mabao manne bila majibu kwenye fainali.
Ushindi huo ni mkubwa kihistoria, kwa sababu haijapata kurekodiwa kwenye fainali yoyote ya ama Kombe la Dunia wala Kombe la Ulaya. 4-0 ni mabao mengi.
Mchezaji wa Hispania, Andreas Iniesta alitajwa kuwa mchezaji bora wa Euro 2012 na kuiongezea sifa timu yake hiyo.
Baada ya kila timu kuanza mashindano zikitanguliza mbwembwe na kushangiliwa, zikiamini kusonga mbele, ni timu nane tu ziliingia robo fainali.
Zilizofanikiwa kuvuka ni mabingwa Hispania, Italia, Ujerumani na Ureno zilizoingia nusu fainali. Nyingine nne zilizoishia robo fainali ni England na jirani zao Ufaransa; Jamhuri ya Czech na Ugiriki, mbili za mwisho zikiwashangaza wengi kwa kuvuka na kuiacha gizani Urusi.
Watu hupenda soka ya kuvutia, ya kutanua uwanja, pasi na mashambulizi makali, na si ile anayosema ‘The Special One’ Jose Mourinho ya kuweka basi kwenye lango kwa minajili ya kujihami.
Zipo timu zinazotumia mbinu hiyo kama njia ya kuvuka kwenye mtihani, hasa zinapokabiliwa na timu ngumu; England ilitumia mfumo huo dhidi ya Italia, washambuliaji wake wakatokea kuwa ‘mabeki’ wazuri.
Kwa kuwa mpira ni magoli, na hakuna kosa ‘kuweka basi golini’, Chelsea walifanya hivyo kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya hadi wakafanikiwa kulitwaa taji, wakiwaduwaza Barcelona London na Madrid, kisha Bayern Munich nyumbani kwao Ujerumani.
Kocha Vincente Del Bosque anasema mtindo huo wa mchezo wa soka haukuwa na nafasi kwenye mashindano haya, akisema wanachotakiwa kuwa nacho wachezaji ni mbinu za kutembeza mpira, si kuzuia usichezwe.
Ukweli ni kwamba timu zote zilizotolewa kwenye hatua ya robo fainali zilitumia, kwa kiasi fulani, mtindo huo wa kujihami kupita kiasi, badala ya kuimarisha kiungo na kutafuta mabao.
Pamoja na kujaribu mbinu hiyo, kimbunga hakikuziacha , ziliondoka, hata kama ni kwa mikwaju ya penati baada ya muda wa kawaida na ule wa ziada.
Mungu bariki ni kwamba hakuna timu iliyokuja kushinda kwenye mikwaju ya penati ambayo haikuwa imeoyesha kiwango uwanjani.
Hata washabiki wa England walikubalia kwamba bora Italia ilipita, kwa sababu iliwazidi kila idara, ikatawala mchezo lakini wakakosa kilichotakiwa kwa wingi hadi kwenye penati.
England, hata hivyo, katika dakika chache za mwanzo, karibu 10 hivi, walionyesha kuwa tishio kiasi kabla ya kupoa na kuanza kujihami kwa karibu dakika 110 za mchezo.
Jamhuri ya Czech nayo ilijitutumua mbele ya Ureno iliyokuwa na akina Cristiano Ronaldo na Nani, hivyo kwamba kwa dakika 90 za mchezo haikulenga hata shuti moja golini mwa Ureno. Waliishia kufungwa bao 1-0
Ugiriki kwa upande mwingine, waliamua kulinda lango lao kama mboni ya jicho, lakini walijikuta wakipigwa bao katika nusu ya kwanza, kwa kombora la Philipp Lahm wa Ujerumani.
Hata kusawazisha kwao goli kupitia kwa Georgios Samaras hakukuwasaidia sana, kwani hatimaye Wajerumani waliwazidi ujanja na kuwafunga mabao 4-2.
Pengine kati ya timu zote kwenye robo fainali, Ufaransa ndiyo ilikuwa na kibarua kigumu zaidi, maana ilikwaana na Hispania – mabingwa wa dunia. Le Blues walijitahidi kutojihami sana, lakini walirejeshwa golini na pasi za uhakika za wachezaji wa Hispania. Hata hivyo jasho liliwatoka Hispania kuweza kutanua uwanja, na hawakufanya kama ambavyo wangetaka.
