SIMULIZI za msimu wa soka wa Ligi Kuu England (EPL) 2018/19 zimeisha kwa habari zile zile za Liverpool kwamba wamekuwa wakifanya vyema lakini kombe hawapati.
Ni kama masuala ya upasuaji, ambapo madaktari nguli wanaweza kutoka kwenye chumba cha upasuaji na kuwaeleza mwenye mgonjwa wao kwamba upasuaji ulikuwa wa mafanikio makubwa lakini mgonjwa alifariki dunia.
Maana ya hiyo ni kwamba taratibu zote za kumwandaa mgonjwa, ukusanyaji vifaa pamoja na zoezi zima la upasuaji vilienda kwa mujibu wa taratibu na maadili ya utabibu, mbaya tu ni kwamba mgonjwa alipoteza maisha yake.
Manchester City wametetea ubingwa wao kwa mara ya pili, ukiwa ni msimu wa tatu kwa kocha Pep Guardiola kuwa nao Etihad Stadium, na huyu ndiye Guardiola tunayemjua, tangu Baracelona hadi Bayern Munich.
Liver walisumbua sana lakini wameshindwa kwa alama moja tu, wakifunga jamvi wakiwa na alama 97, kama kawaida Jurgen Klopp akionesha kutosikitika kivile, japo alikuwa na hamu nay eye anyanye kombe.
Wapo wanaosema kwamba Klopp ni mmoja wa makocha wasiokuwa na bahati zaidi katika EPL kwa soka ya nyakati hizi, kwa jinsi makombe yanavyomponyoka huku akiwa na kikosi kipana.
Chelsea waliosuasua hatimaye walijiimarisha katika dakika za mwisho chini ya Maurizio Sarri, na kufanikiwa kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) sambamba na Tottenham Hotspur.
Hiyo pia ilitokana na kuzorota kwa Arsenal waliofungwa mechi hovyo kuelekea mwisho wa ligi hiyo, wakati Manchester United kama walivyotarajiwa, wamekuwa nje ya nne bora na kwao na Ligi ya Europa mwakani.
Wakati hali ikiwa hivyo huko juu na wengine hapo katikati wakiwa kimya, kule chini wameshuka daraja akina Huddersfiend, Fulham na Cardiff.