in ,

EPL WIKIENDI HII:


CHELSEA WANAWAWINDA SPURS

Mabingwa watetezi, Chelsea wanajaribu kuwafukuza Tottenham Hotspur kutafuta nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Kuna pengo la alama 5 kati ya timu hizi mbili za jijini London zikiwa zimesalia mechi nne kwa kila timu kabla ya msimu kufikia tamati. Chelsea watakuwa wageni wa Swansea Jumamosi ndani ya uwanja wa Liberty kusaka alama tatu muhimu.

Vijana hawa wa Antonio Conte walishaonekana kuwa nje ya vita ya kuwania nafasi ya nne wiki chache zilizopita lakini michezo miwili waliyoshinda na baada ya Spurs kupoteza mchezo mmoja na kutoa sare mwingine sasa kumebakia alama 5 pekee zinazowatenganisha. Ushindi dhidi ya Southampton wiki iliyopita uliwapeleka Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA na pengine hili limewaongezea hali ya kujiamini kuelekea mchezo wa Jumamosi.

Mauricio Pochettino atavaana na Watford nyumbani Jumatatu. Kikosi chake kinalazimika kutafuta ushindi kwenye mchezo huo ili kuepuka kuwakaribisha Chelsea karibu zaidi na nafasi ya nne ambayo wanaishikilia wao kwa sasa. Kushindwa kutinga kwenye fainali ya Kombe la FA baada ya kupokea kipigo cha 2-1 kutoka kwa Manchester United wiki iliyopita huenda kumedhoofisha ari ya kikosi cha Tottenham ambacho hakijashinda taji lolote kwa miaka 10 sasa.

WENGER KUIAGA OLD TRAFFORD

Arsène Wenger, na José Mourinho

Baada ya kuiwezesha Arsenal kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu 19 mfululizo Arsene Wenger anakwenda kuhitimisha wakati wake ndani ya klabu hiyo huku akielekea kushindwa kuiwezesha kumaliza kwenye nafasi nne za juu kwa msimu wa pili mfululizo. Ni safari yake ya mwisho kuitembelea Old Trafford kama kocha wa Washika Bunduki hao wa London.

Mchezo wa Jumapili baina ya timu hizi ndani ya Old Trafford hauna chochote cha maana kwa yeyote. Hata hivyo kimahesabu Manchester United bado hawajajihakikishia kuwemo kwenye nafasi nne za juu na hivyo wanahitaji alama 2 kwenye michezo minne iliyosalia ili kupata uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Pia Mourinho amenukuliwa mara kadhaa hivi karibuni akisisitiza nia yake ya kumaliza kwenye nafasi ya pili. Hivyo anatarajiwa kuupa uzito mchezo huo.

Kwa upande wa Arsene Wenger mchezo huu haumpi ulazima wa kutafuta ushindi. Analazimika kupumzisha nyota wake kadhaa muhimu kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Europa dhidi ya Atletico utakaopigwa Alhamisi ijayo baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani. Aubameyang hata hivyo anatarajiwa kuongoza mashambulizi dhidi ya Manchester United kwa kuwa hana uhalali wa kucheza Ligi ya Europa.

Uhasimu baina ya timu hizi mbili umeleta msisimko mkubwa kwenye Ligi Kuu ya England kwa miongo miwili ya karibuni hasa kipindi cha Sir Alex Ferguson dhidi ya Arsene Wenger. Mchezo wa Jumapili unakosa uzito wa kutosha lakini unabaki na kiasi kikubwa cha mvuto kwa kuwa unabeba kumbukumbu nyingi za michezo mingi iliyopita ya kusisimua baina ya timu hizi zenye historia kubwa ndani ya Ligi Kuu ya England.


VITA YA KUSHUKA DARAJA

West Bromwich Albion wapo kwenye hatari kubwa ya kushuka daraja wikiendi hii huku Stoke City na Southampton wakiwa vibarua vya kupigana kujaribu kujinasua kutoka kwenye ukanda wa kushuka daraja. West Bromwich wanaburuza mkia kwenye jedwali la EPL wakiwa na alama 25 chini ya Southampton na Stoke City kila moja ikiwa na alama 29.

Ni matokeo ya ushindi pekee kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Newcastle United ya mwalimu Rafael Benitez yanayoweza kuwaepusha West Bromwich kushuka daraja wikiendi hii. Hata hivyo ushindi kwenye mchezo huo utakaopigwa ndani ya dimba la St. James Park unatarajiwa kuwachelewesha kushuka daraja na si kuwaepusha moja moja.

Mwalimu wa Southampton Mark Hughes naye ana kibarua kigumu cha kupambana kuibakiza timu yake kwenye Ligi Kuu ya England. Ana kazi ya ziada ya kufanya ili kuepuka kuweka rekodi ya kufundisha klabu mbili zilizoshuka daraja msimu mmoja. Southampton waliobaki na michezo minne wanawakaribisha Bournemouth Jumamosi kufuatia sare waliyoipata kwenye mchezo uliopita dhidi Leicester City.

Timu ya zamani ya Mark Hughes, Stoke City itacheza dhidi ya Liverpool ndani ya dimba la Anfield. Liverpool pengine hawana cha kupoteza kwenye mchezo huu lakini kufuatia matokeo mazuri kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya AS Roma huenda wataweka kikosi chenye nyota muhimu na hasa Salah mwenye uchu wa kuvunja rekodi zaidi za mabao.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MAENEO MUHIMU KWENYE MECHI YA SIMBA NA YANGA

Tanzania Sports

KWANINI YANGA ITASHINDA MBELE YA SIMBA