Kujihami kwaweza kuonekana kama njia nzuri, lakini matokeo mara nyingi huwa dhidi ya timu dhaifu, kwa sababu timu imara itawavuta wachezaji pinzani kinamna na kupachika mabao, au walau moja. Hayatokei ya Chelsea mara nyingi.
Mlinzi wa kulia wa Jamhuri ya Czech, Theodor Gebre Selassie aling’ara vyema mashindanoni, na kwa karibu muda wote wa mchezo alimwangalia kwa umakini Ronaldo wa Ureno.
Hata hivyo, ukijua huu na wenzako wanajua huu, Ronaldo alijificha nyuma ya Gebre Selassie ghafla, akapata mpira na ni hapo alipofyatua fataki na kuwa bao pekee la mchezo na ushindi kwa Ureno.
Ujerumani ilishaanza kupewa nafasi kubwa ya kuchukua kombe badala ya Hispania, kwa sababu vijana wa Kocha Joachim Loew walionyesha soka nzuri ya kushambulia kwa nguvu.
Hakika yao ilikuwa soka ya kusisimua na aina ambayo wadau wa kandanda hupendelea, lakini walipofika kwa Italia, walilazimika kufunga breki zao, na watabiri wakageuka vinyonga, wakasema Italia ndiyo bora.
Wataliano waliwafunika Wajerumani kwa kila namna, hasa kwa mabao mawili ya mapema ya mchezaji wa Manchester City aliyetokea Afrika, Mario Balotelli.
Mchezaji wa zamani wa Newcastle na timu ya taifa ya Uingereza, Alan Shearer alisikika akisema baada ya mechi ya fainali kwamba Hispania ndiyo timu bora zaidi duniani, hata kama kuna wanaozungumzia mambo ya Brazil ya enzi za Pele.
Bosque amejiwekea rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kuongoza timu iliyotwaa ubingwa katika Kombe la Dunia, Ubingwa wa Ulaya na Ligi ya Mabingwa.
Na katika usiku ule wa kukumbukwa wa Hispania kutawazwa tena kuwa mabingwa wa Ulaya, kipa wao, Iker Casillas alitokea kuwa kipa wa kwanza kuamkia kwenye karne ya ushindi wa kimataifa.
Pamoja na mengine yaliyojitokeza kwenye michuano hii, ukweli ni kwamba imeiongezea Hispania rekodi kwa kiasi kikubwa.
Sasa ni timu pekee iliyopata kushinda makombe makubwa kwa mara tatu mfululizo; hayo yakiwa ni Euro 2008, Kombe la Dunia 2010 na sasa Euro 2012.
Rekodi nyingine ni kwamba katika mechi zao 12 zilizopita katika Ubingwa wa Ulaya, Hispania haijapata kufungwa katika dakika 90. Ilishinda mara tisa na kutoka sare mara tatu, ikiwa nayo ni rekodi mpya kwenye mashindano hayo.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Hispania haikukubalia kufungwa hata bao moja kwenye mechi zao tano za mwisho kwenye mashindano hayo. Walikuwa na wastani wa pasi 626.3 kwa mechi.
La Roja hawa hawa kwa upande wa kumiliki mpira wana wastani wa asilimia 60.03 kwa mechi, kiwango kikubwa kuliko timu nyingine tena.
Hispania wanajulikana kwa aina yao ya soka ya kutaka kuumiliki mpira kwa mchezaji wao kubaki nao ama kwa kupeana pasi, hata kama ni kumrejeshea golikipa wao na si kuzuzuka na kufanya mashambulizi bila mpango. Ni mtindo unaotumiwa na timu yake ya Barcelona pia.
Casillas sasa amelingana na Edwin van der Sar kwa rekodi ya kutoachia bao katika mechi tisa za mashindano hayo.
Fainali ya Jumapili ilikuwa mechi ya 100 kwa Casillas kushinda kati ya 137 za kimataifa alizopata kucheza. Anashikilia rekodi ya dunia ya kutofungwa bao katika mechi 79.
David Silva ametokea kuwa mchezaji aliyeshiriki katika kuipatia timu mabao mengi zaidi mwaka huu, kwani alifunga mawili na kusababisha matatu.
Katika mechi yao ya fainali na Italia, Hispania walimaliza wakiwa wanamiliki mpira kwa asilimia 52, ambapo La Roja walikuwa na pasi 529 dhidi ya 451 za Azzuri.
Mechi hiyo ilikuwa na rekodi nyingine ya aina yake, kwani Juan Mata wa Hispania alikuwa mchezaji wa akiba aliyeingia na kufunga goli haraka zaidi – ilikuwa baada ya dakika moja na sekunde 14 tu.
Fernando Torres naye alijipatia rekodi yake, akiwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye mechi mbili za fainali ya Euro.
Antonio Cassano wa Italia amevunja rekodi ya kuwa mchezaji ambaye nafasi yake uwanjani ilichukuliwa mara nyingi zaidi kupisha mwingine, akiwa ametoka mara nane.
Alivunja rekodi hiyo alikuwa akishikilia pamoja na Dennis Bergkamp na Mario Gomez. Rekodi nyingine ni kwamba timu zote mbili manahodha kwenye fainali walikuwa magolikipa – Casillas na Gianluigi Buffon. Rekodi nyingine kama hiyo ilikuwa kwenye fainali ya mwaka 1934 ambapo Italia iliwakilishwa na Giampiero Combi huku Czechoslovakia akiwa Franta Planicka.
Hii ndiyo michuano iliyozalisha magoli mengi zaidi ya kichwa, yaliyofikia 22 kuliko fainali nyingine zote za Ulaya.
Tangu mwaka 1992 hadi sasa, imewekwa rekodi kwamba hakuna mchezaji aliyefanikiwa kufunga zaidi ya magoli mawili.
Haikuwa ajabu sana kwa Poland na Ukraine kuaga mashindano mapema, kwa sababu rekodi inaonyesha kuwa timu tano kati ya saba zilizoandaa mashindano yaliyopita zilitupwa nje kwenye hatua ya kwanza ya makundi.
Hao ni pamoja na waandaaji wenza wa 2008 ambao ni Austria na Uswisi. Hata hivyo Poland imejiunga na Austria kwa kutoshinda walau mechi moja kwenye kundi lake.
Mchezaji wa Ugiriki, Giorgos Karagounis ametoka na rekodi ya aina yake, kwa kupewa kadi nane za njano kwenye mechi 10, zikiwa ni nyingi kuliko za mchezaji mwingine yeyote kwenye mashindano kama hayo.
Ama kwa Uingereza iliyotolewa na Italia kwenye robo fainali, ilitoka na karekodi kadogo ambako pasi zake nyingi zaidi zilikuwa kati ya golikipa wake, Joe Hart na Andy Caroll. Itakumbukwa siku hiyo England walicheza kwa kujihami zaidi.
Italia waliichezesha kwata England, wakitoka na jumla ya pasi 815 dhidi ya 320 za England. Waliishia kwa sare, ndipo Italia ikaja kuwatoa England kwa mikwaju ya penati.
Katika mashindano hayo, Miroslav Klose alifikisha idadi ya magoli 64 katika mechi za kimataifa, yakiwa ni manne pungufu ya Gerd Muller anayeshikilia rekodi.
Limchukua mshambuliaji wa siku nyingi wa Jamhuri ya Czech, Milan Baros dakika 217 kabla ya kufanikiwa kulenga mkwaju golini ambao hata hivyo haukuwa goli.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Uholanzi kushindwa kufuzu hatua ya makundi kuingia robo fainali. Ureno imeendeleza wimbi lake la kuingia robo fainali kwa mara zote sita ilizoshiriki mashindano hayo.
Ireland imeisogelea Yugoslavia ya 1984 kwa kufungwa mabao mengi zaidi, ambapo mwaka huu Ireland ilipigwa tisa wakati Yugoslavia ilichakazwa 10.
Wayne Rooney alimaliza ukame wa dakika 673 bila goli alipoifungua England kwa kichwa, wakati magoli manne kati ya matano ya timu hiyo yalitokana na krosi.
Andriy Shevchenko alifunga mabao mawili dhidi ya Sweden licha ya kuwa ameumiliki mpura kwa sekunde 15 tu.
Cristiano Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza wa Ureno kufunga mabao katika mashindano makubwa matano, ambayo ni Euro 2004, 2008 na 2012 pamoja na Kombe la Dunia la mwaka 2006 na 2010.
Euro 2012 imemalizika, timu zimerejea makwao na tayari nyingine zimeanza kujipanga upya, zikiweka mikakati na baadhi zikiadhibu waliovuruga mambo.
Kwa Hispania, sherehe zitachukua muda kumalizika, kwa sababu ya historia waliyoweka wachezaji na kocha wao; walipokewa na maelfu ya wananchi, na kutembeza kombe kwenye basi la wazi kwa saa mbili unusu kabla ya kupokewa kwenye viwanja vya Jiji la Madrid.
[email protected]
Comments
Loading…